DHANA YA MICHEZO KWA MAENDELEO ILENGE PIA USHIRIKISHWAJI WA TIMU ZA WATU WENYE ULEMAVU

 



NA MARYAM NASSOR

  Dhana ya michezo kwa maendeleo , imekuja kuwapa hamasa vijana wanaotaka kujiajiri kupitia sekta ya michezo bila ya kubagua  jinsia zao .

Wakiwa na imani kuwa,  ajira ni ngumu kupatikana lakini kupitia fursa zinazotokana na michezo  wanaweza ‘ kutoboa’ kimaisha.

Kwa hapa Zanzibar kuna vyama 42 vya michezo, vilivyosajiliwa na ofisi ya mrajisi wa vyama vya michezo, vikiwemo vyama vya michezo ya watu wenye ulemavu.

Katika makala haya mwandishi, anaangazia umuhimu wa kushiriki michezo kwa maendeleo, kwa watu wenye ulemavu.

  Michezo wanayoshiriki  timu za watu wenye ulemavu hapa Zanzibar , zinakabiliwa  na changamoto lukuki ingawa wakienda kuiwakilisha nchi nje ya nchi, wanarudi na medali za dhahabu au fedha.

Kassim Mohamed Ramadhan, mchezaji wa timu ya watu wenye ulemavu wenye mguu mmoja na mkono mmoja, akizungumza na mwandishi wa makala haya, amesema michezo imemrudishia tabasamu lake tena.

Amesema, miaka  13 iliyopita baada ya kupata ajali mbaya iliyopelekea kukatika kwa mguu wake mmoja, akiwa na umri wa miaka 7 alikuwa mtoto mnyonge sana.

 Alisema kuwa,  alikuwa katika hali ya ulemavu na watu katika kijiji chao, walimtenga lakini hakukata tamaa alisoma kwa bidii na kujiunga katika timu ya watu wenye ulemavu.

Amesema,  baada ya  kukatwa mguu hakuwa na matumaini yoyote katika maisha yake, lakini kwa sasa michezo ndio uponyaji wake na sehemu inayompa matumaini mapya.

“ kwangu mimi naamini kuwa, michezo ni ajira lakini bado kwa sisi watu wenye ulemavu hatujafikia huko, lakini mimi naichukulia kama uponyaji wangu na sina mawazo nikishiriki michezo”alisema.

Aidha alisema kuwa, mwaka jana alishiriki michezo ya AFCON alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa cha tembo warrious walipoenda nchini misri na kutokea mshindi wa tatu kwa  timu ya Tanzania.

“Kutoka kutengwa na jamii hadi kusimama kwenye jukwaa na kupeperusha bendera ya nchi, ama kweli hiyo ndiyo nguvu ya michezo “alisema.

Aidha, aliiomba Serikali kama mdau nambari moja kuzidi kufanya uwekezaji katika  sekta  ya michezo, ili ile dhana ya michezo kwa maendeleo izidi kuonekana kwa wote.


Nae, kocha timu ya watu wenye  ulemavu wa mguu mmoja na mkono mmoja, Hassan Haji Silima, alisema  bado timu za watu wenye ulemavu zinakabiliwa na ukosefu wa kiwanja maalum cha kufanyia mazoezi.

“ Timu za watu wenye ulemavu, hatuna kiwanja maalum cha kufanyia mazoezi, mwanzo tulikuwa tukifanyia uwanja wa Amaan ndani, tukahama wakati kinafanyiwa matengenezo na kwasasa bado hatujarudi tena kule” alisema.

Amesema kuwa, hawana ufadhili  wanaupata katika timu zao, hilo linawapelekea kufanya mazoezi mara chache kutokana na kuwa wachezaji wanakaa mbali na wenye  magari hawapendi kuwachukuwa watu wenye ulemavu.

 Nae,mwenyekiti wa timu ya special olympik ya Zanzibar( SOZ)  Saada Hamad Ali amesema kuna umuhimu mkubwa kwa watu wenye ulemavu kushiriki michezo kwa maendeleo.

Amesema kuwa,timu za watu wenye ulemavu zikishiriki kwenye mashindano zinafanya vizuri kuliko za wale waliyokuwa hawana ulemavu.

Lakini tatizo liliopo ni  kutengwa na kudharauliwa kwa timu hizo, kwani  washashiriki mashindano ya olympik mara saba nje ya nchi na mara zote  wanashinda  na wanarudi na medali. 

Aidha amesema kuwa, mwaka jana timu yao ilishiriki special olimpik na kutokea mshindi wa kwanza, nchini ugiriki na Rais wa Zanzibar alikwenda kuwaona wakati wako kule na kuahidi wakirudi waendee kumuona, lakini mpaka leo bado hawajafanikiwa kumuona kutokana na ahadi yake hiyo.

“Mwaka jana wakati tuko nchini Ugiriki, Rais Dk Mwinyi alikuwepo kule kwenye ziara zake za kiserikali na alikuja kutuona na kututaka tukirudi nyumbani, twende tukamuone  Ikulu na watoto wetu lakini huu ni mwaka  sasa ,kila tukienda kuulizia   utaratibu tunazungushwa huku na kule’’alisema.

Alisema kuwa, michezo ni muhimu hasa kwa kuimarisha urafiki baina yao, na kutekeleza mkataba wa haki  za watu wenye  ulemavu.


Aidha alisema kuwa, changamoto wanazokumbana nazo kabla ya kwenda mashindano hayo, ni  kuwa hawana fungu la bajeti ya timu zao, kwani hawajawahi kupatiwa fungu kutoka tasisi za umma tokea kuasisiwa kwa mashindano hayo mwaka 1988.

Nao, baadhi ya wazazi   wenye watoto walemavu,waliyozungumza na mwandishi wa makala haya, walisema kuwa michezo kwa watu wenye ulemavu ni muhimu mno.

Walisema kuwa, watu wengi wenye ulemavu ni wenye msongo wa mawazo kwani huwa hawashirikishwi katika mambo mengi ya kijamii, hivyo kukutana kwenye michezo ni jambo linalowapa faraja.

Na kuitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuendelea kuzisaidia timu hizo na kuwasaidia kutafuta wadhamini ili kuwe na ligi za mikoa na wilaya kama timu nyengine.

Hija Mohamed Ramadhani, mshauri wa maswala ya jinsia katika michezo kutoka shirika la Ujerumani (G IZ)hivi karibuni alipokutana na wandishi wa habari, alisema mradi wa michezo kwa maendeleo hapa Zanzibar  utaboresha mazingira mazuri ya mindombinu ya viwanja na inalengo la kujenga viwanja saba Unguja vinne na Pemba vitatu .

Lakini ipo haja kwa shirika hilo na taasisi nyengine kujitoa zaidi kudhamini ligi za timu za watu wenye ulemavu, ili kuwapa hamasa na kuiona hasa ile dhana ya michezo kwa maendeleo inavyofanya kazi kwani waswahili wanasema ‘ kuona  ndio kuaminii’.

                              MWISHO






No comments

Powered by Blogger.