MFUMO DUME UNAVYOZIMA NDOTO ZA WANAWAKE KUWA VIONGOZI.
Na Maryam Nassor
“Nilipogombea
nafasi ya udiwani kwa mara ya kwanza, sikukutana na changamoto ya wapinzani
pekee, bali nilipambana na dhana iliyojengeka kwenye jamii kwamba siasa ni kazi
ya wanaume. Wengi waliniambia, wanawake ni wa jikoni, siyo wa majukwaani.”
Mwanachama
huyo wa chama cha ACT-Wazalendo ni mmoja
wa wanawake wachache waliothubutu kugombea nafasi ya uongozi mwaka 2020.
Asha, mwenye umri wa miaka 38, amesema ndoto
yake ilikuwa kushirikiana na wananchi wake katika kuleta maendeleo, lakini
mfumo dume uliokuwa ukitawala ndani ya chama na jamii ulimfanya akabiliane na
upinzani mkali kutoka kwa wanaume na hata wanawake wenzake.
Anaamini
kuwa kila mwanamke ana uwezo wa kuongoza, lakini changamoto kubwa ni vikwazo
vinavyotokana na mila, mitazamo ya kijinsia, na mgawanyo wa majukumu ya
kifamilia unaowafanya wanawake wengi wasione nafasi ya kushiriki kwenye siasa.
“ Mfumo dume
bado ni tatizo katika jamii na ndani ya
vyama vya siasa ambapo mara nyengine unagombea katika uchaguzi wa ndani wajumbe wanakupitisha anakuja mtu
anakwambia usigombee nafasi hiyo
hutoiweza mwachie mwanaume agombee” amesema jambo linalorudisha nyuma jitihada
za wanawake katika kugombea nafasi za uongozi.
Amesema kuwa, wanawake wako wengi kuliko
wanaume lakini mifumo dume inawafanya wasisonge mbele na kutimiza ndoto zao za
kuwa viongozi.
“Wanawake tuna nguvu, tuko wengi ukilinganisha
na wanaume na tuna maono. Lakini mfumo
dume unatuweka pembeni. Ni jukumu letu sasa kuvunja kuta hizi na kuthibitisha
kwamba ndoto za wanawake kuwa viongozi si za kufikirika bali ni za kweli.”
amesema.
Kwa upande
wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bahati Ali
Rashid , ambaye ni kada wa chama hicho
na mgombea udiwani wadi ya Kihinani jimbo la Mfenesini Unguja, amekiri kwamba bado nafasi za uongozi zimejaa wanaume
zaidi ya wanawake.
‘’Wanawake tuko wengi, takribani nusu ya
wanachama wa chama chetu ni wanawake, lakini unapokuja kwenye maamuzi makubwa,
bado mfumo dume unatawala,” amesema Bahati .
Amewataka ,wanawake mwaka huu wa uchaguzi kuwaunga mkono wanawake wenzao
ambao wamepitishwa na vyama vyao vya
siasa ,kugombea nafasi mbali mbali za
uongozi ili washinde na kuongeza
ushiriki wao kwenye nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi.
Tanzania na
Zanzibar tayari zimeridhia Mkataba wa Maputo na Mkataba wa Kimataifa wa
Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake na mkataba wa (CEDAW).
Ambayo yote yanataka usawa wa kijinsia katika
nafasi za uongozi, Pia kuna sera za kitaifa kama Sera ya Maendeleo ya Jinsia ya
mwaka 2000 na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yanayosisitiza usawa
wa kijinsia. Lakini pamoja na makubaliano haya, ushiriki wa wanawake katika
siasa na uongozi bado ni mdogo.
Takwimu za
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (2024) zinaonyesha
wanawake wanaoshikilia nafasi za uongozi kitaifa ni asilimia 30 pekee,
ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 70. Hali hii inapingana na lengo la
kufikia uwakilishi sawa wa 50/50 kama lilivyoainishwa kwenye Mpango wa
Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP 2021/2026).
Machavu
Bakar Juma ambaye anakaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa
ACT-Wazalendo, amesema changamoto kubwa
zaidi ni namna vyama vyenyewe vinavyoendeshwa.
“Vyama vingi bado vinaongozwa kwa misingi ya
mfumo dume. Wanawake wanapopewa nafasi mara nyingi huwaza heshima au kusaidia
kampeni, badala ya kusimama kwenye nafasi za maamuzi,” amesema Machavu.
Kwa upande
wake, Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), amesisitiza kuwa wanawake hawapaswi kukata tamaa. “Iwapo
tutakubali mfumo dume ututawale, hatutafika. Wanawake wanapaswa kujitokeza
kugombea nafasi zaidi katika uchaguzi wa
mwaka huu 2025 ili tufikie lengo la
50/50.”
Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ambayo imeongezwa Kifungu cha 10C, inavitaka vyama vyote kuwa na sera ya jinsia na kuhakikisha
wanawake wanashiriki ipasavyo katika siasa na uongozi.
Naibu
Msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar, Mohamed Ali Ahmed, amesema kifungu hicho
ni hatua muhimu ya kuvunja mfumo dume ndani ya vyama. “Vyama sasa vinatakiwa kuhakikisha wanawake wanapata
nafasi sawa na wanaume,” amesema Mohamed.
Hata hivyo,
bado changamoto kubwa ni utekelezaji wa sera na sheria hizo. Mara nyingi zipo
kwenye makaratasi lakini hazionekani katika vitendo.
Ripoti ya
Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 imeonyesha Zanzibar ina wanawake wengi zaidi
(asilimia 51.6 ya wakazi wote), lakini uwiano huo hauakisi kwenye uongozi.
Wanawake wachache zaidi ndiyo waliowahi kugombea na kushinda nafasi za
majimboni, huku wengi wakipata uwakilishi kupitia viti maalum pekee.
Mwisho

Post a Comment