UMUHIMU WA SHERIA NZURI ZA HABARI ZANZIBAR
Na -Maryam Nassor
Katika jamii
yoyote yenye demokrasia, sheria nzuri ya habari ni msingi wa maendeleo, uwazi,
na utawala bora. Sheria nzuri ya Habari huweka misingi inayowezesha uhuru wa
vyombo vya Habari.
Inalinda haki
za waandishi wa habari na kuhakikisha kuwa raia wanapata habari sahihi na kwa
wakati unaofaa. Katika makala haya tutajadili umuhimu wa kuwa na sheria nzuri
ya habari na faida zake kwa jamii.
Sheria nzuri ya
habari inahakikisha kuwa waandishi wa habari na vyombo vya habari vinaweza
kufanya kazi zao bila hofu ya kuingiliwa au kubanwa na mamlaka.
Uhuru huu ni
muhimu katika kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinaweza kutoa taarifa za
ukweli na kusaidia wananchi kuwa na uelewa wa kina kuhusu masuala mbalimbali ya
kijamii, kisiasa, na kiuchumi.
Akizungumza na mwandishi wa Makala haya,
Mjumbe wa Kamati ya Wataalam wa Masuala ya Habari Zanzibar ( ZAMECO) Jabir Idrissa anasema Sheria nzuri ya Habari inachangia
uwazi katika utawala na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi.
Anasema kuwa, kupitia vyombo
huru vya habari, wananchi hupata fursa ya
kufuatilia shughuli za serikali, kubaini matumizi ya rasilimali za umma, na
kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao. Hii inasaidia kupunguza ufisadi na
kuimarisha utawala bora.
Aidha amesema
kuwa, Sheria nzuri za Habari zitasaidia kulinda haki za wananchi za kupata habari
sahihi kwani jamii ina haki ya kupata habari sahihi na kwa wakati.
“Sheria bora ya
Habari inayolinda haki kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya habari vinawajibika na
kutoa taarifa zilizo sahihi na zisizo na upendeleo. Hii inasaidia kuepuka
upotoshaji wa habari na kusambaa kwa taarifa za uongo,” anasema Jabir.
Naye, mwandishi
wa Habari wa kujitegemea Thuwaiba Habibu amesema Habari ni chombo cha maendeleo, kwani
husaidia watu kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao. Sheria nzuri ya habari
inahakikisha kuwa vyombo vya habari vinatoa habari za kielimu, afya, uchumi, na
maendeleo ya kijamii, ambazo zinaweza kusaidia wananchi kuboresha maisha yao.
Amesema kuwa, Sheria
nzuri ya habari inapaswa kuwalinda waandishi wa habari dhidi ya unyanyasaji,
vitisho au mashambulizi kutokana na kazi zao. Katika mazingira mengi, waandishi
wa habari hukabiliwa na changamoto kama vile kushambuliwa, kutishiwa maisha, au
hata kufungwa kwa sababu ya taarifa wanazotoa.
Aidha amesema
kuwa, Sheria inapaswa kuwalinda na kuhakikisha kuwa wanaweza kufanya kazi zao kwa
uhuru na usalama bila ya vitisho na shinikizo kutoka vyombo vya dola.
Shadida Omar ni Afisa Programu kutoka Ofisi ya Watetezi za
Haki za Binadamu Zanzibar ( THRDC) anasema kuwa i Ingawa
uhuru wa habari ni muhimu, pia ni muhimu kuwa na sheria inayodhibiti matumizi
mabaya ya habari, kama vile uenezaji wa taarifa potofu (fake news), uchochezi,
au habari zinazokiuka maadili ya jamii.
Anasema
kuwa, Sheria nzuri za Habari
inapaswa kuweka miongozo thabiti kuhusu matumizi sahihi ya habari bila kuathiri
uhuru wa Vyombo vya
Habari nchini.
Aidha anasema
kuwa, Sheria nzuri ya Habari ni
msingi wa jamii iliyo huru, yenye maendeleo, na inayozingatia haki, inapohakikisha
uhuru wa vyombo vya habari, inasaidia uwajibikaji, uwazi, na maendeleo ya kijamii.
Hata hivyo’’ sheria hizi zinapaswa kuwekwa kwa
uwiano mzuri ili zisitumike kama chombo cha kuwakandamiza waandishi wa habari
au kuzima uhuru wa habari,”
anasema Shadida.
Naye, Afisa Programu ya Maswala ya Sheria za Habari
kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar - TAMWA ZNZ ,
Zaina Mzee anasema
serikali na wadau wengine wanapaswa
kushirikiana kuhakikisha kuwa kuna mfumo wa kisheria unaounga mkono uhuru wa habari
na kupatikana sheria rafiki ya habari
itakayotoa uhuru
kwa waandishi.
Anasema kuwa, Sheria nzuri ya Habari itaharakisha Maendeleo kwani waandishi wa Habari watapata fursa ya kufanya kazi zao bila ya upendeleo wala hofu kutoka kwa wenye mamlaka.
Akijibu, maswali ya waandishi
wa habari, katika kikao cha
Tathimini ya Mafanikio ya
miaka minne ya Dokta Hussein Mwinyi, Waziri wa Habari Utamaduni, Vijana na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amesema muswada
wa Sheria ya Habari upo,
katika Kamati ya Ufundi ya Taifa (N TC)
ambako unashughulikiwa.
Katika hatua nyengine, Waziri huyo amesema kuwa anatamani mswada huo
ufikishwe katika Baraza la wawakilishi hivi karibuni.
"Sheria ya Habari itasomwa wiki ijayo na Mswada huo kwa mara ya kwanza unatarajiwa kupelekwa Baraza la Wawakilishi katika kikao kinachoanza tarehe 7 na kwa vile Rais anapenda mambo yaende haraka tunatarajiwa sheria hiyo itapitishwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tutakuwa na sheria mpya ya Habari" Waziri Tabia katika uzinduzi wa Mfumo mpya wa matangazo ya ZBC RADIO, SPICE FM NA SPICE TV- huko karume Zanzibar mwezi huu wa nne mwaka 2025.
Ni zaidi ya miongo miwili sasa waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu Zanzibar wameendelea kudai Sheria rafiki ya Habari bila ya mafanikio yoyote.
MWISHO

Post a Comment