WAWAKILISHI WANNE HAWATOSHI KATIKA MAJIMBO 50 YA UCHAGUZI ZNZ



Na Maryam Nassor

Katika majukwaa ya siasa za Zanzibar, mjadala kuhusu usawa wa kijinsia katika uongozi umeendelea kushika kasi, hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania  wa mwaka 2025.

 Katika uchaguzi huo ,jumla ya wagombea wawakilishi 484 waliogombea katika nafasi ya uwakilishi katika majimbo 50 ya uchaguzi Zanzibar kwa vyama vyote 11 vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, 2025.

 Lakini cha kusikitisha  ni wanawake  wanne tu, ndio waliyoshinda nafasi hiyo ya uwakilishi katika majimbo ,  na wanaume  walipata majimbo 46.

 Wanawake wanne pekee, katika majimbo 50 ya uchaguzi ni ishara tosha kwamba ushiriki wa wanawake katika uongozi bado ni mdogo na unahitaji nguvu mpya za kisera na kijamii ili kufikia uwiano wa kweli wa kijinsia.

 Hali hiyo ,imeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa ushiriki wa wanawake katika siasa na utekelezaji wa Dira ya Endelevu ya Maendeleo Zanzibar (ZADEP 2021–2026), inayolenga kufikia asilimia 50/50 katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi.

Mboja Ramadhan Mshenga, kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM),  mkoa wa Kaskazini Unguja aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo, anasema wanawake wana uwezo wa kuongoza,wanachohitaji ni fursa na mabadiliko ya mitazamo katika jamii kuhusu wanawake na uongozi.

Anasema kuwa,  tatizo si uwezo wa wanawake bali ni mazingira yanayokwamisha ushiriki wao kwani wengi wanakosa  rasilimali fedha za kampeni na uchaguzi  . “Wanawake huwa tunajitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwa sababu tunao uwezo, lakini wengi hawapewi nafasi za kugombea na matokeo yake hatufikii usawa wa kijinsia,” anasema Mboja, mwakilishi wa jimbo la Mahonda.

 

Mboja anaeleza kuwa, mfumo wa kisiasa uliopo bado haujatoa nafasi ya kutosha kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika michakato ya uongozi, kutokana na kujengeka kwa dhana kwamba uongozi ni wa wanaume. Hali hii, anasema hupunguza uungwaji mkono hata kutoka kwa wanawake wenyewe.

Pamoja na hatua zilizopigwa katika usawa wa kijinsia, uchaguzi wa mwaka 2025 umeonesha kuporomoka kwa uwakilishi wa wanawake kisiasa, ambapo idadi ya wanawake waliochaguliwa imepungua kutoka wanane katika kipindi cha 2020/2025 hadi wanne katika kipindi cha 2025/2030.

 Aidha anasema kuwa,  mfumo wa special seats hauwezi kutatua changamoto hiyo kwani hauwapi wanawake nafasi ya ushindani wa moja kwa moja majimboni.

Anashauri, kuwepo kwa sheria mahsusi zitakazolazimisha uwiano sawa wa kijinsia katika nafasi za kugombea, ili kutoa nafasi zaidi kwa wanawake kushiriki katika majimbo.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wanawake katika chama cha Alliance for Democrats Change (ADC), Nadhira Ali Haji, anasema kuwa asilimia 50/50 katika nafasi za uongozi ni haki ya kijamii na si upendeleo.

 Anaeleza kuwa, wanawake Zanzibar bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa rasilimali, elimu ya kisiasa na uungwaji mkono wa kijamii.

Nadhira anasema wanawake wanapojitokeza kugombea hukabiliwa na vitisho, kubezwa, pamoja na kukatishwa tamaa na familia na jamii. Hali hiyo husababisha wengi kushindwa kufika mbali katika safari ya kugombea nafasi za uongozi.

 Anapendekeza kuwepo kwa mfumo wa kitaifa unaolazimisha vyama vya siasa kuweka asilimia maalum ya wagombea wanawake katika majimbo.

“Usawa wa kijinsia si ombi, ni haki ya wanawake ambayo imechelewa kutimizwa,” anasisitiza Nadhra.

 

Mashavu Bakar kutoka chama cha ACT-Wazalendo anasema kuwa Serikali bado haijaonesha utayari wa dhati wa kuwapa wanawake nafasi za uongozi ili kufikia 50/50.

 Anasema  kuwa, wanawake wengi kutoka vyama vya upinzani wanajitokeza kugombea, lakini hawapewi nafasi stahiki.

“Kufikia asilimia 50/50 katika vyombo vya maamuzi na nafasi za uongozi ni nadra katika Serikali zetu zisizokuwa na usawa katika uchaguzi,” anasema Mashavu.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ)  ni mdau muhimu katika kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi. Afisa Program wa mradi wa Young Media Fellows (YMF), Tatu Ali, anasema changamoto kubwa inayoathiri ushiriki wa wanawake ni mitazamo ya kitamaduni kwamba siasa ni kazi ya wanaume.

“Tumekuwa tukiwapa mafunzo wanawake viongozi  kutoka vyama vyote vya siasa nchini, ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi “ anasema.

Mchambuzi wa masuala ya wanawake na uongozi, Almasi Mohd, anaeleza kuwa, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar  imeweka wazi umuhimu wa usawa wa kijinsia kama msingi wa maendeleo jumuishi. Hata hivyo, utekelezaji wake unahitaji nguvu zaidi, hasa katika kupunguza pengo la uongozi wa kijinsia.

Anapendekeza ,programu maalum za kuwaandaa wanawake kuingia katika siasa na kuondoa dhana ya kwamba uongozi ni wa wanaume.

“Zanzibar haiwezi kufikia dira ya maendeleo bila kuwapa wanawake nafasi sawa mezani kwa maamuzi, kwani wanawake ni wengi  zaidi ya milioni 1.8 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivyo, ni lazima wapewa nafasi sawa katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi,” anasema.

 

Mwisho

 

No comments

Powered by Blogger.