VYAMA VYA SIASA VIMETAKIWA KUWA NA SERA YA JINSIA ILI KUHAKIKISHA USAWA WA KIJINSIA

NA MARYAM NASSOR

VYAMA vya Siasa nchini vimetakiwa kuanzisha  sera  na madawati ya Jinsia katika vyama vyao ili  kuhakikisha usawa wa kijinsia.

Ameyasema hayo,  Afisa  mradi wa kuwawezesha wanawake  katika maswala ya uongozi na haki za kidemokrasia  kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ)  Sabrina Yussuf alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa vyama 19 vya siasa nchini huko  katika  Ofisi kuu za chama hicho Tunguu.

Amesema,  lengo la mafunzo hayo ni kukuza ushiriki wa wanawake katika  maswala ya jinsia,  na kuona namna  gani vyama vya siasa  vinatekeleza mikakati  hiyo ipasavyo  ili kuongeza ushiriki  wa wanawake katika  nafasi za uongozi .

“Mafunzo  haya  yatawasaidia viongozi wa vyama  vya siasa kuwa makini katika kuzitekeleza sheria za vyama vya siasa nchini kwa kuanzisha dawati la jinsia  na   kukuza usawa wa kijinsia katika vyama vyao ,” amesema .

Aidha amesema kuwa,  wameandaa mafunzo ya viongozi wa vyama  vya siasa  kutokana na mabadiliko ya  sheria ya uchaguzi ya mwaka  2024  kifungu no.10 C ambayo kinalazimisha kila chama  cha siasa kuwa na sera  ya jinsia  ndani ya chama.  

Amesema kufuatia hatua hiyo, wameona ipo haja ya kuwapa  mafunzo viongozi hao  ,ili wajuwe namna gani wataazisha madawati ya jinsia ili kuhamasisha ushiriki wa wanawake kugombea nafasi za uongozi.

“Tathimini inaonesha  bado wanawake wako kidogo katika nafasi mbali mbali  za uongozi nchini , kwani mpaka sasa ni asilimia 37 tu ndio ambao  wako katika baraza la wawakilishi” anasema  Sabrina.

Nae, Mkufunzi  katika mafunzo hayo,Dk Sikujua Omar Hamdani amevitaka  vyama vya Siasa kuwa na sera Madhubuti  za kijinsia  na utekelezaji wake ili kushajihisha ushiriki wa wanawake katika kugombea nafasi za uongozi.

Amesema kuwa,  lazima vyama vya siasa viwe na mikakati mbali mbali ya kuimarisha usawa wa kijinsia na kudhibiti vitendo vya udhalilishaji wanavyotendewa wagombea wanawake.

“ Lazima vyama vya siasa kujidhatiti  na kuwa na mikakati maalumu ya  kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili 50/50 ifikiwe” amesema Dk Sikuju.

 Nae, mshiriki  Suleiman  Ali Seif  kutoka Chama cha Act Wazalendo amesema  suala la jinsia katika chama chao limezingatia, kwani  katika baraza lao la Mawaziri kivuli  limewashirikisha jinsia zote.

Amesema kuwa, Chama chao kimekuwa kikihamasisha umuhimu wa dawati la jinsia  ili kuwapa fursa wanawake kugombea kwa wengi katika nafasi za uongozi.

 Nae,  Salma Omar Saidi Katibu   Idara ya Uchaguzi kutoka Chama cha Mapinduzi  (CCM) anasema katika chama chao, sera ya jinsia wanaitekeleza  kwani kila nafasi itakayo tokea wanapendekeza jinsia mbili kugombea.

“Sote mashahidi katika chama chetu kuanzia viongozi wa  ngazi ya Taifa hadi shina ni wanawake na wanahamasisha pia wanawake kugombea katika kila nafasi ya  uongozi” anasema.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandalia na Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) , kwa kushirikiana na  Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar ( JUWAUZA) na PEGAO  kwa upande wa Pemba kimewashirikisha viongozi wa vyama 19  vya siasa nchini na wandishi wa  Habari.

 

                                              Mwisho

No comments

Powered by Blogger.