SERIKALI IMEONGEZA TIJA YA UZALISHAJI WA KILIMO CHA MPUNGA ZANZIBAR
NA MARYAM NASSOR
WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mhe. Suleiman Masoud Makame amesema Serikali imeongeza tija ya uzalishaji wa kilimo cha mpunga kwa kutoa ruzuku inayowezesha upatikanaji wa zana za kisasa za kilimo, zinazotumika , katika kutoa mafunzo kwa vijana wanaohudumia mabonde ya mpunga.
Akizungumza na waandishi
wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuhusu siku 100 za mafanikio
ya uongozi wa awamu ya pili ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatua hiyo
ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya sekta ya kilimo unaolenga
kuwaunganisha vijana katika kuimarisha thamani ya kilimo.
Amesema, lengo la Serikali ni kuwaunganisha vijana hao na
taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuwawezesha
kupata mikopo nafuu kwa ajili ya ununuzi wa zana na teknolojia za kisasa za
kilimo.
“Nia
ya Serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za kisasa zitakazoongeza
uzalishaji wa mpunga na mazao mengine ya kilimo,” alisema Mhe. Makame.
Aidha, amefahamisha kuwa Serikali imeendelea kuimarisha sekta
ya mifugo kwa kuanzisha miradi ya ufugaji wa kuku ikiwemo kiwanda cha vifaranga
kilichopo katika eneo la Kwambani chenye uwezo wa kuzalisha vifaranga 30,000
kwa wiki.
“ Tunawapa vijana mafunzo ya vitendo ili waweze kuwa wataalamu katika kuhudumia
mabonde ya mpunga na kuongeza tija katika uzalishaji,” aliongeza Waziri.
Ameongeza kuwa, mwekezaji
mwingine katika eneo la Pangeni yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha
ujenzi wa kiwanda cha vifaranga pamoja na kiwanda cha uzalishaji wa chakula cha
kuku, miradi ambayo inatarajiwa kuimarisha sekta ya ufugaji wa kuku na
kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
“Haya yote
yasingewezekana bila ya uwepo wa mashirikiano mazuri baina ya wakulima,
wafugaji na wataalamu wa wizara wenye jitihada za dhati na malengo ya pamoja ya
kuleta mageuzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo-biashara,”
ameeleza Mhe. Makame.
Aidha,
amewasisitiza vijana kujikita katika shughuli za kilimo na ufugaji ili
kujiimarisha kiuchumi, akieleza kuwa sekta hiyo imeendelea kuwa mkombozi mkubwa
katika kuleta maendeleo ya wananchi, kukuza uchumi wa nchi na kuongeza kipato
cha mtu mmoja mmoja.
Post a Comment