MASHIRIKA YA WANAWAKE YAKOSHWA NA KASI YA WANAWAKE KUGOMBEA URAIS NA MAKAMU WA RAISI.


 Mashirika ya Wanawake yakoshwa na kasi ya wanawake kugombea Uraisi na Makamu wa Raisi 20/8/2025 Mashirika yanayojihusisha na masuala ya wanawake na uongozi Zanzibar yanawapongeza wanawake 13 nchini wanaotegemewa kugombea nafasi ya uraisi na Makamu wa Raisi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

 Mashirika hayo yamesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 36 kati ya wagombea waliochukua fomu kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) ambao jumla yao ni 36 katika ngazi ya Uraisi na Umakamo.

 Taarifa hiyo ilisema kwa upande wa nafasi ya Uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inagombewa na wanawake watatu ambao ni pamoja na Raisi aliyepo madarakani Dk. Samia Suluhu Hassan anaegombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) huku Bi Mwajuma Mirambo akigombea kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) na Bi Swaumu Rashid kutoka Chama cha United Democratic Party (UDP).

 Aidha, katika nafasi ya Ugombea Wenza, wanawake Kumi wamejitokeza wakiwemo Devotha Minja (CHAUMA), Amana Suleiman Mzee (TLP), Chumu Juma (AAFP), Chausiku Khatib Mohammed (NLD), Azza Haji Suleiman (Chama cha Makini), Mashavu Alawi Haji (UMD), Satia Mussa Bebwa (SAU), Fatma Abdulhabib Fereji (ACT-Wazalendo), Husna Muhamed (CUF) na Dkt. Eveline Wilbard Munisi kutoka chama cha NCCR-MAGEUZI.

 Tunafuraha kusema kuwa kati ya hawa wagombea tisa (9) wametokea Zanzibar; mmoja katika nafasi ya Uraisi na nane wagombea wenza na hivyo kuweka historia ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za siasa za ushindani. 

 Wanawake hao ni pamoja na Dk Samia Suluhu ambaye ni Raisi wa sasa kupitia CCM na kwa upande wa wagombea wenza ni Amana Suleiman Mzee (TLP), Chumu Juma (AAFP), Chausiku Khatib Mohammed (NLD), Azza Haji Suleiman (Chama cha Makini), Mashavu Alawi Haji (UMD), Satia Mussa Bebwa (SAU), Fatma Abdulhabib Fereji (ACT-Wazalendo) na Husna Muhamed (CUF).

 Mashirika hayo, ambayo ni pamoja na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Wanawake Wanasheria Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), yameona hayo ni maendeeo makubwa ya kidemokrasia na njia sahihi kuelekea usawa wa kijinsia kwa vile kwa miaka mingi kutokana na mifumo dume wanawake waliaminishwa kuwa hawana uwezo wala nafasi ya kutamani nafasi za uongozi katika hatua ya juu. 

 Idadi hii imeweka rikodi katika historia ya nchi tokea kuanza kwa siasa za vyama vingi mwaka 1995. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kati ya wagombea 30 wa nafasi ya Uraisi na Makamu wa Raisi, wanawake walikuwa 7 pekee sawa na asilimia 23.3, Kati ya hawa watano (5) ndio waliotoka Zanzibar.

 Mashirika hayo yameeleza kuwa Tanzania ina wajibu mkubwa wa kufikia usawa wa kijinsia katika vyombo vyote vya maamuzi kama inavyoelezwa katika mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo imesaini ikiwemo ile ya Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake, 1979 (CEDAW), Umoja wa Africa, 2003 (AU) na Jumuiya ya Maendelao ya Kusini mwa Afrika, 2008 na 2015 (SADC). Yamesema hatua hii pia itawatia moyo zaidi watoto wa kike kuwa wana uwezo wa kuwa na ndoto za kimaendeleo na kuyafikia bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.

 Mashirika hayo yanapenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyama vyote vya siasa vilivyoweka wagombea wanawake katika ngazi hizo za Uraisi na Ugombea mwenza na hivyo kuonesha kutambua na kuthamini mchango wa wanawake katika demokrasia na maendeleo kwa jumla. Mashirika hayo pia yamewataka wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha mazingira ya kisiasa yanabaki salama, yenye heshima na usawa kwa wagombea wote bila kujali jinsia wala vyama ili kuhakikisha kuwa wanawake wanakuwa ni washirika sawa katika maendeleo. Imetolewa na: TAMWA ZNZ, JUWAUZA, ZAFELA & PEGAO

                                                                     MWISHO

                                          

No comments

Powered by Blogger.