MATUMAINI YA WADAU WA HABARI YAKO KWA KAMATI YA UFUNDI YA TAIFA “NATIONAL TECHNICAL COMETEE" (NTC)



NA ASIA MWALIM

LICHA ya waandishi wa habari kutajwa kuwa ni daraja la mafanikio kati ya jamii na serikali lakini katika kisiwa cha Unguja na Pemba bado wamekua wakikosa mueleko mzuri katika utendaji wa kazi zao kutokana na kukosa sheria bora na rafiki.

 

Takriban miaka 10 sasa wadau wa habari na waandishi wa habari Zanzibar wanalililia mabadiliko ya sheria za habari zanzibar ambazo ndani yake kuna vifungu vinavyokwaza na kuminya uhuru wa habari.

Wadau hao ni pamoja na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ZNZ (TAMWA) Baraza la Habari Tanzania (MCT) Zanzibar Press Club, (ZPC) Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) lakini hawajakata tamaa kutokana na ahadi wanazopewa na viongozi wa serikali ya awamu ya nane.

Kwa sasa waandishi wa habari na wadau wa masuala ya habari matumaini yao wameyaelekeza kwa Kamati ya Ufundi ya Taifa (NTC) kutokana na maelezo ya Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, aliyoyatoa katika mkutano wa waandishi wa habari katika kikao cha Tathmini ya mafanikio ya miaka minne ya Dk. Hussein Ali Mwinyi ambapo amesema, Mswaada wa Sheria ya habari upo katika Kamati ya Ufundi ya Taifa (NTC) unashughulikiwa.

Katika hatua nyengine Waziri huyo amesema anatamani mswaada huo ufikishwe katika Baraza la Wawakilishi, “natamani mswaada huu ufikishwe katika Baraza la Wawakilishi hivi karibuni”.

WADAU WA HABARI

Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) Dk.Mzuri Issa Ali anasema kwa sasa matumai makubwa ya wadau wa habari na waaandishi wa habari yapo kwa kamati ya ufundi ya Taifa ambayo mswaada wa sheria ya habari upo.

Akitaja baadhi ya sheria wanazotamani kufanyiwa marekebisho kwa haraka ni pampja na Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997, hasa kutokana na kukosekana kwa maana halisi katika baadhi ya vifungu.

Sheria nyengine ni ile ya Tume ya Utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 1 ya mwaka 2010.

Anasema umefika wakati sasa wizara husika kulipa umuhimu sulala hilo ambalo limeshatolewa ahadi na maelezo mara kadhaa ili kupata sheria rafiki za habari ambazo zinaendana na wakati.

Anasema jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya sheria zinachukua muda mfupi kufanyiwa marekebisho lakini nyengine ikiwemo sheria za habari zimechukua muda mrefu, jambo ambalo si jema. 

“Kuwepo sheria rafiki ya habari kutapelekea uhuru wa kujieleza, kutoa maoni na kuimarika huduma za kijamii na kimaendeleo kwa ujumla ni haki yetu kupata sheria zilizobora” anasema Dk.Mzuri.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Habari za Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) wanasema wakati umefika kwa watunga sheria kusikiliza kilio hicho cha wadau na waandishi wa habari cha kutaka kupitishwa sheria mpya ambayo imefika kwa Kamati ya Ufundi ya Taifa (NTC) ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

“Jambo la sheria halitokua na msaada kwetu tu na serikali pia itanufaika kutokana na baadhi ya maoni yatakayotolewa na wnanchi yatawajenga watawala” anasema.

Afisa Mradi wa Sheria za Habari kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) Zaina Mzee anasema kuwepo kwa sheria rafiki ya Habari kutapelekea uhuru wa kujieleza na kuimarika huduma mbali mbali za kijamii hatimae kupata maendeleo.

“waandishi wa habari hatupaswi kukataa tamaa tunapaswa kushirikiana kwenye hili ili kufanya uchechemuzi wenye nia ya kuleta mabadiliko”anasema.

Anafafanua kuwa sheria ya adhabu namba 6 ya mwaka 2018 kifungu cha 31 kinachoeleza kuwa “Mtu yeyote amabae ametia nia ya kufanya moja kati ya makusidio ikiwemo (e)kuanzisha vita dhi ya Zanzibar na kuionesha nia hiyo kwa kitendo cha dhahiri au kwa dhahiri au kwa kuchapisha chapisho lolote au maandishi atakua ni mkosa na atapewa adhabu ya kifungo cha maisha.

Kifungu hichi kinaonesha vitisho vya wazi kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa kupewa adhabu ya juu endaponwataandika jambo ambalo litatafsiriwa kuwa ni kuanzisha vita dhidi ya serikali ikiwa watapatikana na hatia, aya hii ni vyema ikafutwa kwa sababu inakinzana na haki ya kujieleza.

 WAANDISHI WA HABARI

Issa Yussuf mwaandishi wa habari Mkongwe Zanzibar anasema sheria za habari zinazotumika Zanzibar haziendani na wakati huu ni vyema kufanyiwa marekebisho ili waandishi kupata fursa ya kufanya kazi zao kwa weledi.

Anasema mswaadaa huo wa habari umechukua muda mrefu kupelekwa Baraza la Wawakilishi jambo ambalo linawanyima amani wadau wa habari na waandishi wa habari. “Tunatamani mswaada huo ifikie siku usomwe maana ahadi zinazotolewa zishakuwa nyingi” anasema.

Ahmed Abdullah muandishi wa habari kijana kutoka zenji Fm redio, anasema jinsi ilivyo hivi sasa uhuru unapewa lakini hapo hapo unapokonywa, akidai hali ya ukinzani uliopo kati ya haki zinazotolewa na katiba ya Zanzibar 1984 na vizingi vilivyowekwa na sheria za habari. 

Jambo hili sio sahihi linahitaji mabadiliko na wahusika wa hili waliangile kwa jicho la tatu, akimaanisha kwa umakini wa hali ya juu zaidi.

WANASHERIA

Harusi Mpatani mwanasheria kutoka Zanzibar anasema katika nchi yeyote duniani haiwezinkupata maendeleo pasipo na sheria rafiki zinazowaongoza waandishi wa habari ambao wananafasi ya kutangaza mazuri na mabaya yanayofanywa nchini.

“yombo vya habari vina msaada mkubwa sana kama nia ya serikali ya Zanzibar ya kutangaza na kukuza uwekezaji kwenye maeneo mbali mbali ikiwemo Zanzibar SUKUKI amabyo imetangazwa ndani na nje ya nchi inatarajiwa kufanikiwa”

Anaeleza kuwa katika kikao cha wajumbe wa Baraza la Habari Tanzania, MCT na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi kilichofanyika Disemba 22, mwaka 2023 huko Ikulu Zanzibar kilitoa matumaini.

“Dk.Mwinyi,alinukuliwa akikiri mbele ya ujumbe wa MCT kuwa sheria za habari za Zanzibar ni za muda mrefu na hivyo serikali yake kwa kushirikiana na wadau wa habari itaendelea kuzifanyia kazi pendekezo walilipoleka wadau wa habari ili kuwe na sheria nzuri zaidi”alisema.

MWISHO

 

No comments

Powered by Blogger.