SEKTA YA UTALII ZANZIBAR YACHANGIA ASILIMIA 30 YA PATO LA TAIFA
NA MARYAM NASSOR
WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga,
amesema sekta ya utalii ni mhimili muhimu wa uchumi wa Zanzibar, ikichangia
zaidi ya asilimia 30 ya Pato la Taifa na kutoa ajira zaidi ya 65,000.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara
ya Habari Maelezo kuhusu siku 100 za mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya
Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati
thabiti ya kukuza sekta hiyo kwa kuzingatia utalii endelevu, ubora wa huduma na
ushirikishwaji wa wananchi.
Amesema katika kipindi hicho cha siku 100, Wizara
imefanikiwa kutekeleza hatua mbalimbali, ikiwemo kuimarisha utalii wa mikutano,
matamasha, michezo na matibabu.
“Tumeshiriki na kuratibu matukio ya kimataifa kama vile
FITUR nchini Hispania, World Travel Market (WTM) London, Sauti za Busara,
pamoja na tamasha na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Hatua hizi
zimeendelea kuitangaza Zanzibar kimataifa na kuongeza ushindani wake,” amesema.
Aidha, amesema katika juhudi za kuongeza idadi ya watalii, Zanzibar imepokea watalii 273,773 kutoka mataifa mbalimbali, ikiwa ni ongezeko la asilimia 115 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020/2021.
Ameongeza kuwa muda wa ukaazi wa wageni umeongezeka kutoka
siku 6 hadi siku 8, jambo linalochangia kuongezeka kwa mapato na manufaa kwa
wananchi.
Kwa upande wa uwekezaji, amesema kumekuwa na ongezeko la
vyumba vya hadhi ya juu hadi kufikia zaidi ya 17,000, hatua inayolenga kuvutia
watalii wenye matumizi makubwa.
Sambamba na hilo, Wizara inaendelea kuelimisha wadau wa
sekta, kurasimisha huduma za “beach boys na beach girls”, pamoja na kuimarisha
usimamizi wa bahari kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu kupitia
mpango wa ‘Marine Spatial Planning’.
Katika kuendeleza utalii wa kijamii na vijijini
(Community-Based Tourism), pamoja na kuimarisha utalii endelevu, Wizara
imeendelea kutekeleza kampeni ya “Greener Zanzibar”, kuweka mfumo wa usimamizi
wa taka katika maeneo ya utalii, na kuandaa miongozo ya viwango vya kimataifa
vya utalii endelevu.
Zanzibar pia ni mwanachama wa Global Sustainable Tourism
Council (GSTC) kwa miaka miwili mfululizo na inaendelea kujenga uwezo wa
taasisi na wadau, ambapo taasisi hiyo hutoa miongozo ya viwango vya utalii
endelevu duniani.
Kutokana na mafanikio hayo, Zanzibar imepata tuzo ya kimataifa ya World Travel Awards kama kituo bora cha “Corporate Retreat” kwa mara ya kwanza, jambo linalothibitisha ubora wa huduma na mazingira ya uwekezaji.
Aidha, Zanzibar imefanikiwa kushinda kuwa mwenyeji wa
mkutano wa kimataifa wa Inter Island State Tourism Policy Forum (ITOP)
utakaofanyika mwaka 2027, utakaowaleta pamoja viongozi na wadau wa utalii
kutoka mataifa mbali mbali.




Post a Comment