IIT MADRAS ZANZIBAR INATEGEMEA KUTEKELEZA PROGRAM YA KITAALUM PAMOJA NA ZUT.
TAASISI ya
Teknolojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) inategemea kuanza
utekelezaji wa programu za kitaaluma za pamoja katika masuala ya teknolojia kwa
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Zambia (ZUT).
Hayo
yamebainika kufuatia mazungumzo yaliyofanyika baina ya uongozi wa IITMZ na
uongozi wa ZUT ikiwa ni miongoni mwa hatua za ufatiliaji wa Hati ya Makubaliano
ya Maelewano (MoU) yalifikiwa na taasisi
hizo mbili mapema mwaka 2025.
Mazungumzo
hayo yaliyofanyika katika ofisi za IITMZ yameongozwa na Mkurugenzi Dhamana
IITMZ Prof. Brabhu Rajagopal pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ZUT Dk. Betty
Shitima Bweupe.
Akizungumza
juu ya ugeni huo Mkurugenzi Dhamana wa IITMZ Prof. Prabhu Rajagopal amesema
kuwa, ni furaha kubwa kwa uongozi wa ZUT kufika katika kampasi za IITMZ,
ikizingatiwa kuwa ZUT ni miongoni mwa vyuo vinavyoongoza katika elimu ya
teknolojia nchini Zambia. Na kuthibitisha kuwa, ameona maono makubwa kuelekea
kuendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili kusudi kuleta elimu ya
teknolojia iliyo bora ndani na nje ya nchi.
Ameongezea kwa kusema kwamba, kazi ya IITM
Zanzibar ya kupanua mipaka ya sayansi ya data na kuendeleza taaluma za kisasa
za uhandisi imepokelewa kwa hamasa kubwa na wajumbe wa ZUT.
“Tumekubaliana
kushirikiana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kubadilishana wahadhiri na
wanafunzi, hususan katika ngazi za Shahada za Uzamili na Uzamivu (Masters na
PhD), pamoja na kuimarisha ushirikiano wa utafiti kati ya nchi za Kusini mwa
Dunia (South-South Collaboration).
Ameongezea
kwa kuthibitisha kuwa, uwezo wa IIT Madras katika nyanja za vihisishi
(sensors), akili unde (AI) na roboti una umuhimu mkubwa kwa Ukanda wa madini wa
Copperbelt nchini Zambia ambako ZUT ipo.
Aidha, uwepo
wa wanafunzi wengi wa Zambia katika kampasi ya IITMZ umeifanya ziara hio kuwa
ya kipekee na ya kukumbukwa sana.
Akitoa maoni
yake juu ya ujio wa ugeni huo, Mkuu wa Taaluma wa IITMZ, Prof. A.K. Suresh,
amesema wamejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano wa kitaaluma kati ya IITMZ
na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Zambia (ZUT), yenye lengo la kuimarisha
maendeleo ya elimu ya juu na utafiti nchini.
Prof. Suresh
amesema kuwa licha ya ZUT kuwa taasisi iliyopo kwa miaka mingi, kama chuo kikuu
bado ni taasisi inayokua na yenye dira inayofanana na IITMZ katika kupanua
ubora wa elimu na tafiti.
Ameeleza kuwa fursa zilizobainishwa ni pamoja na kubadilishana wanafunzi, kubadilishana wahadhiri kwa ajili ya ufundishaji na utafiti, pamoja na utekelezaji wa miradi ya pamoja ya utafiti.
Aidha,
amesema kuwa kutokana na ZUT kuwa na utaratibu wa kuajiri wahitimu wa Shahada
ya Uzamili katika kitivo chake, pia wamejadili uwezekano wa wahitimu wa Shahada
ya Uzamili kutoka IITMZ kupewa nafasi za ualimu chuoni hapo, hatua
itakayochangia kukuza rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu Zanzibar.
Nae
Mkurugenzi Mtendaji wa ZUT Dk. Betty Shitima Bweupe amesema hatua ya
kuitembelea kampasi ya IITMZ ni kwa
lengo la kupitia makubaliano ya kiutendaji yaliyokubaliwa awali, kadhalika
kushudia utendaji halisi wa IITMZ kwa mujibu wa programu za kitaaluma
zinazotegemwa kunufaisha pande zote mbili na Taifa kwa ujumla.
Pia,
amethibisha kuridhishwa na hatua za kimaendeleo zilizofikiwa na IITMZ ndani
kipindi kifupi tokea kuanzishwa kwake mwezi Oktaba, 2023.
‘Uwepo wangu
katika kampasi ya IITMZ umeniachia matumaini makubwa, nimefurahia ubora wa
taaluma inayotolewa na Taasisi hii. Amesema Dk. Betty.
Akiedendela kuizungumzia IITMZ Dk. Betty ameongezea kwa kusema kuwa, ZUT itatilia mkazo utekelezaji wa programu mfanano ambazo zinatekelezwa na taasisi hizo.
Vile vile, amesema kuwa, ZUT kuwa na chuo pekee nchini Zambia kinachotoa taaluma ya masuala ya teknolojia kina nafasi kubwa zaidi ya kufanya kazi karibu na IITMZ kubadilishana utaalamu.
Adha, Dk.
Betty amethibitisha kufurahishwa na
msimamo wa wanafunzi wa IITMZ ambao ni raia wa Zambia wanaondelea na masomo yao
katika kampasi hiyo kwa kuonesha utayari wao wa kutumia ujuzi wao kushirikiana
na taasisi mbalimbali kutatua changamoto
za kijamii, kitaaluma na kiteknolojia nchini Zambia mara tu watakapomaliza
masomo yao.
Ujumbe wa
ZUT katika kampasi za IITMZ ulilenga pia
kupitia na kufahamu kwa kina programu zinazoendesha na IITMZ, kuwatambua
wataalamu kitaaluma pamoja na kushuhudia mazingira halisi ya kimafunzo
yanayoendesha katika kampasi hiyo.
Kutoka ZUT
wengine walioshiriki katika ziara hiyo ya siku mbili ni Dk. Gabriel Musonda
ambae ni Mkurugenzi Taaluma na Dk. Geofrey Mumba, Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Biashara na Masoko.
Post a Comment