ASASI ZA KIRAIA ZAHIMIZA WANAWAKE KUCHUKUA FOMU ZA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA VYAMA VYAO

NA MARIAM NASSOR

ZANZIBAR

Asasi Za kiraia zinazoshughulikia masuala ya wanawake na uongozi zinawahamasisha wanawake wote wenye sifa kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Ushiriki wa wanawake katika uongozi ni jambo la msingi katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuleta maamuzi jumuishi yanayoakisi mahitaji ya jamii nzima. Katika kipindi hiki ambacho vyama vya siasa vimeanza kutoa fomu za kugombea nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na hata urais, na vyengine kutangaza tarehe za kuchukuwa fomu hizo, Asasi hizo zinatoa wito kwa wanawake kuchangamkia fursa

hii ili kuongeza ushiriki mkubwa wa wanawake katika nafasi za uongozi. Asasi hizi kwa pamoja zimefanikiwa kutoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake zaidi ya 200 kwa Unguja na Pemba wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kupitia Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (SWIL).

Takwimu za chaguzi zilizopita zinaonesha kuwa bado kuna uwakilishi mdogo wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, jambo linaloathiri uwiano wa kijinsia katika ngazi za maamuzi. Ripoti ya uchaguzi wa mwaka 2020 iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar inaeleza kuwa kati ya wagombea 601 waliochukua fomu mwaka 2020 wanawake walikua ni 135 tu sawa na asilimia 22.4 ya wagombea wote. Hii inaonesha kwamba bado wanawake hawajaitumia vizuri haki yao ya kikatiba kushiriki kikamilifu katika michakato ya nchi ikiwemo kuomba kuchaguliwa katika nafasi mbali mbali. Asasi hizi pia zinatoa wito kwa wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kujiepusha na vitendo vya rushwa, iwe kutoa au kupokea na pia zinawahimiza wanawake hao kuripoti vitendo vyovyote vya rushwa wanavyokumbana navyo ili kurahisisha mchakato wa ushiriki wao katika uongozi kufanyika kwa haki, uwazi na kwa ufanisi.

Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Na. 5 ya mwaka 2023 ya Zanzibar kifungu cha 50 (1 na 2) kinaeleza kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kutoa au kupokea rushwa kwa lengo la kumshawishi mtu kupiga kura ama kuacha kupiga kura na adhabu yake ni faini isiyopungua milioni tano au kifungo kisichopungua miaka mitatu au adhabu zote kwa pamoja.

Aidha kupitia kifungu cha 98 na 99 cha sheria hio kinatoa ulinzi maalum kwa mashahidi wanaotoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa, ili kuhakikisha usalama wao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

Taasisi zinaendelea kusisitiza umuhimu wa uadilifu na uwajibikaji katika mchakato mzima wa uchaguzi, kwa kuwa hayo ni misingi muhimu ya kukuza demokrasia na usawa wa kijinsia katika uongozi.

Asasi zinazohusika ni pamoja na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa mashirikiano na Serikali yaNorway.

Imetolewa na:

TAMWA ZNZ, JUWAUZA, ZAFELA & PEGAO.

No comments

Powered by Blogger.