RUSHWA YA NGONO SUALA LINALOWARUDISHA NYUMA WANAWAKE KUWA VIONGOZI
Rushwa ya Ngono,suala linawarudisha nyuma wanawake kuwa Viongozi
Na –Maryam Nassor.
Zanzibar: ‘’Niliishiwa
na nguvu wakati aliponiambia kama unaitaka hii nafasi basi lazima tukutane
kimapenzi kwanza ndio uiptae”Amesema Sharifa.Huku kitu pekee kilichomjia kichwani
kwake ni kuliweka jambo hilo liwe siri, libaki
milele kwenye shimo la nafsi yake, hakutaka mume wake ajuwe nini
kilimkuta hata akaachana na siasa mwaka 2015 labda ingeweza kumnusuru na wimbi la aibu na fedheha.
Hii ni baada ya kutakiwa kimapenzi
na kiongozi wake ndani ya chama, katika kikao cha kujadiliwa ili agombee nafasi
ya mjumbe wa kamati kuu ya Chama hicho huko Wilaya ya Chake chake Mkoa wa
Kusini Pemba.
Sharifa*39 mama wa watoto
wanne,anayeishi na mume wake Kisiwani Pemba, aligombea nafasi ya ujumbe w
Kamati Kuu ya Taifa ya Chama, Wilaya ya Chake Chake mwaka 2015, katika kikao cha kujadiliwa aliitwa na
kiongozi wake wake na kumpa sharti kama anaitaka nafasi hiyo kwanza wakutane
kimapenzi.
“Maneno yake yalinivunja moyo na
nikajiona kama nimevuliwa nguo,aibu niliona na nikajihisi kama sijui hata
nisemeje mimi” Aliendelea kusema Sharifa mwaka 2015 ulikuwa mgumu kwake, baada
ya ndoto yakee ya kuwa kiongozi kuishia hapo kutokana na ukatili wa kisaikolojia uliopitia.”Sikuwa
na ujasiri wa kumuhadithia mtu kadhia hiyo iliyomkuta mpaka nikaachia ngazi,na
kujitoa katika kinyanj’anjiro hicho, na hilo lilipelekea kupata matatizo ya kisaikolojia.” Aliishia hapo
Sharifa.
Udhalilishaji wa kijinsia na suala
linawatafuna wanawake waliopo kwenye vyama vya sasa hii Tatu*40 ambae
alikatisha ndoto zake za kuwa kiongozi mwaka 2020 Wilaya ya Kaskazini ‘A’
Unguja.
Tatu mama wa watoto wawili mama wa
nyumbani mkaazi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, ni miongoni mwa wanawake
waliokatisha ndoto zao za kuwa viongozi, kwa sababu ya ukatili wa kisaikolojia
uliompata wakati anagombea.
Sababu kubwa ya kukatisha ndoto
zake, ni baada ya kukumbwa na ukatili wa
kisaikolojia , baada ya kutakiwa kimapenzi na msaidizi wake wa kampeni na
kuliweka jambo hilo kuwa siri, kwa kuhofia ya aibu na fedheha kutoka kwa
wanajamii.
‘’Sikuwa najua kama ningekutwa na
mkasa ule, kwani yule mtu aliyenitaka kimapenzi ni mtu ambae, anaaminika na
mume wangu, nilihofia hata kumuhadithia kadhia ile” Amesimulia huku akiinamisha
sura kwa aibu.‘’Nilipata msongo wa mawazo, nilikuwa nakaa ndani nalia pekee
yangu, nikihofia siri ile kuja kujulikana, sura yangu nitaiweka wapi’’ Amehoji
Tatu.
Utafiti uliofanya na Wizara ya
Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na Makundi Maalum, imeonesha idadi kubwa ya wanawake na wanaume wanaofanyiwa ukatili wa kingono, kimwili na
kisaikolojia.Matokeo ya utafiti huo, wa SIGI -2022 yanaonesha asilimia 55 ya
wanawake wenye umri wa miaka 15-49, wameshawahi kufanyiwa aina moja wapo ya
ukatili.Ambapo, asilimia 16 wameshawahi kufanyiwa ukatili wa kisaikolojia, asilimia
15 ukatili wa kimwili na asilimia 7 wameshawahi kufanyiwa ukatili wa kingono.
Tatu Ali Abass ni daktari na mwanasaikolojia wa maswala ya afya ya akili,
Hospitali ya Wilaya Vitongoji Mkoa wa
kusini Pemba,amesema madhara makubwa huwapata watu wanaopata ukatili wa kisaikolojia,
ikiwemo msongo wa mawazo na endapo hawatatibiwa mapema, wanaweza wakapata
ugongwa wa afya ya akili na ugongwa wa sonona.“Wathirika wa vitendo vya ukatili
wa kisaikolojia, wamekuwa wagumu kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo, kutokana
na kuhofia aibu na fedheha kutoka kwa wanajamii ila kusema ni moja wapo ya
tiba”Amesema Daktari Tatu.
Ripoti ya sensa ya watu na makaazi
ya Tanzania ya mwaka 2022 inaonesha kuwa Zanzibar ina wakaazi 1,889,773 kati ya
hao, wanaume ni 915,492 na wanawake ni 974,281.Hii, ina maana kwamba wanawake
ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar, lakini wingi wao huo hauonekani
katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi kutokana na vikwazo vingi lakini
pia, ukatili wa kisakolojia.
Anna Athanas Paul, ni Naibu Waziri
wa wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema tathimini
iliyofanya na wizara hiyo, katika taasisi mbalimbali imeonesha kuwa wanawake
bado wapo kidogo katika nafasi za Uongozi, ukilinganisha na wanaume jambo
ambalo linahitaji kuangaliwa.‘’Takwimu
zilizokusanywa na wizara kutoka taasisi mbalimbali kwa mwezi machi mwaka 2024,zinaonesha ni
asilimi 30 tu ya wanawake ambao wako
katika uongozi, ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 70’’ Amesema Naibu Waziri
Anna.
Anna, ameongeza kuwa Serikali inaendelea
na jitihada katika kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya 2050 na mpango
wa Maendeleo (ZADEP) 2021/2026 ambapo lengo katika nafasi za uongozi ni kufikia
50/50.
Ziko Mamlaka ambazo zinahusika na
maswala ya rushwa na uhujumu Uchumi- ZAECA, kupitia Afisa Elimu wake Yussuf
Juma Suleiman amesema kuwa, ‘’ Sheria ya kuzuia Ruchwa na uhujumu Uchumi
Zanzibar, sheria namba 5 ya mwaka 2023 kifungu cha 52, kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo hivyo’’
Amesema Yussuf huku akiwataka wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi
kwanza kusoma elimu ya uraia, ili kutambua haki zao bila ya kubabaishwa na mtu.
Chama cha wandishi wa habari
Wanawake Tanzania Zanzibar,-TAMWA ZNZ ni
Taasisi isiyo ya kiserikali,inayojishuhulisha na maswala ya utetezi wa haki za mtoto wakike, Mkurugenzi mtendaji wa
TAMWA ZNZ, Dk Mzuri Issa amesema wanawake wanaogombea nafasi za uongozi
wanakumbwa na vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia na kisaikolojia.”Wanawake
wenye nia ya kugombea wasivunyike moyo na wawe majasiri ili kuongeza wingi wao katika nafasi za uongozi mwaka 2025
na kuripoti vitendo hivyo katika taasisi husika ili waweze kupata msaada”
Amesema Dkt Mzuri
Mohamed Ali Ahmed, ni Naibu Msajili
wa vyama vya Siasa Tanzania,kwa upande wa Zanzibar,amesema kuongezeka kwa
kifungu cha 10 C ndani ya sheria ya vyama vya siasa nchini, kinatoa nafsi kwa
wanawake kuongeza ushiriki wao,na kuwajibika kwa vyama kwa kuwa na sera ya
jinsia muda wote, kwani hapo awali havikupaswa vyama kuwa na sera hiyo.”Wanawake
wanatakiwa kuwa wajasiri na wenye uthubutu ili kuongeza wingi wao katika nafasi
za uongozi, na kuviripoti vitendo vyote vya udhalilishaji na ukatili wa
kijinsia vinavyowakumba, kwani kugombea nafasi za uongozi ni haki ya kila mmoja
raia wa Tanzania’’ Amemaliza Mohamed.
Post a Comment