JUMLA YA WANACHAMA 25 KUTOKA VIKUNDI 16 VYA WILAYA YA KUSINI UNGUJA WAPATIWA MAFUNZO
NA MWANDISHI WETU,
Jumla ya wanachama 25 kutoka vikundi 16 vya kuweka na kukopa katika Wilaya ya Kusini Unguja wamepatiwa mafunzo ya siku mbili ya kuchagua, kupanga na kusimamia biashara, chini ya Programu ya Mashirikiano ya Pamoja kwa ajili ya Haki za Watu wenye Ulemavu (CADiR) inayotekelezwa na Chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Jumuiya ya wasioona Zanzibar (ZANAB) kwa ushirikiano mkubwa na Shirika la Watu Wenye Ulemavu la Norway (NAD).
Washiriki
hao ambao 16 ni watu wenye ulemavu na 9
ni walezi na wasimamizi wa Watoto wenye ulemavu
wamehudhuria mafunzo kama wawakilishi wa vikundi vyao,
na wanatarajiwa kuyafikisha maarifa haya kwa wanachama wenzao, ili kila kikundi
kinufaike kwa pamoja na kuimarisha biashara zake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Aziza Ismail ambae ni Mratibu wa program ya CADiR kutoka NAD, amesema taasisi zinazoshirikiana katika programu hii zina matumaini makubwa kuwa mafunzo haya yatawawezesha wawakilishi wa vikundi kupeleka elimu waliyoipata kwa wenzao, hatimaye kusaidia wanachama wote kuchagua biashara bora na zenye tija.
“Kwa vile miongoni mwa malengo makuu ya
program hii ni
kuwawezesha watu wenye ulemavu kuinuka kiuchumi na kupata kipato rasmi, tunaamini mafunzo haya yatasaidia kikamilifu
kulifikia lengo hili”, alisisitiza Mratibu huyo.
Mkufunzi
wa mafunzo hayo, Muhidini Ramadhan kutoka TAMWA ZNZ amesema kuwa hali ya umasikini
inaweza kupungua kwa watu wenye ulemavu iwapo wataelimishwa juu ya ujuzi na
miradi ya kiuchumi yenye tija.
Nae Meneja
wa Programu kutoka TAMWA ZNZ Nairat Ali, amesema mafunzo haya ni muhimu kwa
ajili ya kuwasaidia wanachama kupanga na kuchagua biashara zenye tija ili
vikundi viwe endelevu na viweze kujitegemea kiuchumi.
Kwa
upande wake ndugu Khamis Ali, Afisa Program kutoka ZANAB, amewataka washiriki
wa mafunzo hayo kujifunza kwa umakini mafunzo hayo ili waweze kuchagua biashara
sahihi zitakazowawezesha kupata mikopo na kuweza kurudisha kwa wakati.
Washiriki
walijadili na kuandika mipango ya biashara, baadhi wakieleza ndoto zao za kukuza
biashara ndogondogo walizonazo, ikiwemo kilimo, ufugaji, kufungua maduka na ushonaji.
Akizungumza
kwa niaba ya washiriki wenzake, Yusra Ali Hassan ambaye ni Msaidizi Katibu wa
kikundi cha Mtu ni Utu cha Kajengwa, ameshukuru waandaaji wa mafunzo
hayo na kusema
yamewapa muongozo mzuri wa namna ya kupanga biashara na kutumia vizuri fedha
katika kukuza biashara zao.
“Kupitia
mafunzo haya tumejifunza kupanga matumizi kwa uangalifu na kuweka mipango
thabiti ya biashara, binafsi
nimeona namna biashara ya ushonaji inavyoweza kukua zaidi nikiwa na maarifa
haya mapya,” amesema Yusra.
Mafunzo
hayo ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa walimu Kitogani ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa
program ya CADiR katika eneo la uwezeshaji kiuchumi ambalo linalenga kuanzisha
na kuimarisha vikundi vya watu wenye ulemavu vya kuweka na kukopa katika wilaya
11 za Unguja na Pemba.
Mwisho
Post a Comment