USARIFU WA BIDHAA ULIVYOWAINUA KIUCHUMI WANAWAKE WA MKOA WA KUSINI
NA MARYAM NASSOR
Katika miaka
ya hivi karibuni, ujuzi wa kusarifu
matunda umekuwa mchango mkubwa katika
kuboresha Maisha ya wanawake katika
jamii za vijiji mkoa wa kusini Unguja.
Usarifu wa
matunda unahusisha mbinu zakulinda, kuhifadhi
na kutengeneza bidhaa mbali mbali
kutokana na matunda, hali inayopelekea
faida nyingi ikiwemo kuongezeka
kwa kipato, ulinzi wa mazingira na
kusaidia kutunza afya.
Tafiti
zinaonesha kuwa, ujuzi wa kusarifu
bidhaa ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya wanawake hasa wa vijijini.
Katika Shehia ya Bungi wanawake wanatumia
vikundi vya kusarifu bidhaa kama njia
ya kujikwamua kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na
kijamii.
Sabra
Abdalla Ali kutoka katika shehia ya
Bungi ni Mwenyekiti wa kikundi cha Nani Kaoni akiwa ni mnufaika wa elimu na ujuzi wa kusarifu mazao kutoka katika
mradi wa ZANZI ADAPT.
Anasema kuwa, hapo zamani msimu wa matunda
kama maembe na mapapai walikuwa hawajui umuhimu wa kuyatunza ili kutumia baada ya msimu kuisha.
Sabra ambae ni mama wa Watoto saba, anasema baada ya kupata elimu ya
kusarifu matunda na tea masala kutoka
katika mradi wa ZANZ ADAPT kipato cha wajasiriamali kimeongezeka na kupata hadi elfu 30 kwa wiki jambo ambalo
hapo awali walikuwa hawana.
Amesema
kuwa, wanawake wengi wanajishughulisha
na usarifu wa matunda, ambapo wameweza kuanzisha biashara ndogo za kutengeneza
na kuuza bidhaa kama juisi, jamu na
pilipili katika maeneo ya vijijini kwa
kutumia matunda kama maembe , mapapai na
tungule ” Hii bishara sii tu inatupa kipato lakini inatusaidia kuwa na uhuru wa kiuchumi” anasema Sabra.
Amesema
kuwa, matunda mengi yalikuwa yanapotea , lakini baada ya kupata elimu ya
kusarifu tungule na matunda mengine yameongeza kipato” kwasasa tungule moja ukiisarifu inaweza kukupa hadi
elfu 3000 badala ya mia tano ikiwa haija sarifiwa” anasema Sabra.
Asma
Sadiki Hussein, mkaazi wa Kijiji cha Bungi na mwanachama katika kikundi cha
kusarifu Matunda anasema, usarifu wa
matunda unachangia katika kuboresha afya za wanawake na familia zao, kwa kutengeneza
bidhaa zenye virutubisho kutoka katika
matunda.
“Jamii
nyingi za vijijini zimeweza kubaini
umuhimu wa kutumia matunda katika milo yao ya kila siku, hivyo kupunguza
magonjwa yanayotokana na lishe duni” amesema Asma.
Amesema
kuwa, wanawake wanaoshiriki katika usanifu wa matunda wanachangia katika
uhifadhi wa mazingira ,kwani wanatumia mbinu za kienyeji za kutengeneza bidhaa
na kukausha matunda , hii njia inasaidia kupunguza matumizi ya plastiki na
kuongeza thamani ya matunda.
Nae, Salama
Hussein mkaazi wa Shehia ya Unguja Ukuu amesema elimu ya kusarifu matunda imewasaidia kupika bidhaa tofauti
tofauti kwa lengo la kuyahifadhi matunda na kufanya biashara.
Amesema
kuwa, ujuzi wa kusarifu matunda waliyoupata umewasaidia kuinua kipato
chao, ambapo hutengeneza biashara ndogo
ndogo na kuuza sokoni.
Zulfa
Mbwana, ni Afisa mradi wa mabadiliko ya tabianchi kutoka Community Forest Pemba ( CFP) anasema wamewapa mafunzo ya
usindikaji wa bidhaa za matunda wanawake kutoka
shehia nne, ambazo ni Unguja Ukuu,
Bungi , Uzi na Ng’ambwa kwa lengo la kuongeza thamani na kuinua kipato cha
wakulima.
Amesema
kuwa, wajasiriamali hao ambao ni wakulima viongozi wamepatiwa elimu ya
uhifadhi wa hesabu na usarifu wa mazao
mbali mbali ya ujasiriamali ili kukuza
kipato chao na kuwa na uhuru wa kiuchumi” Mafunzo haya ya ujasiriamali ni kwa
ajili ya kuongeza thamani za bidhaa za wakulima
na utuzaji wa hesabu”
anasema Zulfa.
Mbarouk Omar
Mussa ni Mkurugenzi katika taasisi ya
Community Forest Pemba anasema mradi wa ZANZ ADAPT umewawezesha wanawake
kuhifadhi na kusarifu bidhaa za matunda
mbali mbali ili kuongeza thamani na kuongeza kipato kwa wajasiriamali wanawake.
Aidha
amesema kuwa, usarifu wa matunda unatoa fursa nyingi kwa wanawake katika jamii
ikiwemo uhifadhi wa mazingira,
kuboresha Maisha ya wanawake na jamii zao kwa ujumla.
Mradi wa
ZANZ ADAPT unatekelezwa na taasisi ya Community Forest Pemba ( CFP) na Chama
cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar -TAMWA ZNZ na kufadhiliwa na Community Forest
Internation ( CFI ).
Post a Comment