WAANDISHI WA HABARI WAMETAKIWA KUHAMASISHA JAMII KURIPOTI VITENDO VYA RUSHWA KIPINDI CHA UCHAGUZI.


NA MARYAM NASSOR

MAMLAKA ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imewataka wanawake wanaogombea nafasi  mbali mbali za uongozi kutoa taarifa mapema za vitendo vya rushwa kwani kuna sheria inayomlinda shahidi na mtoa taarifa.

 Akizungumza katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa Habari Afisa Elimu na kinga   kutoka ZAECA, Yussuf Juma huko  katika  Afisi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar   (TAMWA ZNZ) Tunguu Unguja.

Amesema,  sheria ya ZAECA namba 5 ya mwaka 1992, kifungu cha 98  kinamlinda  mtoa taarifa na kifungu cha 99 kinamlinda shahidi, hivyo ikiwa shahidi utapata ulinzi lakini pia ukiwa mtoa taarifa  sheria inakulinda.

 Amesema kuwa ,  Rushwa ndio kikwazo kikubwa kwa  maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa  , hivyo ni vizuri jamii kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa mapema kabla tukio halijafanyika.

Aidha amesema kuwa, silaha imara dhidi ya rushwa ni kila mtu kujitambua na kujua  thamani yake kwa kufuata sheria na kutokuwa tegemezi

“ Kesi nyingi tunazozipata  huwa zimeshatokea aidha  mtu kaahidiwa ajira kakubali kutoa rushwa hatowi taarifa mpaka atakapokosa hiyo ajira ndipo anakuja kwetu katika hatua za mwisho kabisa”  amesema  Yussuf.

Amesema  kuwa,   vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi vinatokea lakini taarifa hazifiki kwao “rushwa ya ngono ipo lakini haizungumzwi kwa sababu watu wanaichukulia kama Jambo la kawaida “ amesema .

Aidha amewataka viongozi wanaogombea  nafasi mbali mbali  za uongozi kufuata  sheria na taratibu za nchi na za uchaguzi ili wasiwe wao ndio visababishi vya rushwa.

 “ Sababu kubwa za kutokea kwa rushwa ni kuvunja sheria na taratibu na kanuni, kwani mtu ili agombee lazima  awe na sifa za kugombea  “ amasema.

Nae, Mwezeshaji wa mafunzo hayo Asha Abdi Makame amewataka waandishi wa Habari kuandika habari za  mafanikioz za wanawake viongozi waliofanikiwa kuleta maendeleo.

Amesema kuwa, kazi kubwa ya waandishi wa Habari ni kuibua na kutetea haki za wanawake, hivyo ni vizuri  kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa wanawake kugombea nafasi za uongozi.

“ Jamii bado  haina uwelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa wanawake kuwa viongozi, hivyo ni vyema waandishi wa habari kuandika Makala na Habari za wanawake waliofanya vizuri kwenye uongozi ili waonekanae “ ameshauri  .

 Nao baadhi ya waandishi walioshiriki  mafunzo hayo,  Maryam Naasor amewashauri waandishi wachanga  waliopata mafunzo hayo, kujitoa zaidi ili kufanikiwa  katika kazi zao.

Amewataka waandishi hao , kushirikiana na waandishi wengine ambao wazoefu  wapo katika mradi huo ili kupata urahisi wa kazi zao.

Awali  mafunzo hayo, yalifunguliwa na Afisa program wa mafunzo hayo ya waandishi  wa Habari wachanga (Young Media Fellows)   Tatu Ali ambapo aliwataka waandishi wa mradi huo kuendelea kuandika Habari za wanawake na uongozi hasa kipindi kinachoelekea cha uchaguzi.

Mafunzo  hayo ya siku moja ,  yamewashirikisha  waandishi wa Habari 14 wa unguja kutoka vyombo mbali mbali vya Habari nchini ikiwa ni muendelezo wa mradi wa YMF kutoka TAMWA ZNZ.

No comments

Powered by Blogger.