UWEZO MKUBWA WA ASKARI POLISI WA KUKAMATA NA KUPEKUWA CHOMBO CHA HABARI NI KILIO KWA WANAHABARI.
NA MARYAM NASSOR
ZANZIBAR ni nchi yenye sheria mbaya ambazo zinaminya
uhuru wa habari kiasi ambacho waandishi
wa habari wanashindwa kuandika habari za uchunguzi na kuikosoa Serikali.
Taaluma ya uandishi wa habari ni kazi kama kazi
nyengine ambazo zipo rasmi na zinatambuliwa kisheria duniani kote kutokana na
umuhimu wake katika kuhabarisha jamii na taifa kwa ujumla.
Inaaminika kuwa tasnia ya habari, kutokana na
umuhimu wake inaweza kuwa ni muhimili wa nne wa nchi ukitoa Bunge, Serikali na Mahakama.
Uwepo
wa sheria ambayo inampa mamlaka makubwa Askari Polisi kukamata na kupekua gazeti
lolote popote linapopatikana kwa kushuku kuwa limechapishwa kinyume na sheria
kitendo hicho kinanyima uhuru wa habari nchini.
Kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Usajili wa Wakala wa
Habari, Magazeti na Vitabu Na.5 ya 1988 na marekebisho yake Na.8 ya 1997 kinasema, “Afisa polisi
yeyote anaweza kukamata gazeti lolote, popote linapopatikana, ambalo
limechapishwa au ambalo anashuku kuwa limechapishwa, kinyume na Sheria hii.”
Hiki ni kifungu chenye matatizo sana na ni miongoni mwa vifungu vinavyonyang’anya
haki ya kutoa habari iliyoainishwa na Katiba.
Akizungumza na mwandishi wa
Makala hii, Mjumbe wa Kamati ya masuala ya Habari Zanzibar( ZAMECO ) Jabir
Idrisa anasema sheria hii ni kikwazo kikubwa kwa wandishi wa Habari Zanzibar
kwani inanyima uhuru wa Habari na
inakwenda kinyume na katiba ya nchi.
Amesema
kuwa, uwezo aliyopewa Askari Polisi wa kupekuwa na kukamata gazeti popote
litakapopatikana unaathiri uhuru wa habari nchini kwani waandishi wengi wa habari wana hofu na wasiwasi
na vyombo vyao kuandika habari zinazokosoa Serikali na viongozi wake.
Amesema
kuwa, “utendaji kazi wa Askari Polisi unajulikana ulivyo si wa kupewa mamlaka
hayo, kwani Polisi wengi hawana uelewa wa vyombo vya habari anaweza kuyatumia
vibaya mamlaka hayo,” anasema.
Aidha amesema
kuwa, Polisi wanaweza kuyatumia mamlaka hayo vibaya au kwa upendeleo kulenga vyombo vya upinzani [Ma1] bila
sababu za msingi na kupelekea kuviuwa
vyombo hivyo.
“Sisi tunataka sheria hii irekebishwe au ifutwe
kabisa kwani ni ya muda mrefu na
imepitwa na wakati” anasema Jabiri.
Naye,
mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka Zanzibar Ali Amour
amesema , tasniaasisi ya Hhabari
ni fani kama fani nyengine haiwezi kuingiliwa na
askari polisi kwa kushuku tu bila
ya uhakika.
Amesema kuwa ni vyema sheria hiyo ikabadilishwa ili
kutoa uhuru wa habari, mamlaka makubwa ya Askari Polisi aliyopewa yanaweza
kutumika vibaya na kuathiri uhuru wa habari nchini.
Aidha
mwanasheria huyo, alishauri kuwa kabla Askari Polisi hajapekuwa na kukamata
chombo cha habari ni vyema angeshirikiana na Bodi ya Habari kuhakikisha kuwa
haminyi uhuru wa habari nchini.
Akizungumzia kuhusu sheria hiyo, mwandishi wa Habari
Mkongwe Kisiwani Unguja Bw. Salim Said Salim anasema sheria nyingi zimekuwa zikirekebishwa
na mchakato wake hauchukui hata miezi sita, kama Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya
Huduma na posho kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
“Sheria hii ya Habari iko zaidi ya miongo miwili
sasa tunafanya uchechemuzi bila ya mafanikio yoyote, je, ugumu wa kurekebishwa
uko wapi?” amehoji Bw. Salim.
Amesema kuwa uwezo
aliopewa Askari Polisi wa kupekua na kukamata gazeti popote litakapo patikana na ambalo limechapishwa au anashuku kuwa limechapishwa kinyume na sheria hii , unaathiri uhuru wa habari nchini.
Aidha
ameiomba Serikali kusikiliza kilio cha muda mrefu cha waandishi wa habari na
wadau cha kutaka kuwapo kwa sheria rafiki za habari ambazo zitaendana na wakati
wa sasa.
Shadida Omar ni Afisa Programu kutoka Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
Zanzibar - THRDC anasema kifungu cha 27 (1) cha sheria ya Sheria ya Usajili wa Wakala wa
Habari, Magazeti na Vitabu kimempa mamlaka makubwa
Askari Polisi kupekua au kukamata gazeti au kufungia chombo cha habari, hii
inazuia ufanisi wa utafutaji wa taarifa na utoaji wa taarifa.
Amesema kuwa, sheria
hii ni mwiba kwa vyombo vya habari kwani inaweza kupelekea Askari kutumia vibaya nafasi
hiyo kwa maslahi ya kisiasa kuua vyombo vya habari vinavyomilikiwa na vyama vya
upinzani au hata vyombo vya habari binafsi.
Naye Afisa
Programu wa mradi wa sheria kutoka TAMWA ZNZ, Zaina Mzee amesema mradi
huu ni muendelezo kuwanoa waandishi wa habari ili wawe mahiri zaidi katika
kuchambua masuala ya sheria za habari na kufanya uchechemuzi ili sheria
kandamizi zifutwe.
Amesema kuwa, ni vyema waandishi wasichoke kufanya
uchechemuzi ili hatimayezipatikane sheria rafiki za habari kwani itasaidia
kuondokana na sheria mbaya na ambazo zimepitwa na wakati.
Dkt Mzuri Issa ni Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ) amesema ni kweli sheria hizi zimepitwa
na wakati na zinaenda kinyume na Katiba ya nchi.
“Huu sio wakati tena wa kuwa na sheria kama hizi za
habari, hivi sasa dunia imekua kijiji kutokana na maendeleo ya Sayansi na
Teknolojia na tunaona umuhimu wa kuwa na uhuru wa habari na jinsi
unavyoshajiishwa duniani kote, iweje mpaka leo Zanzibar tuwe na sheria
kandamizi za habari?” Amehoji Dkt Mzuri.
Aidha ameongeza kuwa, kwanini Zanzibar haifuati nchi
kama Afrika ya Kusini ambayo mara tu baada ya kujikomboa kutoka katika utawala
wa ubaguzi wa rangi, walivipa uhuru vyombo vya habari kuandika kwa uwazi na
kuikosoa Serikali ili kuharakisha maendeleo.
Mwisho
[Ma1]vyombo vya upinzani ndiyo vipi?

Post a Comment