WAANDISHI WATAKAO GOMBEA NAFASI ZA UONGOZI WAONDOKE KATIKA VYUMBA VYA HABARI- MCT



NA MARYAM NASSOR

WAANDISHI wa Habari   nchini wanaojihusisha na masuala ya siasa wametakiwa kuondoka katika vyumba vya Habari ili kuepusha mgongano wa kimaslahi.

Akizungumza na wandishi wa Habari  katika Afisi za Chama Cha Wandishi wa Habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ)   huko Tunguu,  Mjumbe wa Kamati ya Maswala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) bi Hawra Shamte.

Akisoma muongozo, wa Baraza la Habari Tanzania  (MCT) uliyotolewa mwaka huu 2025 na kutiwa Saini na Mkurugenzi wa Baraza hilo , bi Hawra Shamte  amesema kila raia wa nchi hii ana haki ya kugombea.

Amesema , Katiba ya Jamuhuri ya  Muungano wa Tanzania  ya mwaka  1977 ibara ya (21)  inampa kila raia  haki ya kugombea  nafasi za kisiasa , ibara hiyo inasema kila raia  wa  Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  anastahili  kushiriki katika  Serikali ya nchi hii ama moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliyochaguliwa kwa hiari yake kwa kufuata utaratibu uliyowekwa na sheria hii inajumuisha haki ya kupiga kura na kugombea katika chaguzi mbali mbali

Amesema kuwa, kwa hali hiyo wandishi wa Habari wana haki ya kugombea  nafasi za kisiasa  kama ilivyo kwa raia wengine, hata hivyo kuendelea  kuwa mwandishi wa Habari  huku ukijihusisha na siasa ni kinyume  na maadili ya taaluma ya Habari.

Kwa mujibu  wa muongozo huo wa  ( MCT)  mwandishi  anayegombea nafasi ya kisiasa anapaswa kuondoka kwenye  chumba cha Habari ili kuepuka  mgongano wa  kimaslahi na kupoteza uwaminifu kwa umma.

 Anaendelea kusema kuwa, wandishi wa Habari wanaojihusisha  na siasa kwa kugombea nafasi za uongozi  huku wakiendelea na kazi yao, wanakabiliwa na athari kubwa kwa taaluma yao , na tasnia ya habari.

“ Kwa mfano mwandishi wa Habari kagombea Chama cha ACT yeye ni mwandishi wa Habari  lakini anapokwenda kuchukuwa Habari Chama cha Mapinduzi  ( CCM )   atakataliwa  kwa sababu hawatamuamini kwa hiyo huo sio uwandishi” amesema.

Amesema mwandishi wa Habari hapaswi kuwa na upendeleo, sasa unapokuwa na mapenzi makubwa ya chama kiasi cha kugombea unaonekana na  wewe huwezi kufanya haki wakati ukiandika Habari zako, unaonekana hutendi uwaminifu katika kazi  na  unaitia dosari taaluma.

Aidha amesema kuwa,  unapotaka kuwa mwanasiasa kindaki ndaki   bora  kazi ya habari uiyache  kwa muda  ili kuepuka mgongano  ya kimaslahi na kupoteza uwaminifu kwa umma na jamii kwa ujumla.   

 Awali katika kikao hicho, Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dk Mzuri Isaa amewashukuru wajumbe wa baraza la wawakilishi ambao kwa namna moja au nyengine wameuliza maswali kuhusu sheria ya Habari.

Amesema kuwa, ZAMECO itaendelea kushirikiana na wajumbe wa baraza hilo ili kuona sheria  nzuri na rafiki ya Habari inapatikana.

“ Katika kipindi tunachoelekea wandishi wa Habari mara nyingi wanakumbana na matukio ya  kiusalama hivyo ni vizuri tungepata sheria mpya na rafiki ili kuwalinda wandishi wanapotimiza majukumu yao” amesema .

Nae, bi Shifaa Saidi mjumbe wa ZAMECO amesema kuwa,  kuelekea katika uchaguzi mkuu ni vyema wandishi wa Habari wakafanya kazi kwa mashirikianao.

Aidha amewataka , wandishi wa Habari watakaopata matatizo kuelekea kipindi cha uchaguzi  ni vyema wakatoa taarifa mapema ili kuweza kusaidiwa.

Nae, mwakilishi wa jimbo la Pandani Pemba Profesa  Omar Fakih amewataka ZAMECO kuendelea kufanya uchechemuzi wa sheria rafiki ya habari  kwani sheria inayotumika sasa ni ya zamani tokea miaka ya 1988 na haiendani na wakati.

Amesema kuwa, sheria hiyo tayari imeshaanza kuzungumzwa katika baraza la wawakilishi na anaimani muda si mrefu ujayo sheria hiyo itamfikia Spika wa baraza hilo.

Nao, Baadhi ya Wandishi wa Habari waliopata nafasi ya kuchangia katika  kikao hicho wamesisitiza  kuwa, wandishi wa Habari kuendelea kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano na kulindana wakati wa matatizo.

Kikao hicho cha siku moja kimeandaliwa na kamati ya Maswala ya Habari (ZAMECO)  kimewashirikisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ( B L W)   na wandishi wa Habari .



No comments

Powered by Blogger.