KUKOSEKANA MAANA HALISI KWA BAADHI YA VIFUNGU VYA SHERIA YA HABARI KUNAVYOKWAMISHA UHURU WA HABARI ZANZIBAR
NA ASIA MWALIM
NCHI yoyote haiwezi kuwa na maendeleo pasipo na sheria rafiki ya kuwaongoza wananchi katika kufanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuvunja misingi ya kidemokrasia au kubughudhiwa.
Ili kuhakikisha Demokrasia inatekelezwa ipasavyo kupitia uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza ni lazima serikali kuweka umakini mkubwa kwa baadhi ya vifungu vya sheria za habari hapa Zanzibar.
Katika mazingira ya Zanzibar kuna changamoto kubwa zinazohusiana na Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997, hasa kutokana na kukosekana kwa maana halisi katika baadhi ya vifungu.
Waandishi wa habari wanakua na hofu ya kuandika au kuripoti habari zinazowahusu watu wenye matabaka futalani ikiwemo viongozi wa serikali au wanasiasa kwa kuhofia baadhi ya vifungu vya sheria vilivyokosa maana halisi kaika Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997.
SHERIA INASEMAJE?
Baadhi ya vifungu vya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 8 ya mwaka 1997, ikiwemo kifungu cha 48 (1) kinachoeleza kuwa mtu yeyote ambaye;
(a) kafanya au anajaribu
kufanya maandalizi yoyote ya kufanya au kula njama na mtu yeyote kufanya
kitendo chochote kwa nia ya uchochezi.
(b) ametamka maneno yeyote
kwa nia ya uchochezi.
(c) kuchapa, kuchapisha
kuuza matoleo ya kuuza, kusambaza au kutoa uchapishaji wowote wa uchochezi.
(d) anaingiza nchini machapisho yoyote ya uchochezi isipokua kama hana sababu ya kuamini kwamba ni uchochezi, atakua ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni moja au kifungo cha miaka mitano jela au adhabu zote kwa pamoja na uchapishaji huo utataifishwa na serikali.
Pia kifungu namba 57(1) cha Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997, kinaeleza iwapo uchapishaji wa mambo ya kashfa ni wa haki, ikiwa suala hilo limechapichwa na Rais, Serikali, Baraza Wawakilishi au Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa waraka wowote rasmi au shauri.
Mtu yeyote atakae patikana na hatia kwa kosa la kashfa ya maandishi au ya maneno chini ya sheria hii atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi laki tatu au kifungo cha miezi sita au adhabu zote mbili.
Tumeshuhudia kuwa katika sheria hiyo makosa ya kashfa yametajwa katika vifungu tisa 9 vyenye vipengele vingi vya kuithibitisha hiyo kashfa ambavyo vinajichanganya.
Pia haitambuliki ni nani anaamua kuwa jambo hilo ni kwa maslahi ya umma?
Kupitia baadhi ya vifungu vya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997, ni wazi kuwa inazoretesha utendaji wa kazi hasa kwa waandishi wa habari hivyo kuwakosesha wananchi haki yao ya kupata habari n ahata kutoa maoni yao kupitia vyombo vya habari kwa hofu ya kutenda makosa.
WANASHERIA
Mkurugenzi Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud, anasema kwa kua sheria ni muongozo unaotumika kwa kila mmoja hivyo ilipaswa ifafanue na kubainisha maana halisi ya maneno yaliyomo ndani ya sheria na kuanisha mazingira gani yakitokea mtu anaweza kufanya maamuzi na isiwe tu sheria imeweka maamuzi hayo moja kwa moja kwa dhana ya kulinda maslahi ya umma.
Jamila anasema jambo hilo linaloleta ukakasi kwa wadau na waandishi wa habari na kujiuliza maswali yanayokosa majibu neno nia ya uchochezi inapimwa kwa njia gani, namna gani na kwa watu wa kundi gani?
Aidha suala la tuhuma za uchochezi linazalisha maslahi ya kisiasa, vifungu hivi vinapunguza uhuru wa vyombo vya habari na kuhatarisha uhuru wa kujieleza kwa wananchi.
Hadia Ali Makame, Msaidizi wa Sheria wilaya ya Kaskazini Unguja, anasema sheria hiyo inakwaza jamii kubwa sio waandishi wa habari pekee kwani wanakosa kutoa maoni na kupaza sauti zao.
Aidha anasema umefika wakati serikali kulipa kipaumbele suala hilo ambalo lina maslahi mapana ya taifa na maendeleo ya wananchi kwa ujumla ambao wananafasi kubwa ya kuchangia maendeleo kwa kutoa maoni yao kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu katika mustakabali wa maisha yao na nchi kiujumla.
WAANDISHI WA HABARI
Jabir Idrissa mwandishi wa habari maarufu Zanzibar, anasema sheria hiyo inampa nguvu waziri mwenye dhamana kufungia au kuzuia uchapishwaji wa gazeti chini ya kisingizio cha “maslahi ya amani na utulivu”.
Kwa vile tu hakuna maana halisi ya maneno hayo, hivyo huleta ukakasi kwa jamii kwa mfano Kiongozi mwenye dhamana anapata mwanya kukitumia vibaya kifungu hicho cha sheria.
Anabainisha kuwa sheria hiyo inampa nguvu Rais wa nchi kuzuia uingizwaji wa chapisho lolote linaloonekana kuhatarisha “maslahi ya amani na utulivu” pia kupitia sheria hiyo anaweza kuwafungulia mashitaka watu watakaokutwa na chapisho lilozuiwa kuingia nchini.
“Inashangaza kuwa sisi Zanzibar bado tunaongozwa na sheria kandamizi kiasi hichi, hivi kweli mtu akutwe tu na chapisho lilokatazwa kuingia nchini, afunguliwe mashitaka? Ikiwa kuna tangazo mule analisoma si haki hili” anasema.
Huwaida Nassor mwandishi wa habari kutoka Assalam Radio Zanzibar, anasema waandishi wa habari wanategemewa na kuamiwa na jamii kubwa katika kuibua changamoto zao na kuwaonesha njia.
“Ikiwa waandishi wanadhibitiwa namna hiyo hakuna atakaejaribu kupaza sauti ya mnyonge aliyedhulumiwa na kudai haki yake nah apo bila shaka uhuru wa waandishi na hata wananchi ndiyo haupo, tusifichane,” anasema.
Rukia Mputila mwaandishi wa habari kutoka Shirika la Utangazi Tanzania (TBC) anasema wapo vijana wengi waliosomea taaluma ya habari wakiwa mitaani bila ya ajira ambao wanasubiri sheria mpya ya habari ipitishwe ili kujiajiri kupitia mitandao ya kijamii lakini hofu zimewatala kwa sheria Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 8 ya mwaka 199 jinsi ilivyokandamizi.
WADAU WA HABARI
Muandishi wa Habari Mkongwe Zanzibar, Salim Said anasema anaamini kwamba nia ya kupatikana sheria mpya ya habari haipo kwani serikali ya Zanzibar haina nia ya kulifanyia kazi suala la marekebisho ya sheria za habari badala yake imekua ikifanya udanganyifu kwa kutoa ahadi za uongo.
“Tokea suala hili kuzungumzwa na sisi wadau wa habari kupewa kauli tofauti, mfano tupo njiani, tupo mbioni, mbio hizo hazina mwanzo wala mwisho, hata Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi alipoingia madarakani tulikutana nae alituahidi hivyo na mpaka sasa hakuna kilichofanyika”
Salim anasema Wazairi wa wizara hiyo Tabia Maulid Mwita imekua tabia yake kila anapoulizwa kwa takriban mara 3 ameahidi mswaada huo utasomwa katika kikao kijacho hakuna ahadi aliyoitimiza.
“Katika miaka 20 hii tunayopigania uhuru wa habari na tunaoshuhudia Baraza la wawakilishi Zanzibaar limepokea na kuzirekebisha au kuzitunga sheria zaidi ya 100 lakini wanaifumbia macho sheria ya habari.
Anawasihi viongozi kuiga mifano ya nchi jirani na wanapswa kujiulize kwanini nchi kama Uganda, Ruwanda, Burundi na Tanzania Bara wamefanya marekebisho ya sheria na kuweka mazingira mazuri kwa waandishi wa habari kupaza suti zao na kutoa maoni ya wananchi.
“Nahisi Zanzibar haiongozwi na sheria badala yake siasa ndio inaongoza nchi kuwa na sheria kandamizi ya habari kama ilivyo sasa huwezi kusema kama una demokrasia nchini mwako” anasema.
Anaelezea wasisi wake kwa waandishi wa habari kushindwa kufanya kazi zao vizuri na kufichua maovu yaliyojificha kwa mfano hivi sasa wananchi wanalalamika kuhusiana na miradi ya seriakli kutolewa bila ya kuwepo zabuni, je nani atakaefatilia suala hilo ikiwa sheria ni kandamizi?
Kueleka uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 2025, waandishi wanabanwa kufanya kazi zao kwa uwazi na wanapojaribu kuhoji kuhusiana na kitu fulani wanaitwa wachochezi, je hatuna haki ya kufanya kazi kama watu wengine?
Anashauri serikali na viongozi waliopewa
dhamana kuwa na kauli za ukweli kwani binaadamu hupimwa kwa vitu vikuu viwili
ikiwemo kauli na vitendo badala yake itakua ni unafiki, na hivyo kuacha kuogopa
vyombo vya habrai kwani ni wadau wa maendeleo.
Aliyekuwa Afisa Mdhamini wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema sheria hiyo imeshapitwa na wakati na haifai kutumika kwani baadhi ya maneno yanayotumika yanaleta ukakasi kwa wadau na waandishi wa habari.
“Ikiwa utaisoma sheria hii ni lazima utajiuliza maswali yanayokosa majibu kwa mfano neno nia ya uchochezi inapimwa kwa njia gani, namna gani na kipimo gani kinatumika ili kujulikana na kila mmoja kutambua kuwa ni kosa?” alisema.
Mchambuzi wa sheria za Habari Zanzibar Hawra Shamte anasema, kwenye nchi zinazojali kwa vitendo utawala bora na utawala wa sheria, suala la kupata na kutoa habari haliwekewi masharti mazito.
“Zanzibar inadai kuwa na
utawala bora na utawala wa sheria lakini ukiangalia kwa undani utagundua mambo
mazito kwenye kupashana habari kuanzia, kukusanya, kusambaza na hata mtu kutoa
maoni yake,” anasema.
Hawra anafanua kuwa sheria hiyo katika suala la kashafa ni ya kibaguzi kwani wengine inawabana na wengine inawaacha huru kwaniinaeleza kuwa;
“Ikiwa kashfa hiyo itafanywa na viongozi wa serikali ikiwa Rais au yeyote mwenye wadhifa, serikali, Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi ni kashfa ya halali na haki.
“Hivyo ndiyo kusema kuwa kuna watu na mamlaka ambazo zikifanya vitendovya kashfa kama kuandika au kutoa matamsha ya kashfa dhidi ya mtu au mamlaka nyingine ni haki kufanya hivyo,” anasema na kuongeza; “Hiyo siyo sawakabisa.”.
NINI KIFANYIKE
Hawra anasema ni jambo jema na la busara kupata sheria mpya itakayotoa maana halisi ya maneno mbalimbali ikiwemo maslahi ya umma, maslahi ya taifa na amani na utulivu.
Mkurugenzi wa Chama Cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania - Zanzibar (TAMWA Znz) Dk. Mzuri Issa
Ali, anasema katika sheria mpya ya habari ni vyema vifungu vinavyompa uwezo
mkubwa waziri visiwamo.
Anasema kuendelea kutumika
sheria hiyo ni sawa na kukiuka Katiba ya Zanzibar ambayo imetoa nafasi kwa kila
mwananchi kutoa maoni yake na hiyo ndio maana hasa ya demokrasia inavyotakiwa.
WIZARA YA HABARI ZANZIBAR
Waziri wa Habari na
Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, katika vikao vyake vya hivi karibuni
anasema mchakato wa upatikanaji wa sheria bora na rafiki Zanzibar, umewiva
maana mswada wa sheria ambayo imejali maoni mbali mbali ya wadau, itafikishwa
Baraza la Wawakilishi wakati wowote.
Akitoa salamu za Katibu
Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mkurgenzi wa Idara
ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhan Abdallah, katika maadhimisho ya siku
ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyoandaliwa na Kamati ya Wataamalu wa
Masuala ya Sheria Zanzibra ZAMECO Mei 17, 2025 amesema suala la marekebisho ya sheria za habari
Zanzibar litafika mwishoni muda sio mrefu hasa kutokana na msukumo wanaoufanya
waandishi wa habari.
Anasema ni vyema waandishi na wadau wa
habari kuondoa hofu kwani serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara
husika inalisimamia vizuri suala hilo liweze kukamilika.
Aidha aliwapongeza waaandishi wa habari kwa
kupeleka msuko mkubwa katika suala ziama la marekebisho ya sheria za habari
aambalo limekua la muda mrefu.
“Nakumbuka suala hili limeanza muda mrefu
tangu nikiwa mwanafunzi wa tasnai hii na nimeshiriki katika mafunzo mbali mbali
yalioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutoka Zanzibar na Tanzania
bara ” alisema.
Anafahamisha kuwa mtazamo wa wizara hiyo ni
kuwawekea mazingira mazuri wanahabari na vyombo vya habari katika sera na
sheria ya habari.
MWISHO

Post a Comment