WANAWAKE NA HAKI YA KUMILIKI ARDHI NA RASILIMALI ZA UZALISHAJI: FURSA NA CHANGAMOTO ZANZIBAR
NA MARYAM NASSOR
UMILIKI na udhibiti wa ardhi ni msingi muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, Katika jamii nyingi hasa zile za Afrika Mashariki.
Ardhi ndiyo chanzo kikuu cha uzalishaji mali, usalama wa
chakula na urithi wa kifamilia, Hata hivyo wanawake kwa muda mrefu wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto kubwa za kupata haki sawa ya kumiliki na kudhibiti
ardhi na rasilimali za uzalishaji.
Katika muktadha wa Zanzibar, wanawake wanachangia pakubwa
katika kilimo na kazi za uzalishaji, lakini bado idadi kubwa hawana haki ya
kisheria wala kijamii ya kudhibiti ardhi.
Hali hii
imesababisha wanawake wengi kukosa uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu ardhi,
kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi, na kubaki nyuma katika
maendeleo.
Sheria ya Ardhi Zanzibar Inasemaje
Kifungu cha 5 cha Sheria hiyo kinasisitiza kuwa ardhi yote
ni mali ya umma chini ya mamlaka ya Rais, lakini kila raia anayo haki ya kupewa
umiliki au matumizi ya ardhi kwa mujibu wa taratibu, kwa maneno mengine, hakuna
kizuizi cha kisheria kinachomnyima mwanamke kumiliki ardhi Zanzibar.
Changamoto kubwa
inabaki kuwa ni mitazamo ya kijamii na mila zinazomnyima mwanamke nafasi hiyo.
Nafasi
ya Ndoa Rasmi katika Kulinda Haki za Wanawake
Ndoa rasmi ni nyenzo muhimu kwa mwanamke kuhakikisha anapata
haki zake za ardhi na mali.
Shekh Ali Abdalla kutoka Msikiti wa Fuoni wilaya ya
Magharibi ‘B’ Unguja anasema, Mwanamke
anapokuwa katika ndoa isiyo rasmi (kama ndoa ya kimila au bila kusajiliwa
kisheria), mara nyingi anakosa haki ya kurithi mali za mume endapo mume
atafariki.
Amesema ,Sheria za urithi Zanzibar kupitia Sheria ya Mahakama ya Kadhi, zinatoa
mwongozo wa namna mali inavyogawanywa.
“Hata hivyo, haki za mwanamke hupata nguvu zaidi pale ndoa ambapo imesajiliwa kisheria, jambo
linalomlinda baada ya kifo cha mume wake kupata haki zake” amesema .
Haki
za Mwanamke Baada ya Talaka na Kifo
Wanawake wengi hukosa taarifa sahihi kuhusu haki zao baada ya talaka au kifo cha mume. Kwa mujibu wa sheria na taratibu za Mahakama ya Kadhi Zanzibar:
Shekh Ali amesema , Mwanamke aliyepewa talaka anastahili kupata haki zake za matunzo (nafaka) hasa ikiwa ana watoto wadogo.
Aidha anasema kuwa, Endapo mume atafariki mjane ana haki ya urithi kwa mujibu wa masharti ya dini ya Kiislamu na sheria za urithi, na hii inaweza kuwa sehemu ya ardhi au mali nyinginezo.
“Wanawake pia wana haki ya kushiriki katika mgawanyo wa mali zilizochumwa pamoja katika ndoa ikiwa mume atafariki ikiwemo ardhi” amesema .
Umuhimu
wa Mabadiliko ya Mitazamo ya Kijamii
Salama Juma Mkaazi wa
shehia ya Unguja Ukuu amesema, Ingawa sheria zinatoa mwanya kwa wanawake
kumiliki ardhi, bado kuna vikwazo vikubwa vinavyotokana na fikra za kijamii.
“ Jamii nyingi bado zinaamini kuwa ardhi ni ya wanaume
pekee, na kwamba mwanamke anapaswa kutumia ardhi kupitia baba, kaka au mume” amesema
Salama .
Amesema kuwa, baada ya kupata elimu ya umuhimu wa umiliki
wa ardhi kutoka katika mradi wa Zanz Adapt anamiliki ardhi yake mwenyewe ambayo
anaitumia kwa shughuli za kilimo.
“ Baada ya kupata elimu ya umuhimu wa kumiliki ardhi sasa
na mimi namiliki ardhi yangu ambayo naitumia kwa ajili ya kilimo” amesema
Salama huku akiwataka wanawake wengine kuona umuhimu wa kumiliki ardhi.
Aidha amesema kuwa, Ili kubadilisha mitazamo ya
jamii juu ya umiliki wa ardhi , elimu na uhamasishaji ni nyenzo muhimu.
Amesema , Wanawake
wanapaswa kuelimishwa kuwa wana haki ya msingi ya umiliki wa ardhi na
rasilimali za uzalishaji. Kauli mbiu ya “Wanawake wanaweza na wanapaswa
kumiliki ardhi” ni muhimu katika kuondoa vikwazo vya kimtazamo.
Bi Furaha
Yassini mkaazi wa Uzi mkoa wa
Kusini Unguja amesema, Haki za wanawake kumiliki na kudhibiti ardhi na
rasilimali za uzalishaji Zanzibar zipo kisheria, lakini changamoto kubwa
inabaki kwenye utekelezaji na mitazamo ya kijamii.
Aidha amesema kuwa, Serikali, jamii na taasisi za kiraia zina jukumu la
kushirikiana katika kutoa elimu, kuhamasisha mabadiliko ya fikra, na
kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa katika umiliki na matumizi ya ardhi.
“ Kuna umuhimu mkubwa kwa wanawake kumiliki ardhi kwani,
wanakuwa na uhakika na wanachokilima kuwa chao, ikitokea umelima shamba ya mume na
mumeachana mwanamke huwa huna chako’’ amesema .
Nae, Sheha wa shehia ya Unguja Ukuu Khamis Ibrahim Shomari amesema bado elimu inahitajika kwa jamii juu ya umuhimu wa wanawake kumiliki ardhi.
Amesema kuwa, Serikali na taasisi binafsi zishirikiane katika kutoa elimu hiyo kwani jamii bado hawajaona umuhimu mkubwa kwa kumiliki ardhi na kuwa na hati za umiliki kisheria.
" Jamii bado hajawa na uwelewa mkubwa wa kumiliki ardhi na kuwa na hati miliki za maeneo yao elimu zaidi inahitajika hasa huku vijini " amesisitiza .
John Ngonyani ni Afisa kutoka Jumuiya ya Kuhifadhi Misitu Pemba (CFP) amesema, changamoto kubwa inayowapamba wakati wanatekeleza mradi huo mkoa wa kusini
Unguja , wanawake wengi hawamiliki ardhi.
Amesema kuwa, kutokana na Sheria ya Ardhi Zanzibar (Land Tenure Act,
1992) pamoja na marekebisho yake, inatambua haki ya kila mwananchi kumiliki na
kutumia ardhi bila kujali jinsia, lakini ni asilimia 24.7 tu ya wanawake ambao ndio wanamiliki ardhi
ukilinganisha na wanaume .
“ Ipo haja kubwa ya
kuhamasisha jamii na wanawake kuona umuhimu wa kumiliki ardhi na kuwa na hati
za umiliki kisheria kwani wananchi wengi hawajui umuhimu huo”
amesema John.
Mwisho

Post a Comment