ZAMECO YAIOMBA SMZ NA ZEC KUHAKIKISHA USALAMA WA WADAU WA UCHAGUZI WAKIWEMO WAANDISHI WA HABARI.
KAMATI
ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) imeiomba Serikali ya
mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
kuhakikisha usalama wa Waandishi wa Habari, Wanawake wagombea, na Wasimamizi wa
Uchaguzi (Mawakala) katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi mkuu wa
Zanzibar ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Kamati
hiyo imesema inatambua kuwa mazingira salama kwenye masuala muhimu yenye
maslahi mapana na mustakabali wa nchi hususan suala la uchaguzi, ni sharti la
msingi ili kuhakikisha kila mdau anatekeleza majukumu yake kwa uhuru na bila ya
hofu kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 15(1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984:
"(Kila mtu anastahiki
kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na ya
nyumbani kwake, na pia heshima, na hifadhi ya maskani yake na mmawasiliano
yake)."
Aidha
Kamati imesisitiza kuzingatiwa hatua mahsusi kwa mujibu wa sheria na kanuni za
kulinda haki na usalama wa makundi haya wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi
huku ikisisitiza kuwa waandishi na jamii kwa ujumla, wanahaki ya
kupewa fursa ya kupata taarifa bila ya kuingiliwa kwani kila mmoja ana
haki hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Zanzibar 1984 sambamba na
ibara ya 19 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binaadamu (UDHR-1948) inayoeleza
“Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na mawazo yake bila ya kuingiliwa.
Aidha
ZAMECO, imesisitiza umuhimu wa Waandishi wa Habari kupewa nafasi sawa
zisizo na ubaguzi katika kupata taarifa sahihi zinazohusu uchaguzi pamoja na
kupatiwa vitambulisho maalum vinavyotolewa na Tume ya Uchaguzi na kuepuka kutoa
fursa zaidi kwa vyombo vya Serikali na kuvikwepa vyombo visivyokuwa vya
Serikali hali itakayopelekea kufuatilia na kuripoti matukio ya uchaguzi kwa
weledi usawa bila ya kuathiriwa na vikwazo visivyo vya lazima.
Hata
hivyo, kamati imetoa mapendekezo kwa Tume ya Uchaguzi kutoa mafunzo
maalum kwa waandishi wa wabari kuhusu uandishi wa taarifa za uchaguzi kwa
kuzingatia usawa wa kijinsia weledi na maadili ya taaluma kwani mafunzo hayo
yatasaidia kuimarisha uelewa wa waandishi katika kuripoti kwa kuzingatia
wagombea wa jinsia zote.
Katika
hatua nyengine, ZAMECO inapongeza ahadi iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ya kutoa na kuchapisha takwimu za jinsia za washiriki wa uchaguzi,
iikiwemo idadi ya wanawake na wanaume watakaogombea nafasi mbalimbali ikiwemo
Irais, Uwakilishi na udiwani pamoja na wapigakura na washiriki wa mchakato
mzima wa uchaguzi ambapo takwimu hizi zitakuwa nyenzo muhimu katika kufuatilia
uwiano wa kijinsia na kkusaidia kufikia lengo la usawa wa asilimia 50/50
nchini.
ZAMECO
inahitimisha kuwa, uchaguzi huru wa haki na jumuishi unahitaji
mazingira salama taarifa sahihi, na upatikanaji sawa wa fursa kwa wanawake na
wanaume ili kuimarisha demokrasia na mshikamano nchini.
Post a Comment