UKATILI WA KIMTANDAO UNAVYORUDISHA NYUMA VIONGOZI WANAWAKE
NA MARYAM NASSOR
Azma ya kufikia usawa wa kijinsia kwa karne ya 21
imekuwa ni ajenda inayotiliwa mkazo kimataifa na kitaifa
kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya
kiuchumi na kisiasa.
Jitihada mbali mbali zinachukuliwa siku hadi siku za kuona
kuleta usawa wa kijinsia wa 50/50 katika nafasi za uongozi.
Hii ikijumuisha idadi ya wanawake 974, 281
ambayo ni sawa na asilimia 51 ya wanaume ambao ni asilimia 49. Hii
ni kwa mujibu wa Sensa ya Watu na
Makaazi ya mwaka 2022 kwa Zanzibar.
Licha ya wingi wao, wamekuwa wakikabiliwa na aina mbalimbali
ya vikwazo.
Wanaharakati na watetezi wa haki za wanawake wanakiri kwamba
mtandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuwadhalilisha wanawake.
Asma Mohamed ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wilaya ya
Kati Unguja, ambae alishawahi kugombea nafasi mbali mbali za uongozi
katika Chama cha Mapinduzi -CCM anakiri uwepo wa ukatili wa kimtandao kwa
viongozi wa kike.
"Hali hii imeshawapata viongozi wengi wanawake wa
kisiasa na kwa kweli haifurahishi," anasema Asma.
Anasema kuwa, wakati akiwaita wandishi wa Habari kuzungumza
nao au kuweka kitu mtandaoni, basi hutokea baadhi ya watu utakuta
wanazodoa kile alichoposti, “ lakini mimi huwa siyachukulii kwa uzito mkubwa
hayo, kwani najua lengo langu nikufika mbali kisiasa," anasema Asma.
Anaongezea kusema kuwa wengine humtukana kupitia mitandao ya
kijamii hasa kutokana na yeye kuwa kiongozi
"Yaani naonekana kama sifai kuweka kitu mtandaoni
si haki yangu kuwa kwenye mitandao," anasema.
Hadi mwaka 2023 , takribani watu milioni 10.5 nchini
Tanzania wanatumia mitandao ya kijamii, katika majukwaa maarufu
kama vile Facebook , Whatssap, Instagram na Tiktok ambayo yanatumia zaidi
kwa mawasiliano, burudani na Biashara ,Huku wanawake takribari
asilimia 40 -45 ambao ni zaidi ya milioni 5 wanatumia
internet nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti Maalumu ya Uchaguzi iliyotolewa na
Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa upande wa Zanzibar ,
inaeleza kuwa, nafasi ya uwakilishi kwenye majimbo 50 ya Uchaguzi ,
wanawake ni asilimia 16 ambao ni wanane, wabunge wanao iwakilisha
Zanzibar wanawake ni wanne, sawa na asilimia 8.
Mawaziri wanawake ni sita sawa na asilimia 33, makatibu
wakuu ni saba sawa asilimia 39, kwa upande wa Wakuu wa Mikoa mwanamke ni
mmoja tu sawa na asilimia 20.
Tunu Juma Kondo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake
Tanzania - UWT wa Chama cha Mapinduzi CCM amesema janga la ukatili wa
mitandao ya kijamii ni changamoto ambayo, baadhi ya viongozi wanawake wa
CCM wamekumbana nayo.
“Hii ni mbaya na inanyong'onyesha sana wanawake, wengine
hurudi nyuma kwa woga kwani husemwa sana na kupewa sifa mbaya
na kuathiri nguvu ya uthubutu wa wanawake,” anasema Tunu.
Ukatili wa kimtandao dhidi ya viongozi wanawake wa
vyama vya siasa ni tatizo linalo athiri siasa na jamii kiujumla,
kwani mara nyingi hulenga kuharibu sifa za viongozi hao, na hata
kashfa zisizo ukweli.
Dk Mzuri Issa ni Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari
Wanawake Tanzania -TAMWA ZNZ amesema ukatili wa kimtandao unalenga
wanawake ni miongoni mwa udhalilishaji ambao umekuwa ukiwazuia baadhi ya
wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.
“Watu ni vyema washindane kwa hoja na sio
kudhalilishana hususani katika majukwaa ya mitandao ya kijamii ,hali hii
inawaumiza sana wanawake” anasema Dk Mzuri huku akiwataka viongozi wanawake
waliopo kwenye siasa wasivunjike moyo na wasiogope kupigwa mitandaoni.
Sheria ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Bunge na Madiwani
inazungumza kuwa, ukatili wa wanawake ni uhalifu hivyo wakati umefika
kuchukuliwa hatua muafaka kwa wale wanaowadhalilisha kwa kuwavunjia heshima na
utu sambamba na vyombo husika kusimamia sheria za makosa ya mtandao hii
itaondoa hofu kwa wanawake wanaofanya ukatili huo.
Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Tanzania kwa upande wa Zanzibar Abdul Razak Said Ali, amesema uwepo wa
Sheria inayosimamia makosa ya mitandao Tanzania ya mwaka 2015
lengo ni kuhakikisha ulinzi wa wanawake na unyanyasaji mitandaoni.
“Masuala yote kuhusiana na makosa ya kimtandao yanadhibitiwa
na sheria hiyo, lengo ni kuwasaidia wanawake wanaopata haki zao pindi
wakikumbana na ukatili kwenye mitandao” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA
Jabir Bakari amesema mamlaka hiyo inaendeleza kutoa elimu ya masuala ya
kidigitali na usalama mitandaoni kwa kuhakikisha mazingira salama na
imara ya matumizi bora ya mitandao.
“Ingawaje mipango ya kuengeza uelewa wa umma ni ajenda
ya kudumu ya TCRA ,kampeni hii inatokana na umuhimu wa kipekee kuwapatia
watanzania mbinu za kujilinda dhidi ya mashambulio ya mitandao ya internet na
simu niwaombe hii pia ni kujilinda dhidi ya uhalifu mtandao”
Ameyasema hayo, Dar es Salamu wakati wa uzinduziwa kampeni
ya ‘Ni Rahisi Sana” inayolenga kuelimisha wananchi kwamba mazingira salama
mitandaoni.
Mwanaharakati kutoka vugu vugu la ukombozi wa mwanamke
Duniani kwa Tanzania, Rahima Mussa Hassan amesema kuwa ukatili wa kimtandao
umekithiri na unaathiri viongozi wanawake kwa kiasi kikubwa na
madhara yake ni makubwa.
“Matusi, dharau na maneno yasiyo na staha ni mengi kwa
wanawake kwenye mitandao ya kijamii hususani kwa wanawake waliopo kwenye siasa”
amesema Rahima huku akisisitiza kuwa, lengo la vugu vugu wa
ukombozi wa mwanamke ni kukata mizizi inayokwamisha mwanamke kutofikia
ndoto zake.
MWISHO

Post a Comment