Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar- Changamoto na Fursa za Uwakilishi kwenye siasa
Na Maryam Nassor
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepiga hatua kubwa katika
kujumuisha watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali, ikizingatia mikataba ya
kimataifa na misingi ya usawa wa kijinsia kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.
Hata hivyo, changamoto bado zipo hususan katika kumjumuisha kikamilifu mwanamke
mwenye ulemavu katika siasa ili kufikia malengo ya uwakilishi wa asilimia 50/50.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,
asilimia 11.2 ya Watanzania Bara ni wenye ulemavu kati ya zaidi ya watu milioni
60, huku Zanzibar ikionesha idadi kubwa zaidi ya asilimia 11.4 kati ya watu
milioni 1.8. Hii ni ongezeko la asilimia 5 ikilinganishwa na takwimu za mwaka
2012.
Pamoja na wingi huo,
uwakilishi wao kwenye taasisi za kisiasa unabaki kuwa mdogo mno.
Kwa mfano, kati ya wajumbe 76 wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, ni watatu pekee wenye ulemavu — wawili kupitia viti maalum na mmoja
kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar.
Sauti za Wanawake Wenye Ulemavu
Jamila Borafya, ni mwanamke
mwenye ulemavu wa uoni kutoka MwanaKwerekwe, Wilaya ya Magharibi "B"
Unguja, anaeleza changamoto za watu wenye ulemavu wakati wakigombea nafasi za
uongozi katika vyama vya siasa.
Amesema , Mwaka
2020, alijitokeza kugombea nafasi ya Uwakilishi jimbo la Mwanakwerekwe kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini jina lake halikurudi katika hatua za mwanzo
za uchaguzi ndani ya chama.
“Changamoto kubwa niliyokumbana nayo ni kwamba vyama vya
siasa bado haviamini uwezo wa watu wenye ulemavu kushiriki kwenye siasa za
ushindani,” anasema Jamila kwa masikitiko.
Amesema kuwa, watu wenye ulemavu hawapewi haki yao ya
kugombea kama watu wengine, hata kwenye nafasi zao ambazo ni asilimia mbili katika Baraza la
Wawakilishi na badala yake wanachaguliwa watu kutoka Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) ambao hawana ulemavu mkubwa na hawajui changamoto zao.
Jamila anaamini nafasi mbili za watu wenye ulemavu katika
Baraza la Wawakilishi hazitoshi na hazitoi uwakilishi wa kweli kwa kundi hilo.
Anaeleza kuwa mara nyingi, wawakilishi hao wanaoteuliwa hupitia Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) na si moja kwa moja kutoka jumuiya za watu wenye ulemavu.
“Wale wanaopelekwa pale kwenye Baraza la Wawakilishi mara
nyingi hawajui changamoto zetu. Wanaposhindwa kututetea, si kosa lao bali mfumo wenyewe hauwahusishi moja kwa moja
kutoka kwenye watu wenye ulemavu,”
anasisitiza.
Kwa sababu hiyo, Jamila anaiomba serikali na UWT
kuhakikisha uchaguzi mkuu wa oktoba 29 mwaka huu, unawaleta mezani watu
wanaotoka moja kwa moja kwenye jumuiya za watu wenye ulemavu ili wakawe
watetezi wao.
Mtazamo wa Viongozi wa Jumuiya
Bi Salma Haji Saadat, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake
Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), anaweka wazi chanzo kikubwa cha changamoto
zinazowakumba watu wenye ulemavu ni mitazamo ya jamii.
“Jamii bado inawaona watu wenye ulemavu kama ombaomba au
wasioweza. Lakini changamoto kubwa siyo ulemavu wao, bali ni vikwazo vya kijamii vinavyowanyima haki na
fursa,” amesema.
Amesema kuwa, tafiti zinaonesha Zanzibar ina idadi kubwa ya
watu wenye ulemavu kuliko Bara — jambo linalothibitisha haja ya haraka ya
kushirikishwa kikamilifu kwenye sekta zote, ikiwemo siasa.
Kwa upande wake ,Mwenyekiti
wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), Mwadawa
Khamis Mohammed, anabainisha matumaini mapya kupitia mradi wa CADiR
(Collective Action for Disability Rights) unaotekelezwa kuanzia 2025
hadi 2029.
“Mradi huu utaimarisha haki za watu wenye ulemavu kwenye
elimu, siasa na sekta nyingine. Ni fursa ya kuhakikisha hatubaki nyuma tena,”
anasema.
Wito wa Taasisi za Kiraia
Dk. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) anasisitiza kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo
mkubwa na maarifa — wanachohitaji ni kuwezeshwa na kuwekewa mazingira rafiki.
“Ndio maana dunia leo inazungumzia haki sawa. Jamii lazima
ibadili mtazamo wake na kuwaona watu hawa kama nguvu ya maendeleo, si mzigo,”
anasema Dk. Mzuri.
Msimamo wa Serikali
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Othman Massoud Othman, akizindua rasmi programu ya CADiR, alikiri kuwa bado
mahitaji ni makubwa licha ya hatua zilizopigwa.
Amesema, Serikali
imelenga kuongeza uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwenye vyombo vya maamuzi
kutoka asilimia 2 ya sasa hadi kufikia asilimia 5 ifikapo mwaka 2030.
“Ni jukumu letu kuhakikisha kundi hili linafikiwa na
kushirikishwa kikamilifu ili kutetea haki na maslahi yao,” amesema.
Mwisho
Post a Comment