USHIRIKISHWAJI KWENYE MICHEZO KWA WATU WENYE UALBINO BADO KITENDAWILI

NA MARYAM  NASSOR

JUMUIYA ya watu wenye ualibino Zanzibar imesema kutokushirikishwa ipasavyo kwenye michezo kunawanyima  haki yao ya msingi  ya kikatiba na fursa za ajira kupitia michezo.

Walisema kuwa, katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 12 (1) kimefafanua kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria lakini licha ya katiba kutamka hivyo,bado hawajapewa  nafasi katika michezo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisini kwao mjini Unguja katibu wa  Jumuiya hiyo Abdillah Salum Shaame, alisema wamekuwa  hawashirikishwi  kwenye michezo kama watu wengine waliyokuwa hawana ulemavu na kupelekea kukosa fursa za ajira kupitia michezo.

 Alisema, licha ya katiba  ya Zanzibar  kusema kuwa, watu wote ni sawa, lakini ukiangalia suala la michezo kwa watu wenye ulemavu bado hawajapewa nafasi ipasavyo kutokana na mitazamo ya watu kuona hawana uwezo huo.


Alisema kuwa, sera ya michezo ya mwaka 2018  imetamka nia njema ya serikali katika fursa za michezo lakini bado hizo fursa wao hazijawafikia kutokana na kuwa bado hawana mindombinu rafiki inayowafanya washiriki michezo.

 Alieleza kuwa ni wakati wa jamii kubadilika  na kuondokana na itikadi potofu na badala yake kuwashirikisha , watu wenye ulemavu kwenye michezo  ili kujipatia  kipato kupitia michezo.

 

 Aidha alisema kuwa, watu wenye ulemavu wanahaki ya kushiriki michezo kama  watu wengine, hivyo ni wajibu  wataasisi na wizara ya michezo  kuwashirikisha ili kukuza vipaji vyao.

“ Sisi watu wenye ulemavu hatushirikishi ipasavyo kwenye michezo kutokana na ulemavu wetu, lakini ni haki yetu na sisi kushirikishwa kwenye  michezo “ alisema.

Nae mchezaji katika timu ya  watu wenye ulemavu wa mguu mmoja na mkono mmoja Kassim Mohamed  amesema kuwa, kutokana na ulemavu waliyokuwa nao hawana kiwanja maalum cha kufanyia mazoezi na kupelekea kufanya mazoezi mara tatu tu kwa wiki.

‘’ hatuna kiwanja  maalum cha kufanyia mazoezi na kupelekea kufanya mazoezi mara chache sana kwa wiki” alisema.

Afisa mdhamini Wizara ya habari, vijana na michezo  Pemba, Mfamau lali Mfamau hivi karibuni  alisema wizara  hiyo,  imo kwenye mkakati wa kuboresha mindombinu ya  michezo ikiwemo kujenga  viwanja ili kuona watu wenye ulemavu wanaingia kwenye michezo.

                                 MWISHO



No comments

Powered by Blogger.