WANA MAZINGIRA WALIA NA UKATAJI WA MIKOKO.



NA MARYAM NASSOR

Mikoko ni aina ya miti au vichaka vinavyokua katika maji ya chumvi kwenye fukwe za Bahari.

Tafiti zinaonesha miti ya mikoko  ina uwezo mkubwa  wa  kufyoza hewa chafu ya kaboni kwa zaidi ya asilimia 50 , hivyo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mikoko  ni walinzi wakuu wa kinga ya ardhi na jamii za pwani dhidi ya Dhuruba, tsunami , na  kuongezeka kwa viwango vya usawa wa Bahari na mmomonyoko  wa ardhi .

Waasayansi wanaamini miti ya mikoko inaweza kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia  kwa sasa, wakati ambao ulimwengu  ukiwa  ukishuhudia ongezeko la juu la joto katika karne hii.

Katika Shehia ya Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, wananchi wanatumia mikoko kama njia ya asili ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.

  Abdi Juma Mgeni kutoka Shehia ya Unguja Ukuu ni  Katibu wa kikundi cha Mikoko ni Urithi wetu ,  amesema wameamua kupanda mikoko kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji katika Kijiji chao.

 Amesema kuwa, Miti hiyo ndio urithi pekee unaoweza kupambana na  madhara ya mabadiliko ya tabianchi Kijiji  hapo, ambapo maji ya Bahari hupanda hadi katika maakaazi yao.

Aidha amesema kuwa, kikundi chao kimekuwa mstari wa mbele katika kushajihisha jamii kupanda mikoko  kwani wanaamini wakiwa na mifumo ya ikolojia wanaweza kuboresha Maisha ya watu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“ Kikundi chetu kimeanza kupanda mikoko tokea mwaka 2020 baada ya kupata mafunzo ya upandaji kutoka taasisi ya Zaveko” amesema Katibu huyo huku akionesha hamu yake ya kuendelea kutunza Mazingira .

Amesema kuwa, kitendo kilichofanya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukata mikoko yao  zaidi ya miti 200 kimewasikitisha sana bila ya kupewa kivuja jasho.

“ Serikali kujenga Barabara  ni jambo zuri lakini viongozi wangekuja kutuona sisi watu wa mazingira angalau kututia moyo” anasema Katibu wao.

Mmoja wa  wanachama wa kikundi hicho, Wardat Ramadhan Ali amesema vijana wamevunjika moyo ya kuendelea kupanda  na kuhifadhi  mikoko baada ya miti hiyo kukatwa bila ya kushirikishwa ili kupisha ujenzi wa Barabara ya Uzi Ng’ambwa

Amesema kuwa , utafiti wa UNEP unaonesha kwamba mifumo ya ekolojia ya mikoko ina manufaa kwa Uchumi wa kimataifa na wa ndani ya nchi kwa kusaidia sehemu za uvuvi.

  Aidha amesema kuwa,  mikoko inasaidia kulinda viumbe vya baharini ikiwemo Samaki , Kamba na pia inasaidia maji ya Bahari kutokupanda juu   katika makaazi ya watu.

 “ Hapa Unguja Ukuu zamani ilikuwa tukienda baharini asubuhi baada ya  maji kutoka tulikuwa tunaokota samaki wengi lakini kutokana na mabadiliko ya tabia nchi Samaki wamepote kabisa” anasema Wardat.

Amewataka vijana wenzake kutokuvunjika moyo na kuendelea na harakati za upandaji wa mikoko ili kuzuia maji ya chumvi yasipande katika makaazi yao na kutunza mazingira.

“ Tusivunjike moyo kwa hili la kukatwa kwa mikoko ,japo imetuuma kuruhusiwa watu kukata mikoko yetu bila ya sisi wana mazingira kupewa taarifa” anasema Wardat.

Salama Hussein ni  mwanachama wa kikundi cha Mikoko ni Urithi wetu, amesema kuwa ujenzi  wa Daraja la Uzi Ng’ambwa  lenye urefu wa  kilomita mbili na nusu, Limechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa Mazingira kwa kukatwa miti ya mikoko zaidi ya miti 200.

Amesema  kuwa, ujenzi  huo ulianza mwishoni mwa mwaka jana  ambapo Serikali iliamua  kujenga Daraja hilo , baada ya kilio cha muda mrefu cha wakaazi wa vijiji  hivyo.

Amesema kuwa, hapo awali wanakijiji cha Uzi na Ng’ambwa walikuwa  wanapata shida ya kufuata huduma za kijamii na kiuchumi masafa ya mbali.

Nae Sheha wa shehia ya Unguja Ukuu  Khamis Ibrahim Shomari alikiri kukatwa kwa miti ya mikoko kwa kupisha ujenzi wa Barabara ya Uzi Ng’ambwa, na kusema hilo ni jambo la Maendeleo.

Ameitaka jamii kutokuvunjika moyo na kuendelea kupanda mikoko ili kujikinga na madhara ya mabadiliko ya tabianchi  yanayoathiri Kijiji hicho.

“ Ni wasihi wanakijiji cha Unguja Ukuu kutokuvunjika moyo kwa kukatwa kwa mikoko ili kupisha ujenzi wa Barabara  hilo ni jambo la maendeleo” anasema Sheha huyo.

 

Mahafudh Mohamed Haji ni mwenyekiti wa Taasisi ya kutunza Mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, amesema ni vyema wananchi waendelee kutunza Mazingira na kupanda mikoko ili kutunza mazingira yao.

Amesema kuwa, miti ya mikoko ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika vijiji ambavyo maji yanapanda.”Ni ishauri jamii iendelee kupanda mazingira  kwa kupanda mikoko kwani miti hii ni msaada mkubwa wa kukabiliana na athari  za mabadiliko ya tabianchi” anasema Mahfudh.

Akizungumzia kuhusu kukatwa kwa miti ya mikoko  katika eneo hilo, Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Harous Said Suleiman alisema Serikali  imelazimika kukata miti ya mikoko katika eneo hilo ili kupisha ujenzi wa Barabara.

Amesema kuwa, lakini baada ya kukamilika ujenzi watafanya jitihada za kuirejesha  mikoko hiyo” Tutahakikisha  tunashirikiana na wananchi  katika kupanda tena  mikoko ili kufidia miti ya mikoko iliyokatwa na Serikali imeamua kukata mikoko hiyo, siyo kwa nia mbaya bali ni kuwajengea Daraja wananchi na kurahisisha usafiri” amesema Waziri Harusi.

  Kikundi hicho cha mikoko ni urithi wetu kimeazishwa mwaka 2020 na mpaka sasa kimepanda miti  ya mikoko 2,900,700 huku kikiwa na wanachama  150 .

 

 

 

 

 

 

 

No comments

Powered by Blogger.