WANAWAKE WAMETAKIWA KUHAMASISHANA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI.

NA MARYAM NASSOR

WAANDISHI wa Habari  na jamii kwa ujumla  wametakiwa  kuwa na mikakati  maalumu ya kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kwani bado wako kidogo katika nafasi hizo.

Ameyasema hayo,  Afisa Programu wa michezo kwa Maendeleo kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar- TAMWA ZNZ Khairat Haji,  alipokuwa akizungumza na wandishi wa Habari na wadau mbali mbali wa michezo katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani huko katika ukumbi wa TAMWA Tunguu Unguja.

 Amesema kuwa, takwimu zinaonesha kuwa  bado kuna upungufu wa  viongozi wanawake katika nafasi mbali mbali za uongozi nchini,  kwani  wanawake mpaka sasa ni asilimia 30  tu ambao wako katika nafasi hizo, ukilinganisha na wanaume ambao wako asilimia 70.

“ Tuwaunge mkono wanawake ambao wanatia nia ya kugombea katika nafasi mbali mbali za uongozi na tusiwavunje moyo, kwani mwanamke akiwa kiongozi basi analeta maendeleo kwa haraka”  anasema Khairat.

Nae, mjumbe wa bodi kutoka TAMWA ZNZ  Bi Asha Abdi amesema historia inaonesha   wanawake waliachwa nyuma  sana katika shughuli mbali mbali za maendeleo, ikiwemo nafasi za uongozi.

Amesema kuwa,  nafasi ya mwanamke katika uongozi  iko nyuma na kwa hapa Zanzibar hali ilikuwa mbaya zaidi.

“ Ni vyema tuwe mabalozi wazuri huko uraiani tuwaunge mkono wanawake wenzetu na ikiwezekana tuwapigie kura ili wawe viongozi” anasema Bi Asha.

Aidha amewataka wandishi wa Habari kutumia kalamu zao, kuwaonesha wanawake ambao ni viongozi na wanafanya vizuri  katika kuihudumia jamii na kuleta maendeleo.

Nae, Afisa Tathimini na Ufuatiliaji kutoka TAMWA ZNZ Mohamed Khatib Mohamed amesema tafiti iliyofanya na chama hicho inaonesha wanawake ni wachache wanaoshiriki katika michezo mbali mbali nchini.

 Amesema kuwa, utafiti huo umewashirikisha  watu 102 wakiwemo makocha, wachezaji na viongozi wa vyama vya michezo, na wamebaini kuwa Zanzibar ina sera nzuri ya michezo ya  mwaka 2018 lakini shida ni utekelezaji wake.

“Sera ya michezo ya mwaka 2018 ni nzuri sana, lakini utekelezaji wake ndio mbaya kwani haina mikakati ya kuwainua Watoto wa kike washiriki michezo” anasema Mohamed.

Nae, Kocha  wa mpira wa miguu katika timu za  wanawake Khatma Mwalim Khamis , anasema udhalilishaji ni mkubwa katika timu za mpira wa miguu kwa wachezaji wanawake na wanaume.

Aidha amesema kuwa, changamoto nyengine inayowakumba wachezaji wa kike ni mila na desturi , ambapo jamii inaona ni kinyume na desturi zao wanawake kushiriki katika michezo.

Nae, mwakilishi kutoka  Serikali ya Ujerumani nchini Tanzania( G IZ) Hija Mohamed Ramadhan  amesema wametengeneza mpango mkakati wa kuwalinda wachezaji  kwa kushirikiana na wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia  Wazee na  Watoto  dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wakiwa kwenye michezo.

Aidha amesema kuwa, kutokana na hatua hizo wanategemea siku za mbeleni ushiriki wa wanawake katika nafasi mbali mbali katika michezo utaongezeka.

Madhimisho hayo ya siku ya wanawake duniani yameadhimisha na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar, na kuwashirikisha wadau mbali mbali wa michezo, na kauli mbiu  ya mwaka huu ilikuwa ni ‘‘Ushiriki wa Mwanamke na Msichana  ni Kichocheo cha Maendeleo’’.

 

                        mwisho

No comments

Powered by Blogger.