WANDISHI WA HABARI NCHINI, WASHAURIWA KUJALI USALAMA WAO KWANZA


NA MARYAM NASSOR,

WAANDISHI wa habari nchini, wametakiwa kuangalia usalama wao kwanza, kuliko kitu chengine wakati wakitimiza majukumu yao ya kila siku.

Wito, huo umetolewa na ndugu Suleiman  Omar Seif   wakati  akichangia mada katika kikao cha kukusanya maoni ya Wandishi wa Habari wa Zanzibar, juu ya mradi wa Uwajibikaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) huko katika ukumbi wa Kidongo chekundu Unguja.

Amesema kuwa,  hakuna kitu   kizuri na chenye thamani  kwa mwandishi  kama kujali usalama wake, kwanza kwani kuna wandishi ambao wameshawahi kufikwa na masahibu mbali mbali wakiwa kazini, hivyo ni vizuri kuchukuwa tahadhari hiyo.

“ Hakuna kitu kizuri kwa mwandishi kama kujali usalama wake,kwanza na ukitokezewa na chochote basi , waarifu wenzako ili wajuwe jinsi ya kukulinda “ alishauri.

Nae, Mtaalamu  elekezi wa mradi wa Uwajibikaji kutoka MCT,  Kajubi Kajanga , amewataka wandishi wa Zanzibar kutoa maoni yao kuhusiana na mradi huo, kwani unategemea kuanza mapema mwakani   hapa Zanzibar kuliko sehemu,nyengine za Tanzania  bara.

Aidha, amesema kuwa, ni vyema Zanzibar ikawa na sheria ya haki ya  kupata Habari , ili uwe rahisi kwa wandishi kupata Habari kwa urahisi bila ya pingamizi zozote  kutoka kwa mamlaka husika.

Aidha ameshauri kuwa, nini kifanyike katika kuondoa umasikini katika vyombo vya Habari nchini  hususani vya Zanzibar ambavyo, vinategemea matangazo ili vijiendeshe .


Nae, mwandishi mkongwe  na mjumbe wa ZAMECO, Salim saidi amesema kuwa,  ni miongo miwili sasa tokea waanze kudai sheria rafiki  ya Habari, bila ya mafanikio.

Amesema kuwa,mbona  sheria nyengine zinachukuwa miezi sita au mwaka kurekebishwa kama sheria ya uchaguzi na sheria ya huduma za posho kwa wawakilishi,ugumu wa  sheria za Habari kurekebishwa uko wapi.

“ Ni miongo miwili sasa, tunadai sheria rafiki ya Habari bila ya mafanikio, lakini tunashuhudia sheria nyengine zinachukuwa miezi sita au mwaka, kurekebishwa ugumu uko wapi kwenye sheria hii” amehoji Mr Salim.

Nae, mwandishi  wa Habari  wa  DW Zanzibar, Salma Said  akichangia mada katika kikao hicho,alisema usalama wa waandishi bado ni mdogo, wandishi wana hofu kutokana na kuwa hakujapatikana  sheria rafiki ya Habari ambayo itawalinda hasa kipindi cha uchaguzi  mkuu mwakani  2025.

Kikao hicho, cha siku moja cha kujadili na kutoa maoni ya mradi wa Uwajibikaji , ambao  ni wa miaka sita na unatarajiwa kuanza mapema  mwakani, umewashirikisha wandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali  nchini na wadau wa habari.

No comments

Powered by Blogger.