UMUHIMU WA WANAWAKE KWA WANAWAKE KUSHIRIKIANA NA KUSHIRIKISHWA KATIKA MAAMUZI YA JAMII


 

Na Maryam Nassor


WANAWAKE ni nguzo muhimu ya maendeleo ya jamii, na mshikamano kati yao ni silaha yenye nguvu katika kuleta mabadiliko chanya.

 Pale wanawake wanaposhirikiana na kuunda maeneo salama ya kusaidiana,  kushirikishana uzoefu na kuongeza uelewa kuhusu haki na fursa mbali mbali mara nyingi huleta tija katika jamii.


Utamaduni wa women supporting women (wanawake kusaidiana) unajenga mshikamano wa kijamii na kiuchumi, huku ukitoa nafasi kwa wanawake kupata sauti ya pamoja.

 Katika jamii nyingi hususan vijijini, wanawake wamekuwa wakianzisha vikundi vya kujifunza, kujiendeleza na kusaidiana katika shughuli za uzalishaji na malezi ya familia.

Katika maeneo mengi ya vijiji, hususan Mkoa wa Kusini Unguja, utaratibu huu umekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya huko Uzi wilaya ya Kati Unguja, Salama Khamis, mkazi wa kijiji hicho amesema mfumo wa kusaidiana wanawake kwa wanawake umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Huku kwetu utaratibu wa kusaidiana wanawake kwa wanawake upo, na umeleta maendeleo makubwa. Tunashirikiana katika kilimo, miradi midogo na hata malezi ya familia,” alisema Salama.

Ameongeza kuwa ,kupitia Shule za Mashamba Darasa (Farmer Field Schools – FFS), wanawake wamepata nafasi ya kukutana, kujifunza mbinu bora za kilimo, kubadilishana uzoefu, na kujua jinsi ya kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi.

“Kupitia mashamba darasa, tunajifunza mbinu mpya za kilimo, tunapata ujasiri wa kujiamini na kufanya maamuzi bora kuhusu uzalishaji na afya za familia zetu,” aliongeza Salama.

Kwa upande wake,  Safia Ali Mohamed, mkazi wa Bungi, alisema uundwaji wa vikundi vya wanawake kama vile COFMAs (Community Forums for Management and Action) umesaidia sana wanawake kushiriki katika maamuzi ya kijamii.

“Kupitia vikundi hivi, tunajadili changamoto zetu, kuibua mawazo mapya na kushawishi mabadiliko. Wanawake tunaposhirikiana, sauti zetu zinasikika na tunashiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa,” alisema  Safia.

Ameongeza kuwa ni ukweli usiopingika kwamba wanawake wanapopendana na kusaidiana katika shughuli za kiuchumi na kijamii,  ambapo jamii hunufaika kwa maendeleo endelevu.


Asma Sadiki, mkulima kiongozi kutoka Bungi, amesema ushirikiano wa wanawake siyo tu ishara ya mshikamano, bali ni injini ya maendeleo endelevu.

“Kupitia Mashamba darasa ya  COFMAs, wanawake wanapata ujasiri wa kushiriki katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Tunajifunza kutoka kwa wenzao, tunashirikiana na tunajenga mtandao wa wanawake wenye dira moja,” alisema Asma.

Amesema, vikundi hivyo vinawasaidia wanawake kuimarisha uongozi wao, kujenga ujasiri wa kuchukua nafasi za maamuzi, na kuondoa dhana kwamba mwanamke hawezi kuwa kiongozi bora.

Kwa upande wake, Asha Suleiman, mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kutoka  Bungi, amesema wanawake wanapopewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi, jamii hupiga hatua kubwa ya maendeleo.

“Wanawake wanafahamu kwa undani changamoto za kijamii kama ukosefu wa maji, elimu na huduma za afya. Wanaposhirikishwa katika maamuzi, wanatoa mawazo ya vitendo yanayogusa maisha ya kila siku,” alisema Asha.

Amesema serikali na mashirika binafsi yanapaswa kuendelea kuimarisha mifumo ya ushirikishwaji wa wanawake kupitia vikundi vya kijamii na elimu endelevu.

Kwa upande wake, Mbarouk Omar, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Community Forestry  Pemba, (C F P), amesema ushirikiano wa wanawake ni sehemu muhimu ya kujenga jamii yenye usawa na maendeleo.

“Kupitia miradi ya mazingira na kilimo cha misitu, tumeona jinsi wanawake wanavyoweza kuwa viongozi bora wa mabadiliko. Tunawahimiza wanawake kuendelea kushirikiana, kujifunza na kuwa sehemu ya maamuzi ya kijamii na kimazingira,” alisema Mbarouk.

Ameongeza kuwa Pemba Community Forestry itaendelea kutoa nafasi kwa wanawake kupata mafunzo ya uongozi wa kijamii na kiuchumi, hasa katika sekta za mazingira, kilimo na uhifadhi wa rasilimali.


“ Mshikamano wa wanawake siyo tu ishara ya upendo na umoja, bali ni chimbuko la maendeleo ya kwel, Kadri wanawake wanavyoshirikiana, kujifunza na kushiriki katika maamuzi, ndivyo jamii inavyopata nguvu mpya ya ustawi wa Pamoja” amesema.



                                                                 Mwisho

No comments

Powered by Blogger.