WASHIRIKA WA MAENDELEO WAZINDUA MPANGO WA PAMOJA KUINUA UCHUMI NA KUJENGA JAMII SALAMA KASKAZINI UNGUJA
Washirika wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali na asasi za kiraia wamefanya ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kutambulisha mradi wa mpango wa pamoja utakaowawezesha wananchi kujiinua kiuchumi na kuishi katika jamii salama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women), Lucy Tesha, alisema mradi huo unalenga kuwawezesha wananchi hususan wakulima wa mazao ya kiuchumi kuongeza thamani ya bidhaa zao na kupata masoko yenye tija.
“Lengo letu ni kukuza kipato cha wananchi kupitia shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali, sambamba na kuhakikisha wanakingwa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika mnyororo mzima wa thamani. Pia tunatoa uelewa namna ya kupambana na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika jamii,” alisema Bi. Tesha.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mmanga Machano, alisema ipo haja ya kufanya juhudi za ujumuishi ili kuwafikia wanajamii wengi zaidi kwa lengo la kuwapa elimu itakayobadili mitazamo yao na kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Nao baadhi ya wananchi waliokutana na washirika wa maendeleo kupitia vikundi vya kilimo walisema changamoto kubwa wanazokumbana nazo ni pamoja na kuitwa majina ya kejeli, kukatishwa tamaa, kunyimwa ruhusa ya kufanya kazi zao kwa uhuru pamoja na udhalilishaji kwenye masoko.
Mradi huo wa pamoja unatekelezwa na mashirika ya UN Women, UNDP, UNFPA, FAWE na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ukiwa na dhamira ya kupunguza umasikini na kuimarisha ulinzi wa jamii dhidi ya ukatili wa kijinsia. ambapo ni mradi wa mwaka mmoja. utakaotekelezwa kaskazini Unguja na kaskazini pemba.
Mwisho



Post a Comment