Changamoto za Upatikanaji wa Mikopo kwa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar
Na Maryam Nassor
Mfumo wa mikopo ambao Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imeanzishwa ukiwa na lengo la kuwawezesha wajasiriamali na vijana kujitegemea
kiuchumi.
Umekuwa pia ukihusisha
makundi maalum yakiwemo watu wenye ulemavu, Hatua hii ni sehemu ya jitihada za
serikali kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika maendeleo ya taifa bila
kubaguliwa.
Hata hivyo, pamoja na dhamira njema ya serikali bado kuna changamoto mbalimbali zinazojitokeza
katika kupata fursa hizo hali
inayowafanya watu wenye ulemavu kuhisi kama hawajanufaika ipasavyo na haki zao
za kiuchumi na kijamii.
Wengi wao wanakumbana na masharti magumu, upungufu wa
taarifa sahihi, na ukosefu wa miundombinu rafiki jambo linalokwamisha jitihada za kujikwamua
kiuchumi kupitia mikopo.
Ushuhuda
wa Watu Wenye Ulemavu
Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Aisha Omar
mjasiriamali na mlemavu wa uoni kutoka
Kikwajuni Mjini Unguja, amesema
changamoto kubwa zinazowakumba ni pamoja na masharti magumu ya dhamana na
nyaraka za mikopo.
Aisha anayejishughulisha na utengenezaji wa udi,
mafuta ya mgando na krimu za ngozi, alisema anahitaji mkopo wa angalau shilingi
milioni moja, lakini hadi sasa hajaufanikisha kutokana na ugumu wa masharti.
“Kutokana
na shughuli zangu za ujasiriamali nahitaji mkopo angalau wa milioni moja,
lakini bado sijafanikiwa kuupata kwani mara nyingi mikopo inayotolewa huwa ni
ya vikundi. Mikopo ya mtu mmoja mmoja masharti yake huwa magumu mno,” amesema
Aisha.
Aisha aliongeza kuwa uelewa mdogo kwa baadhi ya watu wenye
ulemavu ni tatizo kubwa kwani wengi wao hawapati taarifa sahihi kuhusu namna ya
kuomba na kupata mikopo.
Alieleza kuwa
aliwahi kuomba mkopo wa 4-4-2 lakini alikosa kutokana na
kushindwa kutoa dhamana, hali iliyomkatisha tamaa licha ya dhamira yake ya
kukuza biashara ndogo.
Kwa upande wake, Juma Hassan, kijana
mfanyabiashara na mlemavu wa macho kutoka Mwanakwerekwe, amesema watu wenye
ulemavu bado hawajafikiwa ipasavyo na elimu ya mikopo.
“Changamoto kubwa kwetu ni upatikanaji
wa taarifa. Mara nyingi matangazo yanatolewa kwa maandishi pekee, sisi wasioona
tunakosa kabisa nafasi ya kujua mapema,” amesema Juma.
Ameongeza kuwa mara nyingine jamii
huwapuuza watu wenye ulemavu kwa kudhani hawana uwezo wa kurejesha mikopo,
jambo linaloathiri imani ya taasisi zinazotoa huduma hizo.
Fatma Ali, mlemavu wa usikivu kutoka Chaani mkoa wa Kaskazini Unguja, amesema watu wenye ulemavu
wa uziwi mara nyingi hukosa taarifa sahihi kutokana na kukosekana kwa
wakalimani katika vikao vya kutoa elimu ya mikopo.
“Sisi viziwi mara nyingi hatuna
wakalimani kwenye vikao vya elimu ya mikopo. Tukifika tunakaa tu bila kuelewa, mwisho wa siku
tunabaki nyuma kimaendeleo,” amesema Fatma.
Fatma amesisitiza kuwa mikopo ni fursa
muhimu kwa wananchi wote, lakini changamoto wanazokabiliana nazo watu wenye
ulemavu zinahitaji suluhisho la haraka kupitia taratibu bora, utoaji wa taarifa
kwa njia jumuishi, na kuwepo kwa miundombinu rafiki.
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar
ya mwaka 2006 pamoja na marekebisho yake, imeweka wazi kwamba watu wenye
ulemavu wana haki ya kupata fursa sawa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kifungu cha sheria hiyo kinatoa wajibu kwa
serikali kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma kwa sababu ya hali yake ya
ulemavu.
Kwa mantiki hiyo, watu wenye ulemavu
wanapaswa kupewa kipaumbele maalum katika upatikanaji wa mikopo kama ya 4-4-2 ili
kujenga usawa wa kijamii na kupunguza pengo la kiuchumi kati yao na makundi
mengine.
Nae, Mkuu wa Divisheni ya Mfuko wa
Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar ( ZEEA) Hashimu Iddi Simba amesema kupitia programu ya 4 4 2 ni fursa adhimu kwa watu wenye ulemavu kujiendeleza kiuchumi.
Amesema kuwa, tokea ianzishwe programu hiyo mwaka Septemba
2024, mpaka sasa jumla ya watu wenye ulemavu 170 wamenufaika kuwezeshwa kiuchumi, wanawake wakiwa ni 93 na wanaume 79.
Licha ya mafanikio hayo, lakini
anakiri kuwa bado kuna changamoto kubwa ya kuwafikia watu wengi wenye ulemavu
kutokana na kutokukidhi vigezo na masharti.
“ Ni kweli bado hatujawafikia watu
wengi wenye ulemavu kuwezeshwa kiuchumi kwa sababu wengi wao wanakosa vigezo
vya kukopesheka“ amesema.
Kauli ya Serikali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi,
Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, alipoulizwa
kuhusu suala hili, alisema
“Serikali
imekusudia kuhakikisha mikopo inawanufaisha wote bila ubaguzi ,Tumeanza
kuweka utaratibu maalum wa kuyajengea uwezo makundi maalum, hususan watu wenye
ulemavu kwa kutoa elimu, kurahisisha
masharti na kuhakikisha ushirikishwaji wao unakuzwa zaidi.”
Kauli hii inaonesha dhamira ya dhati ya serikali
kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na mikopo hiyo, japo changamoto za
kiutekelezaji bado zinahitaji kushughulikiwa kwa haraka.
Mwisho

Post a Comment