MAREKEBISHO YA SHERIA ZA HABARI YAENDANE NA MIKATABA YA KIMATAIFA
NA ASIA MWALIM
UHURU wa kujieleza na kupata habari ni miongoni mwa mambo ya msingi na muhimu kwa binadamu yeyote duniani, kutokana na umuhimu huo ndio maana kukatengenezwa utaratibu wa kuheshimu uhuru wa kila mmoja katika ngazi za kimataifa,kikanda na kitaifa.
Tanzania, kama nchi mwanachama wa jumuiya mbalimbali za kimataifa na kikanda, imeridhia mikataba kadhaa inayolinda na kusimamia masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.
Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia mikataba hiyo ambayo inalinda masuala hayo muhimu lakini bado inakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wake kutokana na kutumia sheria kandamizi zilizotungwa muda mrefu hivyo ndiyo kusema kuwa zimepitwa na wakati.
Kwa upande wa Tanzania Bara, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ilifutwa na kutungwa sheria mpya ya Huduma za Habari mwaka 2016 ambapo kwa Zanzibar Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na.5 ya mwaka 1988 ilifanyiwa marekebisho na Sheria Na.8 ya1997 mpaka leo haijabadilishwa pamoja na kuwapo vilio vya wadau kutaka sheria hiyo ibadilishwe kwa sababu imepitwa na wakati.
Sheria nyingine ambayo imekua ikipigiwa kelele ni ile ya Tume ya Utangazaji Namba 7 ya mwaka 1997 ambayo nayo ni kongwe na imekua ikiwanyima wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
MIKATABA YA KIMATAIFA NA
KIKANDA
Baadhi ya mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu (UDHR)Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) na imeridhia Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948. Katika tamko hili, kuna vifungu vinavyohusiana na uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa.
Katika sheria hiyo Kifungu cha 19 kinatoa haki kwa kila mtu kutoa mawazo yake bila kuingiliwa.
Mkataba mwingine ni ule wa Kimataifa juu ya Haki za Raia na Kisiasa (ICCPR). Mkataba huu unalinda haki za raia, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza. Tanzania iliridhia mkataba huu mwaka 1976, ikitambua umuhimu wa kulinda haki hizi katika mfumo wake wa kisheria.
Mkataba mwingine ni wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu; Tanzania pia ni mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na iliridhia Mkataba huu mwaka 1986. Mkataba huu unasisitiza umuhimu wa uhuru wa kujieleza kama sehemu ya haki za binadamu.
MIKATABA YA KIKANDA
Sera ya Maendeleo ya Habari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ; sera hii inalenga kukuza uhuru wa vyombo vya habari katika nchi wanachama, ikiwamo Tanzania. Sera hii inatoa mwongozo juu ya jinsi vyombo vya habari vinavyopaswa kufanya kazi bila kuingiliwa.
SHERIA ZA NDANI
Katika ngazi ya kitaifa, Tanzania ina sheria kadhaa zinazohusiana na uhuru wa vyombo vya habari,i kiwamo Sheria ya Huduma za Habari, Iliyopitishwa mwaka 2016 Tanzania Bara), sheria hii inasimamia uendeshaji wa vyombo vya habari nchini pamoja na Sheria ya Uhuru wa Kujieleza.
Zanzibar ina sheria mbili kubwa zinazoongoza waandishi wa habari nazo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Namba 5 ya mwaka 1988 na marekebisho yake Namba 8 ya mwaka 1997 pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji Namba 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebishona Sheria Namba 1 ya mwaka 2010; hizi ni sheria kongwe na zinawakwaza waandishi na wa habari na vyombo vyao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
WADAU WA HAKI ZA
BINAADAMU.
Shadida Omar kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania -THRDC anasema nchi yoyote inayokwenda kinyume na mikataba iliyosaini matokeo yake ni kukiuka haki za wananchi .
Anasema Tanzania-Zanzibar imeona umuhimu wa kuridhia mikataba hiyo na ikiona haiwezi kufuata utekelezaji wake ni vyema kujitoa moja kwa moja kwani imeshindwa kutekeleza yaliyomo katika mikataba iliyoiridhia.
“kutokana na umuhimu wa mikataba hiyo ndio maana kukatengenezwa utaratibu wa kuheshimu uhuru wa kila mmoja katika ngazi za kimataifa, kikanda na kitaifa ili kutoa fursa kwa wananchi popote walipo dunianikufaidi haki hizo za msingi;” anasema.
WAANDISHI WA HABARI
Zulekha Fatawi mwandishi wa habari wa gaazeti la Mwananchi anasema, sheria zinazotumika ni kama zinakiuka Katiba ya Zanzibar, si hasha kukiuka hata mikataba ya kimataifa, hivyo alitoa rai ya kuiheshimu mikataba kwenye kutunga na kusimamia sheria za waandishi wa habari.
“Sasa ikiwa kuna sheria ambazo zitakwenda kinyume na mikataba ya Kimataifa na kikanda hapo ni kukiuka masharti ya mikataba hiyo,” anasema.
Alibainisha kuwa ni muhimu mabadiliko ya sheria za habari kufanyika kwani itasaidia kuifanya Zanzibar kuendana na mikataba ya kikanda na kimataifa hatimaye kupiga hatua katika tasnia ya habari na maendeleo ya nchi kiujumla.
WADAU WA HABARI
Zaina Ali Mzee, Afisa Programu wa Chama Cha Waandishi Wahabari Wanawake Tanzania-Zanzibar (TAMWA ZNZ) anasema licha ya mikataba hiyo kuwapo ni kama kivuli, kwa jinsi ilivyo hivi sasa ni kwamba uhuru unapewa kwa mkono wa kulia lakini hapo hapo unapokonywa kwa mkono wa kushoto, anadai kuwa hakuna majibu ya jambo hilo kwa kiufupi sheria hizio hazifa.
Anafafanua kuwa ukinzani uliopo kati ya haki zinazotolewa na katiba na vizingiti vilivyowekwa na sheria zinazoongoza uandishi wa habari, tunahitaji kufanya mabadiliko ilikwenda sambamba na mikataba.
Katibu Mtendaji Baraza la
Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, anasema moja ya mambo
muhimu aliyoyazungumza Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Hussein Ali Mwinyi ni kuzifanyia marekebisho sheria zote zilizopitwa na
muda.
“Sera za taifa zinatutaka tuwe na sheria jumuishi na rafiki ili kupata utekelezaji mtambuks kstiks majukumu ya msingi katika taifa ikiwemo suala la kupashana habari” anasema Debe.
Anasema sheria mpya itasaidia watu wenye ulemavu kupata fursa zote ikiwamo ya kutoa maoni yao na kupokea taarifa mbali mbali ambazo wengine wasingeweza kufika kwenye maeneo husika kutokana na hali zao.
Mratibu wa Jumuiya ya Wasiiona Zanzibar Adil Muhammed Ali, anasema ukandamizwaji wa waandishi wa habari hudhoofisha maendeleo ya taifa ni vyema kupata sheria bora ya habari ili kuchangia kuwa na jamii bora inayofanya maamuzi sahihi.
Mwenyekiti wa Zanzibar Press Club (ZPC) Abdallah Mfaume anasema, pamoja na mabadiliko makubwa yaliyotokea nchini, ambapo nchi sasa hivi inafuata uchumi huria na kubarikiwa na wingi wa mitandao ya kijamii hivyo sheria hizo kuu ikwemo Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magzeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997 na sheria ya Tume ya Utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 na marekebisho yake ya sheria namba 1 ya mwaka 2010 haziendani na ikataba ya kitafa na kimataifa ambayo imesainiwa.
WIZARA YA HABARI
Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, alipokua katika kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali wa Tanzania bara na Zanzibar April 3 mwaka huu, alisema wanategemea kwenda kuisoma sheria ya habari ya Zanzibar, wanatarajia kuipitisha, na kuupeleka muswada katika kikao cha Baraza la Wawakilishi la hivi karibuni.
Aidha alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah kuendelea kuisimamia sheria hiyo iweze kupita ili Zanzibar ipate sheria iliyokamilika ‘instrument’ ya kuwasimamia maafisa wa habari.
“Tunategemea sana leo April 3 mwaka 2025 kwenda kuisoma sheria yetu ya habari ya Zanzibar jambo ambalo litasaidia katika kusimamia maafisa wetu wa habari,” anasema
Akitoa salamu za Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mkurgenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhan Abdalla, katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyoandaliwa na Kamati ya Wataamalu wa Masuala ya Sheria Zanzibra ZAMECO Mei 17, 2025 amesema suala la marekebisho ya sheria za habari Zanzibar litafika mwishoni muda sio mrefu hasa kutokana na msukumo wanaoufanya waandishi wa habari.
Anasema ni vyema waandishi na wadau wa habari kuondoa hofu kwani serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara husika inalisimamia vizuri suala hilo liweze kukamilika.
Aidha anawapongeza waaandishi wa habari kwa kupeleka msuko mkubwa katika suala ziama la marekebisho ya sheria za habari aambalo limekua la muda mrefu.
“Nakumbuka suala hili limeanza muda mrefu tangu nikiwa mwanafunzi wa tasnia hii na nimeshiriki katika mafunzo mbali mbali yalioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutoka Zanzibar na Tanzania bara ” alisema.
Mwisho

Post a Comment