WAANDISHI NA WADAU WA HABARI ZANZIBAR WALILIA SHERIA MPYA NA RAFIKI YA HABARI
NA MARYAM NASSOR
ZANZIBAR
Waandishi wa Habari Zanzibar wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Sheria mpya na rafiki ya habari ambayo itawawezesha waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kuwa huru na kujiamini kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii.
Wameeleza
hayo katika mkutano wa kupeana mrejesho baina ya waandishi na Wataalamu wa
Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) juu ya kuendeleza utetezi na uchechemuzi
kwenye masuala ya habari Zanzibar.
Wanasema
iwapo Sheria zilizopo zitafanyiwa marekebisho ya haraka kabla ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2025, zitaweza kuondoa hofu ya kukusanya na kutoa taarifa mbali mbali na
kuiwezesha jamii kupata habari kwa wakati.
"Kwa
kipindi kirefu tumeendelea kufanya uchechemuzi lakini marekebisho ya sheria
mbili kuu yaani Sheria ya Wakala wa Habari Magazeti na Vitabu (1988) na Sheria
ya Tume ya Utangazaji Zanzibar (1997) ambazo waathirika wakubwa ni Waandishi, vyombo
vya habari na jamii iliyotuzunguka”, wanaeleza waandishi hao.
Wameongeza
kuwa, Licha ya juhudi za wadau mbali mbali wa sekta ya habari ikiwemo ZAMECO na
waandishi wahabari kuendelea kufanya uchechemuzi kwa kutayarisha Makala na
vipindi mbalimbali vinavyoonesha mapungufu yaliyomo katika sheria za habari
lakini bado matumaini ya kupatikana Sheria mpya yanaendelea kusuasua kila uchao.
Kwa
upande wao baadhi ya wajumbe wa ZAMECO walioshiriki katika kikao hicho wamewahimiza
waandishi kuendelea kupaza sauti zao kwa kuandika kazi ambazo zitaleta athari
kwa jamii sambamba na kupatikana kwa sheria mpya ya habari isiyokua na vifungu
vinavyokandamiza uhuru wa habari.
Mkutano
huo uliowakutanisha waandishi wa habari na wajumbe wa ZAMECO umefanyika katika
ofisi za TAMWA-ZNZ Unguja na Pemba kwa lengo la kukuza na kuendeleza utetezi
kwenye masuala ya kuhamasisha upatikanaji wa Sheria Mpya ya Habari Zanzibar.

Post a Comment