WAANDISHI WA HABARI NCHINI WAMEHIMIZWA KURIPOTI MATUKIO YA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA VIJIJINI.


Na Maryam Nassor

Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuibua na kuripoti matukio ya udhalilishaji wa kijinsia yanayowakumba wanawake na wasichana, hususan katika maeneo ya vijijini ambako bado kuna mwamko mdogo wa kuripoti vitendo hivyo.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Bodi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), Bi. Hawra Shamte, katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa chama hicho, Tunguu, Unguja.

Amesema matukio ya udhalilishaji wa kijinsia yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, hasa katika maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi hushindwa kuripoti matukio hayo na hivyo kutokuchukuliwa hatua stahiki.

“Waandishi wa habari mna jukumu kubwa la kuibua na kuripoti matendo haya, yakiwemo mauaji na vitendo vya udhalilishaji, ili jamii iweze kupata uelewa na kuchukua hatua sahihi,” amesema Bi. Shamte.

Amefafanua kuwa, baadhi ya vitendo wanavyofanyiwa wanawake na wasichana ni pamoja na kushikwa sehemu za miili yao wakiwa kwenye vyombo vya usafiri, pamoja na kuibiwa mali zao hata na baadhi ya waume zao.

Kwa upande wake, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib, amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kuelimisha jamii kuhusu haki zao na kufuatilia kesi za udhalilishaji hadi mwisho ili kuhakikisha haki inapatikana.

“Ni jukumu lenu waandishi wa habari kuripoti matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na wasichana ili kujenga jamii salama,” amesema Khatib.

Naye Afisa Programu wa TAMWA ZNZ, Asya Hakim, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ‘Tunaweza Pamoja Kumaliza Udhalilishaji wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake na Wasichana’, unaotekelezwa katika mikoa miwili ya Zanzibar—Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.

Amesema lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na wadau wengine ili kusaidia kupunguza na hatimaye kumaliza matukio ya udhalilishaji wa kijinsia.

Ameongeza kuwa ,mradi huo unatekelezwa katika maeneo yenye matukio mengi ya udhalilishaji, ikiwemo maeneo ya usafirishaji, masoko na sehemu za kukaushia dagaa, ambako wanawake na wasichana hukumbana na vitendo hivyo mara kwa mara.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo kutoka Asalam FM na Zenji Post Blog wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi na kuripoti kwa ufanisi zaidi masuala ya kijamii.

Mafunzo hayo ya siku mbili yametolewa kwa waandishi 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari Zanzibar chini ya mradi wa Pamoja Tunaweza unaotekelezwa na TAMWA ZNZ, kwa lengo la kuendelea kuibua na kupambana na vitendo vya udhalilishaji  hasa vijijini.



Top of Form

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.