''YAKIKUFIKA MAFIKO MOYO UPE AMINIKO LISILO MWISHO HALIPO'' KAULI YA MTUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA.

 

NAMARYAM NASSOR 

MAHAKAMA Kuu ,iliyopo  Tunguu Zanzibar, imemuhukumu kijana Abrahman Ismail Soli mwenye umri wa Miaka 33 mkaazi wa Kilosa, Mkoa wa Morogoro Tanzania bara,  kutumikia kifungo Cha miaka 15 Chuo cha Mafunzo  Kwa kosa la kusafirisha  dawa za kulevya.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji  Mohamed Ali Mohamed amesema  mshtakiwa huyo, ametiwa hatiani  baada ya  mahakama kujiridhisha, na ushahidi uliyotolewa na upande wa mashtaka , uliyoongoza na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ali Amour.

Jaji Mohamed, alisema kuwa mshtakiwa huyo, mkaazi wa Kilosa,alikamatwa  Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Amaan Abeid Karume, akisafiri kuelekea  Dubai , alipatikana na mafurushi 10 ya bangi akiwa ameyatia kwenye Begi la kusafiria.

Kesi hiyo, yenye namba 82  ya mwaka 2023 ,  jumla ya mashahidi nane walisikilizwa kwa upande wa Mashtaka na upande wa utetezi  kulikuwa na shahidi mmoja ambae ni  mshtakiwa.

Aidha, mshtakiwa huyo, siku ya utetezi wake alisema msemo  ufuatao" Yakikufika mafiko moyo upe aminiko lisilo mwisho halipo, mwisho wa kujitetea.

Awali Ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka Ali Amour, kuwa mnamo siku ya tarehe 10/05/2023  majira ya saa 1:30 usiku  huko, uwanja wa Abeid Amaan Karume (Terminal 3)  bila ya halali alipatikana akisafirisha mafurushi 10 ya madawa ya kulevya aina ya bangi, yenye uzito wa kilogram 2.55 kutoka Zanzibar  kuelekea Dubai kupitia shirika la ndege la fly Dubai.

Mtuhumiwa  huyo, alishtakiwa Kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya , kinyume na kifungu Cha 21 (1) (a) Cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar, Sheria Namba 8 ya mwaka 2021 Sheria za Zanzibar.


    Mwisho

No comments

Powered by Blogger.