WANAWAKE NA NAFASI ZAO MUHIMU KATIKA JAMII: MCHANGO WAO KATIKA UCHUMI, USALAMA WA CHAKULA NA MAAMUZI YA KIJAMII
WANAWAKE wanatambulika duniani kote kama nguzo muhimu ya
maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla, Ingawa mara nyingi kazi zao
hazionekani moja kwa moja katika takwimu rasmi.
Mchango wao katika uchumi wa kaya, usalama wa chakula,
maamuzi ya familia na kijamii ni mkubwa na wa lazima. Katika vijiji na jamii
nyingi za Kiafrika, wanawake huchukua jukumu kubwa la kuhakikisha familia
inapata kipato, chakula na ustawi wa kijamii.
Kwa mujibu wa
takwimu kutoka Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa ( FAO)
zinaonesha kuwa, katika nchi
zinazoendelea asilimia 43 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake, ambapo wana mchango mkubwa katika uzalishaji
wa chakula, wanazalisha chakula kwa asilimia 60/80.
Ripoti ya Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ( UNDP) ya mwaka
(2023) inaonesha kuwa nchini
Tanzania asilimia 67 ya wafanyakazi wa kike wameajiriwa katika kilimo na takwimu
za IFAD zinaonesha kuwa wakulima wadogo wadogo wengi wao wakiwa ni wanawake
ambapo huzalisha asilimia 80 ya chakula nchini.
Wanawake hushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji
mali kama vile kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo na ufundi. Pato
linalopatikana kupitia juhudi hizi hutumika kulipia mahitaji ya msingi kama
vile chakula, ada za shule, huduma za afya na makazi.
Akizungumza na mwandishi wa Makala hii, Asmaa Sadiki
mnufaika wa mradi wa Zanz Adapt kutoka Shehia ya Bungi, mkoa wa kusini Unguja amesema kupitia
mradi huo, wamepata uwelewa mkubwa wa uhifadhi wa chakula na kutambua mchango wao kiuchumi na kijamii katika familia.
Amesema kuwa, Ujuzi na mafunzo waliyoyapata kutoka mradi
huo, umewabadilisha maisha yao kiuchumi
na kimtazamo kwani wanaziona fursa nyingi kupitia kilimo na usarifu wa mazao.
“ Kwa sasa tumejiajiri kupitia kilimo na usarifu wa mazao kwa kutengeneza jamu, achari , tomato na majani
ya chai ambapo vipato vyetu vimeongezeka” amesema Asmaa.
Amesema kuwa, Utafiti
unaonyesha kuwa wanawake wanapopata kipato, sehemu kubwa ya fedha hizo hutumika
kwa maendeleo ya familia kuliko matumizi binafsi. Hii inaonesha wazi kuwa
mchango wa wanawake ni msingi wa ustawi wa kaya na Familia.
“ Kupitia elimu tuliyoipata katika mradi wa Zanz Adapt tumeweza kushiriki katika shughuli mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kukuza pato la familia zetu” amesema Asmaa.
Wanawake na Usalama wa Chakula
Kwa mujibu wa
tafiti kutoka shirika la chakula
duniani ( FAO ) ya mwaka 2021 inasema, Wanawake
ndiyo wazalishaji wakuu wa chakula vijijini, wakihusiana moja kwa moja na
kilimo cha mazao ya chakula, usindikaji na uhifadhi. Pia wao ndiyo
wanaohakikisha mlo bora kwa familia.
Zakia Mansab mkaazi
wa Unguja Unguu na mkulima kiongozi, amesema Wanawake wanahakikisha kuwepo kwa
usalama wa chakula nyumbani na katika jamii kwa ujumla.
“ Bila nguvu kazi ya
wanawake, changamoto za upungufu wa chakula zingekuwa kubwa zaidi hasa huku
vijijini kwani baadhi ya wanaume
hawashiriki kikamilifu katika shughuli za udhalilishaji “ amesema Zakia.
Aidha amesema kuwa, kupitia mradi wa Zanz Adapt wamejifunza
mambo mengi ikiwemo kilimo msitu, upandaji mikoko lakini pia usarifu wa mazao ,
hivyo umesaidia utuzaji wa chakula.
‘’Tuna shukuru sana mradi huu wa Zanz Adapt kwa kweli
umetusaidia , zamani msimu wa matunda tulikuwa tunayatumia na msimu ukimalizika
ndio basi lakini kwa sasa tunaweza kuyasarifu na kuyatumia baadae” amesema
Zakia.
Ushiriki wa Wanawake
katika Maamuzi ya Kaya
Asha Bakar mkaazi wa Shehia ya Unguja ukuu, amesema kuwa Mwanamke
anaposhiriki katika maamuzi ya kifamilia—hasa yanayohusu bajeti, elimu ya
watoto na afya—maisha ya familia huwa bora zaidi.
Amesema kuwa ,Hata hivyo mila na desturi katika jamii nyingi bado
hupunguza nafasi ya mwanamke kushiriki katika maamuzi kikamilifu, Kupaza sauti za
wanawake na kuwashirikisha ni msingi wa ustawi wa kijamii na kiuchumi.
Mchango wa Wanawake katika Maisha ya Kijiji
Katika vijiji vya Unguja Ukuu , wanawake wana mchango mkubwa na huchangia katika maendeleo ya Taifa
kupitia shughuli za kijamii kama vikundi vya akiba, vikoba na ushirikiano wa
kijamii.
Asha Bakar mkaazi wa Kijiji hicho amesema, Wanawake
mara nyingi huendesha miradi midogo midogo ya kilimo na maendeleo inayosaidia sio kaya zao tu bali
jamii kwa ujumla.
“ Kwa mfano, miradi ya bustani za kijiji au vikundi vya
usindikaji vyakula huchangia ajira na kipato kwa wanakijiji wengi “ amesema
Asha.
Wanawake na Maamuzi
ya Kijamii
Asha amesema kuwa, Hata
kama mara nyingi nafasi za uongozi hukaliwa na wanaume, wanawake wanapopewa
nafasi ya kushiriki katika mikutano ya kijiji na maamuzi ya jamii, maamuzi hayo
huwa jumuishi zaidi.
Aidha amesema kuwa, Ushiriki wao hupelekea
huduma bora za kijamii kama elimu, maji safi na afya, kwa sababu wanawake
huelekeza mawazo yao kwenye mahitaji ya msingi ya familia na jamii kwa ujumla.
Wanawake na Uchumi wa Jamii
Salama Juma mkaazi wa
Shehia ya Unguja ukuu. amesema Wanawake
wanaposhirikishwa ipasavyo katika shughuli za kiuchumi na kijamii, pato la
jamii huongezeka.
Amesema kuwa, Hii ni kwa sababu wanawake huleta mawazo
mapya, ubunifu na nidhamu ya kifedha. Miradi ya maendeleo inayoongozwa na
wanawake mara nyingi hufanikiwa zaidi kutokana na mshikamano na uwajibikaji
wao.
“Mchango wa wanawake katika familia, kijiji na jamii kwa
ujumla ni muhimu na hauwezi kupuuzwa, Ni dhahiri kuwa wanawake ni nguzo kuu za
uchumi, usalama wa chakula, ustawi wa familia na maendeleo ya kijamii” amesema
Salama.
Aidha amesema kuwa,
ni wajibu wa jamii na serikali kutambua
mchango huo, kuwawezesha wanawake kwa elimu, mitaji na nafasi za uongozi ili
kuhakikisha usawa na maendeleo endelevu.
Peter Shaaban ni Afisa kilimo na
teknolojia kutoka mradi wa ZanzAdapt amesema katika mradi huo wamewawezesha
wanawake wa vijiji vya Unguja ukuu, Uzi, Ngambwa na Bungi kulima kisasa
na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha amesema kuwa, katika mradi huo
zaidi ya asilimia 80 ya walengwa wa
mradi ni wanawake ambao ni 2,400 na
wanaume ni 600 .
Mwisho

Post a Comment