ZACSO YAHAMASISHA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA TAWAHUDI DUNIANI

Na Maryam Nassor

Taasisi ya Zanzibar Autism Care and Support Organisation (ZACSO) imeujulisha umma kuhusu maadhimisho ya Siku ya Tawahudi (Usonji) Duniani, yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 2 Aprili, kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu hali hiyo na kuhimiza ushirikiano katika kuwasaidia watu wenye tawahudi.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) Tunguu, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Munawarah Mahfoudh Haji, amesema kuwa tawahudi (usonji) ni hali ya ukuaji wa ubongo inayoathiri uwezo wa mtu katika mawasiliano, mahusiano ya kijamii pamoja na tabia.

Amesema kuwa, watoto na watu wenye tawahudi wanahitaji aina tofauti za msaada kulingana na mahitaji yao binafsi, lakini kwa uelewa sahihi, huduma stahiki na mazingira jumuishi, wana uwezo wa kuishi maisha yenye tija na heshima kama watu wengine katika jamii.

Aidha, amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Autism and Humanity, Every Life Has Value” (Tawahudi na Ubinadamu, Kila Maisha yana Thamani), inayolenga kusisitiza umuhimu wa kutambua utu, heshima na thamani ya kila mtu mwenye tawahudi, pamoja na kuhakikisha anapata haki sawa katika nyanja zote za maisha.

Ameongeza kuwa, kaulimbiu hiyo pia inahimiza jamii kuondokana na unyanyapaa na badala yake kujenga mazingira jumuishi yanayowawezesha watoto na watu wenye tawahudi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

 Amesema  kuwa ,kuna ongezeko la utambuzi wa watoto wenye dalili za tawahudi Zanzibar, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuelimisha jamii, kuimarisha huduma za afya na elimu jumuishi, pamoja na kupunguza unyanyapaa unaowakumba watoto hao na familia zao.

 Amesema ,Katika kuadhimisha siku hiyo muhimu, ZACSO imeandaa kongamano litakalofanyika Aprili 8, 2026, likiwakutanisha wadau kutoka sekta za afya, elimu, serikali, mashirika ya kiraia pamoja na jamii kwa ujumla.

Akieleza malengo ya kongamano hilo, amesema ni pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu tawahudi, kuhamasisha mtazamo chanya na jumuishi, pamoja na kuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto katika sekta za afya, elimu na jamii.

Aidha, ametoa wito kwa jamii, wazazi, walezi, wataalamu na wadau wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo na kuunga mkono juhudi za kujenga jamii jumuishi inayotambua na kuheshimu haki za watu wenye tawahudi visiwani Zanzibar.

Amesisitiza kuwa,  kwa pamoja, jamii inaweza kujenga mazingira yanayokubali tofauti na kutoa fursa sawa kwa kila mtu.

MWISHO

Top of Form

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.