ATHARI ZINAZOTOKANA NA WENYE MAMLAKA KUFUNGIA VYOMBO VYA HABARI


NA ASIA MWALIM

KATIKA zama hizi za utandawazi inashangaza sana kumnyima mwananchi uhuru wa kujieleza na kutoa maoni yake kwa sababu dunia nzima inafahamu kuwa hiyo ni haki ya msingi ya watu.

Suala la kunyimwa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni bado linaendelezwa hususan hapa Zanzibar kutokana na sheria kongwe zilizopo zinazotumika kwa zaidi ya miaka 30 sasa, kimsingi sheria hizo zimepitwa na wakati kwani kuna mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyosababisha tasnia ya habari kuendelea na hata kuwa huru zaidi.

Wadau wa masuala ya habari Zanzibar wamejitahidi sana kupigia chapuo ili sheria za Habari zilizopitwa na wakati zibadilishwe. 

SHERIA ZA HABARI

Licha ya mabadiko ya kiutandawazi yanayoendelea ulimwenguni bado Zanzibar inaongozwa na sheria kongwe zilizopitwa na wakati ambazo haziendani na wakati tulio nao.

Mfano wa sheria hizo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997.

Chini ya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997, katika kifungu cha 27 (1) kinaeleza kuwa Afisa Polisi yeyote anaweza kukamata gazeti lolote, popote linapopatikana ambalo limechapishwa au ambalo anashuku kuwa limechapishwa.

Hiki ni kifungu chenye matatizo sana na ni miongoni mwa vifungu vilivyonyang’anya haki ya kutoa habari iliyoainishwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inatambua na kulinda uhuru wakujieleza kama moja ya Haki za Binaadamu, Wajibu wa Raia na Misingi ya Uongozi bora.

Ibara ya 25 (1) ya katiba ya Zanzibar inasema “kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kueleza mawazo yake, na anaweza bila ya kuingiliwa, kutafuta, kupokea na kutoa habari na mawazo kwa njia yeyote ilebila ya kujali mipaka”

Kifungu hichi cha katiba kinahakikisha uhuru wa maoni binafsi, kupokea na kusambaza habari, vyombo vya habari kufanya kazi bila ya kuingiliwa.

Aidha kifungu cha 27 (2) kinaeleza Hakimu yeyote anaweza kutoa hati kumuidhinisha Afisa Polisi yeyote wa cheo cha Inspekta kwa msaada au bila ya msaada kuingia na kupekua mahali popote pale ambapo inashukiwa kuwa kuna gazeti linachapishwa kinyume na sheria hii, linafanya kosa chini ya sheria hii au kanuni zozote zilizotungwa ama limefanya, linafanya au linakaribia kufanya kosa...” 

Hivyo Askari Polisi anaweza kukamata gazeti lolote linalopatikana humo ama kwa kushuku kuwa kuna gazeti lilichapishwa au linachapishwa pamoja na ushahidi mwingine wowote wa kutenda kosa chini ya sheria hii au kanuni zozote zitakazopatikana.

“Aidha hata hiyo sentensi ‘kanuni zozote zitakazopatikana’ ni sentensi yenye kuleta mkanganyika, vipi kama waliotunga kanuni watazitunga kwa maslahi yao? ”

Katika zama hizi za utandawazi kifungu hiki hakistahili kuwepo kwa kuwa hakina maslahi na uhuru wa vyombo vya habari ni vyema kifutwe.

Kifungu cha 30 (1) kinasema;Endapo Waziri anaona kuwa ni kwa manufaa ya umma au kwa maslahi ya amani na utulivu anaweza kuamuru kufungiwa kwa gaazeti na gazeti hilo litakoma kuchapishwa kuanzia tarehe iliyotajwa.

Kitendo cha Waziri kufungia gaazeti ni kudhihirisha mamlaka makubwa aliyopewa, mamlaka hayo yalipaswa kupewa bodi ya Huduma za Habari baada ya Waziri kuitaarifu bodi kuhusu uwamuzi wake wa kulisimamisha /kulifungia gaazeti.

 

WAANDISHI WA HABARI

Ahmed Abdullah mwandishi na mwanzilishi wa Zanlight blog, anasema kitendo cha Waziri kupewa mamlaka makubwa na sheria ya kuweza kukifungia chombo cha habari chochote ni sababu ya kuendeleza hali ya umaskini hasa kwa vijana.

Anasema serikali inahamasisha suala la vijana kujiajiri na kujifunza fani mbali mbali lakini sheria hiyo kwa jinsi inavyokandamizi uhuru wahabari, hata wanaotamani kujiunga na fani hiyo wataogopeshwa na hatimaye wataelekea kwenye fani wasizo zipenda.

Najjat Omar mwandishi wa habari wa gazeti la mtandaoni la “The Chanzo” kutoka Zanzibar anasema sheria hiyo inampa nguvu Waziri mwenye dhamana kufungia au kuzuia uchapishwaji wa gaazeti kwa kisingizio cha “maslahi ya umma au amani na utulivu,”anasema.

Aidha anasema sheria haijafafanua ni yepi maslahi ya umma, maslahi ya amani na utulivu jambo ambalo anadai kutoa mwanya kwa wenye mamlaka kukitumia vibaya kifungu hicho cha sheria.

Anafafanua kuwa sheria hiyo pia inampa nguvu Rais wa nchi kuzuiauingizwaji wa chapisho lolote visiwani Zanzibar linaloonekana kuhatarisha ‘maslahi ya amani na utulivu’ pia anaweza kuwafungulia mashtaka watu watakaokutwa na chapisho lilozuiwa kuingia nchini.

Alitoa mfano wa kufungwa gazeti moja alilowahi kulifanyia kazi na kusema vijana na familia nyingi zilitetereka kwenye uchumi baada ya kukosa ajira baada ya chombo cha habari kuzuiliwa kufanya kazi zake.

WANASHERIA

Afisa Miradi kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Benny Louis Mlingi, anasema suala la kupashana habari ni muhimu; endapo kituo cha utangazaji, au wachapishaji wa nakala wameteleza wanapaswa kuitwa na kueleweshwa na sio kuchukuliwa hatua ya kufungwa kituo. 

“Miezi michache iliyopita nilipata taarifa ya kufungwa kituo cha utangazaji kule chukwani, “Bomba FM” jambo kama hilo linaleta athari kubwa katika maendeleo ni vyema kuwe na sheria rafiki angalau inayo weka nafasi ya kuwapa onyo wanaodaiwa kutenda kosa na kupewa muda wa kujirekebisha,” anasema Benny.


WADAU WA HABARI

Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania -Zanzibar (TAMWA ZNZ)Dk. Mzuri Issa Ali anasema kuna umuhimu gani wa kudhubiti vyombo vya habari wakati kuna mitandao ya jamii kibao inafanya kazi kwenye jamii, ambayo inakwenda sambamba  na mabadiliko ya kidunia? Anahoji.

“Kama kweli viongozi wetu wanafikiri zaidi wasingeweza kudhibiti namna hii kwenye sheria na wanasahau kwamba dunia ya sasa inakwenda na wakati na watu wengi wako kwenye mitandao ya kijamii,” anasema.

Anaongeza kuwa “wanasahau kwamba dunia nzima sasa hivi imejielekeza katiaka mitandao ya kijamii, tukiendelea na sheria hizi kandamizi tutaonekana watu wa ajabu sana huko duniani”.

Shifaa Said Hassan,aliyekua Mjumbe wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Zanzibar anasema vifungu hivyo vinapaswa kuondoshwa kwani kina kandamiza uhuru wa habari na ni vigumu kubaini maana ya “dhana na shauku”tunashauri kiondoshwe. 

Mwanahabari mkongwe Hawra Shamte anasema suala hilo linapaswa kupelekwa katika bodi ya ushauri litolewe uamuzi na ikishindikana lipelekwe mahakamani na hapo ndipo mahakama itoe hati ya upekuzi si vyema afisa wa polisi kupekua bila ya jambo hilo kuthibitishwa.

“Afisa Polisi wa ngazi yeyote asichukue jukumu la kupekua na kukamata kabla ya lalamiko kuthibitishwa, Ikiwa kuna tatizo katika gaazeti utaratibu wa kawaida wa ukaguzi unapaswa kuzingatiwa na sio vyenginevyo au kutumika njia nyengine wanayoitaka” alisema.

Anaeleza kuwa Waziri amepewa mamlaka makubwa ya kuamua kufungia magazeti, kifungu hiki hakina maslahi na uhuru wa habari.

“Mamlaka haya yalipaswa kupewa Bodi ya Huduma za Habari baada ya Waziri kuitaarifu bodi kuhusu uamuzi wake wa kulisimamisha au kulifungia gazeti,” anasema.

Mratibu wa Baraza la Habari Tanzania-Zanzibar (MCT) Ziada Ahmed Kilobo, anasema ni wajibu wa serikali kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya waandishi wa habari ikiwemo kupatikana sheria mpya na rafiki za habar ili kufanya kazi zao kwa weledi.

WAFANYABIASHARA WA BIDHAA ZA MAGAZETI

Mfanyabiashara wa magazeti aliekataa kutajwa majina yake eneo la Malindi mjini Unguja, anasema mamlaka makubwa aliyonayo Waziri kufungia chombo cha habari yanaweza kusababisha mfarakano kwa jamii, ukosefu wa ajira kwa vijana, kupunguza soko la wateja na mara nyingine kupata idadi kubwa ya wagonjwa wa akili.

“Mtu anapokosa kazi yake aliyoizoea katika kujipatia riziki anaweza kuchanganyikiwa kutokana na hali ngumu ya kimaisha wakati huo huo ana familia ya mke na watoto inamtegemea,” anasema.

WIZARA YA HABARI

Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, alipokua katika kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali wa Tanzania bara na Zanzibar April 3 mwaka huu, alisema wanategemea kwenda kuisoma sheria ya habari ya Zanzibar, wanatajia kuipitisha na kuipeleka mswaada katika kikao cha baraza la Wawakilishi la hivi karibuni.

Aidha alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah kuendelea kuisimamia sheria hiyo iweze kupita ili Zanzibar ipate hati rasmi iliyokamilika ya kuwasimamia maafisa wa habari. 

Akitoa salamu za Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mkurgenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhan Abdallah, katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyoandaliwa na Kamati ya Wataamalu wa Masuala ya Sheria Zanzibra (ZAMECO) Mei 17, 2025 amesema suala la marekebisho ya sheria za habari Zanzibar litafika mwishoni muda sio mrefu hasa kutokana na msukumo wanaoufanya waandishi wa habari.

Anasema ni vyema waandishi na wadau wa habari kuondoa hofu kwani serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara husika inalisimamia vizuri suala hilo liweze kukamilika.

Aidha aliwapongeza waaandishi wa habari kwa kupeleka msuko mkubwa katika suala ziama la marekebisho ya sheria za habari aambalo limekua la muda mrefu.

“Nakumbuka suala hili limeanza muda mrefu tangu nikiwa mwanafunzi wa tasnai hii na nimeshiriki katika mafunzo mbali mbali yalioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutoka Zanzibar na Tanzania bara ” alisema.

Anafahamisha kuwa mtazamo wa wizara hiyo ni kuwawekea mazingira mazuri wanahabari na vyombo vya habari katika sera na sheria ya habari.

Akizungumzia kuhusu sera ya vyombo vya habari anasema, tayari imeshakamilika tangu mwaka 2024 na wakati wowote itazinduliwa ambayo imezingatia maoni ya wadau wa habari.

                          MWISHO

 

 

 

No comments

Powered by Blogger.