UKOSEFU WA WATAALAMU WA AFYA BADO NI KITENDAWILI KWA WAKAAZI WA KISIWA CHA UZI.
NA MARYAM NASSOR
KISIWA cha Uzi kiko pembezoni mwa kisiwa cha Unguja kina mkoa wa kusini, kina shehia mbili zenye wakazi 4,233.
Shehia hizo ni
Uzi yenye wakaazi 3,075 (wanawake 1,510 na wanaume 1,565) na
Ng’ambwa yenye wakazi 1,158 (wanawake 571 na wanaume 587). Wote wanategemea
Kituo cha Afya cha Uzi kupata huduma za
afya.
Kituo cha Afya cha Uzi kinachotoa huduma za matibabu
muda saa za kazi tu; kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri siku za
wiki (Jumatatu hadi Ijumaa). Wikiendi hakuna huduma inayotolewa kituoni huko.
Uzi ni
miongoni mwa visiwa 52 vinavyoizunguka Zanzibar (saba vinakaliwa na watu vikiwa na
huduma muhimu kama vile umeme, maji na vituo vya afya).
Kilio
kikubwa cha wakazi wa kisiwani Uzi ni kukosekana kwa watoa
huduma za Afya ya uzazi, jambo wanaloliona
linaweka hatarini maisha ya
mama na mtoto.
Furaha
Yassin (36) mkazi wa kisiwa hicho, anasema alishuhudia
kwa macho yake vifaa vinaondoshwa katika kituo
hicho chaAfya.
Anasema kuwa, vitu vyengine vilipakiwa kwenye
gari hawakujua wapi vinapelekwa ,
wakabaki wanajiuliza vinapelekwa wapi .
“ Kwa hiyo
mpaka sasa watu wanaendelea kuzaa katika
maboti binafsi yangu alikuja mgeni tukamuuguza kwa uchungu tukatafuta gari
ikabidi tumtie kwenye faiba akazaa kwenye chombo hicho”
Anasema
kuwa, Jengo zuri la Hospitali wanalo lakini hawana madaktari wa kuwahudumia
wananchi wa kisiwa hicho.
Jokha Salim
( si jina lake halisi ) almanusura
apoteze uhai baada ya kujifungua akiwa katika boti saa nane usiku wakati
akipelekwa kupata huduma nje ya kisiwa hicho.
"Ninakumbuka
ilikuwa may mwaka jana , saa
sita za usiku uchungu umenikaza kituo chetu cha afya
hakifanyi kazi kwa muda huo lakini pia hakina daktari wa huduma ya mama ya kujifungua," anasimulia Jokha .
Mama huyo
mwenye watoto wanne anasimulia Wakati
uchungu umekaza, maji ya bahari nayo yameshafungamana kisiwani huwezi kutumia mtumbwi wa kawaida kutoka nje
ya kisiwa lazima utumie usafiri wa boti.
Usafiri unaotumika kisiwani hapa ni gari au bodaboda (pikipiki) kwa nyakati ambazo maji ya bahari hayajaingia kisiwani na kufunga Barabara Kutoka hapa Uzi hadi kijiji cha Unguja Ukuu ni wastani wa kilomita tatu.
Jokha anasema kuwa wakiwa katikati ya bahari,
akipelekwa Kituo cha Afya Unguja Ukuu, alijifungua chini ya usimamizi wa mkunga
wa jadi aliyemsindikiza.
"Wakati
ninatoka nyumbani kwangu, niliongozana na baadhi ya wanafamilia pamoja na
mkunga wa jadi ambaye hutusaidia kutuzalisha wakati wa dharura hapa kisiwani ’’
Anasema.
Anasema kuwa, Ni jambo la kusikitisha kwamba,
kisiwa cha Uzi kina kituo cha afya kizuri, chenye vifaa tiba, lakini hakina
wataalamu wa huduma za uzazi.
"Hii
kero inatukwaza na kutudhalilisha sisi wanawake kwa sababu wakati wa kujifungua
kunahitaji faragha chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya.
"Kwa
kweli siku ile sitoisahau maishani mwangu, kujifungua katika boti! Lakini
ninamshukuru Mungu alinisaidia nikajifungua salama mtoto wangu wa kike ambaye
hivi sasa anakaribia kutimiza umri wa mwaka mmoja," anasema Jokha .
Mkasa wa Jokha
unafanana na wa Zakia
Ali (32), mama wa watoto wa wawili na mkazi wa kisiwa
hicho aliyejifungua ndani ya gari wakati akiwahishwa Hospitali ya Unguja Ukuu
nje ya kisiwa hicho.
"Mwaka (2024), nikiwa na ujauzito wa mtoto wangu wa
tano, nilijifungua ndani ya gari mchana kweupe baada ya kukosa wataalamu wa
afya katika Kituo cha Afya Uzi.
Anasema kuwa, Wakazi wa kisiwa hiki wanapobeba
ujauzito huwa na hofu kutokana na kituo kutokuwa na wataalamu wa uzazi, hivyo
baadhi hulazimika kuyahama makazi yao wanapokaribia kujifungua kwa kwenda
kuishi kwa ndugu na jamaa nje ya kisiwa hiki.
"Mimi mimba zangu zote nimejifungua kwa wakunga wa jadi hapa kisiwani. Hii mimba yangu ya mtoto wa tano nilitaka nijifungulie hospitalini kwa sababu wakunga wa jadi sasa wamekatazwa kuzalisha, lakini sikufika hospitalini, nikajifungua ndani ya gari.
Fadhili Omar
(40) baba wa watoto watano mkaazi wa kisiwa
hicho, anasema kituo chao kina daktari mmoja, hivyo wanahitaji wataalamu wa
afya wa kutosha na wawepo kituoni muda wote ili wake zao wasijifungulie kwa
wakunga wa jadi.
"Tatizo
hili haliwaumizi wanawake tu, hata sisi wanaume linatuumiza, tunapata tabu sana
katika kupata huduma. Mimi binafsi nilikwenda na mke wangu katika kituo hicho
ili apate huduma ya kujifungua lakini kutokana na kituo kutokuwa na wataalamu
wa uzazi, nilimsafirisha kumpeleka Kituo cha Afya Unguja Ukuu tulipofika tu akajifungua.
"Kama
tungechelewa kidogo tu kumfikisha Kituo cha Afya Unguja Ukuu, angejifungulia
njiani. Kama hatuna wataalamu wa afya, ninafikiri serikali iendelee kuwapa fursa
wakunga wa jadi kuzalisha ili kuwasaidia wajawazito kisiwani kwetu,"
anasema Fadhil.
UONGOZI WA
SHEHIA
Othman
Mwinyi Haji, Sheha wa Shehia ya Uzi, anakiri kuwepo changamoto ya wataalamu wa
afya katika Kituo cha Afya Uzi, akisema: "Kituo chetu cha afya ni kizuri
mno, tumejengewa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Kina
vifaa tiba vinavyohitajika na tena tuna mpaka nyumba za kuishi madaktari,
lakini kituo hakitoi huduma kwa saa 24.
"Nyumba
za madaktari zilizoko hawaishi na hao wachache waliopo katika kituo chetu cha
afya wanakuja na kuondoka. Changamoto hii tumeshaiwasilisha katika ngazi za juu
serikalini, wananchi kuendelea kuvumilia, serikali itatatua changamoto hii.
"Nyakati
za usiku wananchi wa kisiwa hii, hasa wajawazito wanapata shida kutafuta huduma
za afya na wakati mwingine hulazimika kujifungulia njiani kabla ya kufikishwa
hospitalini au kujifungulia kwa wakunga wa jadi, jambo ambalo ni hatari kwa
afya ya mama na mtoto."
WASIMAMIZI
WA KITUO
Daktari
Dhamana wa Kituo cha Afya Uzi, Seleh Nila Ali, anasema changamoto iliyopo ni
uhaba wa wafanyakazi, hasa kwa wakunga. Kituo hicho kina mkunga mmoja na
kutokana na uhaba wa wataalamu wa afya kinashindwa kuwazalisha wajawazito.
Anabainisha
kuwa kwa mwezi kituo kinatoa huduma kwa wastani wa watu 500 wanaofika kup ata
huduma kituoni hapo.
Daktari huyo
anasema kituo kina upungufu wa wakunga watano na madaktari watatu ili kukidhi
mahitaji ya kutoa huduma za afya. Anakiri ni kero kubwa kisiwani huko kujifungulia kwa wakunga wa
jadi.
Mkurugenzi Kinga kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk
Salim Slim amesema Serikali
itahakikisha inapeleka wataalamu wa Afya wa kutosha katika kituo hicho.
‘’
Ingawa hatutomaliza tatizo hilo kwa
asilimia mia moja lakini tutalipunguza kwani hakuna nchi hata moja
waliofanikiwa kutatua changamoto za afya kwa asilimia mia’’ amesema Dk Salim.
Aidha amesema kuwa, suala la wafanyakazi bado
lina changamoto lakini wanaahidi wafanyakazi katika kituo hicho watapelekwa
hivi karibuni.
mwisho
Post a Comment