ZANZIBAR YALIPA KIPAUMBELE SUALA LA USONJI KATIKA AFYA YA AKILI NA MAENDELEO YA MTOTO
Na Maryam Nassor
WIZARA ya Afya Zanzibar
imesema suala la tawahudi (usonji) ni miongoni mwa masuala yanayopewa
kipaumbele, hasa linapohusiana na afya ya akili na maendeleo ya mtoto,
likihitaji muitikio wa kisera unaozingatia ushahidi wa kitaalamu pamoja na
ushirikishwaji wa sekta mbalimbali.
Akizungumza katika
kongamano la maadhimisho ya Siku ya Tawahudi Duniani, kwa niaba ya Kaimu Waziri
wa Afya Zanzibar, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mngereza Mzee Miraji, alisema
hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa jamii na kusogeza huduma karibu kwa wakati.
Amesema ,Serikali inaendelea kuimarisha mpango mkakati kwa kujumuisha huduma za uchunguzi wa mtoto katika ngazi ya msingi, pamoja na tiba ya usemi na viungo, ili kukabiliana na changamoto za usonji.
Akiwasilisha mada kuhusu
tawahudi, Daktari Bingwa wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dk.
Leonida Isidory Ngongi, alisema mtu mwenye usonji anahitaji msaada maalum
katika ukuaji wake.
Alifafanua kuwa, zaidi
ya asilimia 80 ya watoto wenye usonji wanaweza kugundulika wakiwa chini ya umri
wa miaka miwili, hasa katika hatua za awali za ukuaji ikiwemo kuchelewa
kuzungumza au kushindwa kushikilia kichwa vizuri.
Aidha, alibainisha kuwa
kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtoto mmoja kati ya 100 anaweza
kuwa na usonji. Aliongeza kuwa tafiti kutoka baadhi ya nchi za Afrika
zinaonesha kiwango cha asilimia 0.3 nchini Kenya na asilimia 2.3 nchini
Nigeria, huku Tanzania ikiwa haina takwimu rasmi kutokana na changamoto ya
ukusanyaji wa taarifa.
Dk. Ngongi amesema, hakuna sababu ya moja kwa moja inayosababisha usonji, lakini
vinasaba vinaweza kuchangia, hasa kwa watoto mapacha ambapo uwezekano wa wote
kuwa na hali hiyo ni mkubwa.
Aidha , alitaja uwepo wa magonjwa ya kurithi
kama vile selimundu na hali duni ya lishe kuwa miongoni mwa vihatarishi vinavyoweza kuchangia
hali hiyo.
Akieleza dalili za
usonji, amesema ni pamoja na changamoto za mawasiliano na mwingiliano wa
kijamii, kuchelewa au kushindwa kuzungumza, tabia za kurudia rudia, matatizo ya
mfumo wa fahamu pamoja na hasira za mara kwa mara.
Kwa upande wake,
Mtaalamu wa Tiba kwa Vitendo kutoka Hospitali ya Muhimbili, Coletha Gabriel
Kimario, amesema ni muhimu kwa watoto wenye usonji kusaidiwa kurejea katika
hali ya kawaida ya hisia ili waweze kushirikiana vizuri na wenzao.
Amesisitiza, umuhimu wa kuelimisha familia na walezi kuhusu namna sahihi ya kuwahudumia watoto hao, pamoja na kuhakikisha wanapata haki zao katika elimu na maisha ya kijamii kwa ujumla.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Bi. Salma Saadat, aliitaka serikali kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye usonji, ikiwemo kuboresha miundombinu ya elimu na afya ili kukidhi mahitaji yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zanzibar Autism Care and Support Organisation (ZACSO), Munawwarah Mahfoudh Haji, amesema lengo la taasisi hiyo ni kuongeza uelewa wa jamii, kuondoa unyanyapaa na kuhakikisha watoto wenye usonji wanapata haki zao.
Aliongeza kuwa , kongamano
hilo limelenga kuimarisha kampeni za uelimishaji kuhusu Tawahudi na kuitaka
serikali kuandaa mkakati maalum wa kuwatambua watoto wenye hali hiyo Zanzibar
pamoja na kulinda haki zao.
Kongamano hilo limeandaliwa na ZACSO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, likiwa na kaulimbiu isemayo: “Usonji na Ubinadamu, Kila Maisha Yana thamani.






Post a Comment