RUSHWA YA NGONO ,INAVYOWARUDISHA NYUMA WANAWAKE KUWANIA NAFASI ZA UONGOZI.



‘’Rushwa ya ngono, inavyowarudisha nyuma wanawake kuwania nafasi za uongozi’

Na–MaryamNassor.

Zanzibar:

‘’Niliishiwa nguvu wakati aliponiambia kama naitaka nafasi hiyo basi lazima nikutane nae kimapenzi ndio niipate,” anasema Sharifa.

Licha ya kukataa, lakini kutokana na fedheha aliamua kuliweka jambo hilo moyoni na kulifanya kuwa siri kubwa. Hata mume wake hakumsimulia.

Na huo ndio ulikuwa mwisho wa safari ya ndoto yake katika uongozi mwaka 2015.

Hii ni baada ya kutakiwa kimapenzi na kiongozi wake ndani ya chama, katika kikao cha kujadiliwa ili agombee nafasi ya mjumbe wa kamati kuu ya Chama hicho huko Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Sharifa Juma mwenye umri wa miaka 39 na  mama wa watoto wanne, katika uchaguzi wa kuwania nafasi ya ujumbe wa kamati kuu taifa ndani ya chama chake katika Wilaya ya Chake Chake mwaka 2015, anakumbuka jinsi alivyoitwa na kiongozi wake na kumpa sharti la kumtaka kimapenzi.

“Maneno yake yalinivunja moyo na nikajiona kama nimevuliwa nguo, niliona aibu nikakosa la kusema," anasimulia.

 Sharifa anasema kuwa mwaka 2015 ulikuwa mgumu kwake,baada ya ndoto yake ya kuwa kiongozi kuishia hapo kutokana  na ukatili wa kisaikolojia aliopitia.

”Sikuwa na ujasiri wa kumuhadithia mtu kadhia hiyo iliyomkuta mpaka nikaachia ngazi,nakujitoa katika kinyang'anyiro hicho, na hilo lilipelekea kupata matatizo ya kisaikolojia,”anasema Sharifa.

Tafiti zinaonyesha udhalilishaji wa kijinsia ni suala linalowatafuna wanawake wengi waliopo kwenye vyama vya sisaa kama ilivyokuwa kwa Tatu*40 ambae nae pia alikatisha ndoto yake ya kuwa kiongozi mwaka 2020 huko Wilaya ya Kaskazini‘A’Unguja.

Tatu ni  mama wa watoto wawili mkaazi wa Wilaya ya Kaskazini‘A’Unguja,ni miongoni mwa wanawake waliokatisha ndoto zao za kuwa viongozi, kwa sababu ya ukatili wa kijinsia uliompata wakati anagombea.

Sababu kubwa ya kukatisha ndoto zake,ni baada ya kukumbwa na ukatili wa kijinsia baada ya kutakiwa kimapenzi na msaidizi wake wa kampeni na kuliweka jambo hilo kuwa siri,kwa kuhofia aibu na fedheha kutoka kwa wanajamii.

‘’Sikuwa najua kama ningekutwa na mkasa ule, kwani yule mtu aliyenitaka kimapenzi ni mtu ambae anaaminika na mume wangu,nilihofia hata kumuhadithia kadhia ile,” amesimulia huku akiinamisha sura kwa aibu.

"Nilipata msongo wa mawazo, nilikuwa nakaa ndani nalia pekee yangu, nikihofia siri ile kuja kujulikana, sura yangu nitaiweka wapi,’’ anahojiTatu.

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, mwaka 2022, umeonesha asilimia 55 ya wanawake wenye umri  kati ya miaka 15-49, wameshawahi kufanyiwa aina moja wapo ya ukatili. Ambapo, asilimia 16 wameshawahi kufanyiwa ukatili wa kisaikolojia, asilimia 15 ukatili wa kimwili na asilimia 7 wameshawahi kufanyiwa ukatili wa kingono.

Tatu Ali Abass ni daktari na mwanasaikolojia wa masuala ya Afya ya Akili katika Hospitali ya Wilaya Vitongoji Mkoa wa kusini Pemba, amesema madhara makubwa huwapata watu wanaopata ukatili wa kisaikolojia, ikiwemo msongo wa mawazo na endapo hawatatibiwa mapema, wanaweza kuugua afya ya akili na ugongwa wa sonona.

“Wathirika wa vitendo vya ukatili wa kisaikolojia, wamekuwa wagumu kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo,kutokana na kuhofia aibu na fedheha kutoka kwa wanajamii ila kusema ni moja wapo ya tiba” amesema Daktari Tatu.

Ripoti ya sensa ya watu na makaazi ya Tanzania ya mwaka 2022 inaonesha kuwa Zanzibar ina wakaazi  milioni 1.8 kati ya hao wanaume ni 915,492 na wanawake ni 974,281. Hii, inamaana kwamba wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar, lakini wingi wao huo hauonekani katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi kutokana na vikwazo na ukatili wa kijinsia  na kisaikolojia wanaopitia.

Anna Athanas Paul, ni Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema kuwa tathimini iliyofanywa na Wizara hiyo  katika taasisi mbali mbali imeonesha kuwa wanawake bado wapo kidogo katika nafasi za Uongozi, ukilinganisha na wanaume jambo ambalo linahitaji kuangaliwa.

 ‘’Takwimu zilizokusanywa na wizara kutoka taasisi mbali mbali kwa mwezi Machi mwaka 2024, zinaonesha ni asilimi 30 tu ya wanawake ambao wako katika  uongozi, ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 70,’’ amesema Naibu Waziri Anna.

Anna, ameongeza kusemabkuwa Serikali inaendelea na jitihada katika kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya 2050 na mpango wa Maendeleo (ZADEP) 2021/2026 ambapo lengo katika nafasi za uongozi ni kufikia 50/50.

Ziko Mamlaka ambazo zinahusika na masuala ya rushwa na uhujumu Uchumi-ZAECA, kupitia Afisa Elimu wake Yussuf Juma Suleiman amesema kuwa hakuna kesi  ya rushwa za ngono zilizoripotiwa  kutokana na suala hilo kufanyika kwa siri.

Amesema kuwa, Sheria ya kuzuia Rushwa na uhujumu Uchumi Zanzibar, sheria namba 5 ya mwaka 2023 kifungu cha 52, kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo hivyo.

Amewataka wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kwanza kusoma elimu ya uraia ,ili kutambua haki zao bila ya kubabaishwa na mtu.

Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar- TAMWA ZNZ ni Taasisi isiyo ya kiserikali  inayojishuhulisha na masuala ya utetezi wa haki za mtoto wa kike ,Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA ZNZ, Dk Mzuri Issa amesema wanawake wanaogombea nafasi za uongozi wanakumbwa na vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia na kisaikolojia. 

”Wanawake wenye nia ya kugombea wasivunyike moyo na wawe majasiri ili kuongeza wingi wao katika nafasi za uongozi mwaka  huu 2025 na kuripoti vitendo hivyo, katika taasisi husika ili waweze kupata msaada,” amesema Dkt Mzuri .

Mohamed Ali Ahmed, ni Naibu Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania ,kwa upande wa Zanzibar amesema kuongezeka kwa kifungu cha 10 C ndani ya sheria ya vyama vya siasa nchini, kinatoa nafasi kwa wanawake kuongeza ushiriki wao na kuwajibika kwa vyama kwa kuwa na sera ya jinsia muda wote ,kwani hapo awali havikupaswa vyama  kuwa na sera hiyo ,”wanawake wanatakiwa kuwa wajasiri na wenye uthubutu ili kuongeza wingi wao katika nafasi za uongozi, na kuviripoti vitendo vyote vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia vinavyowakumba, kwani kugombea nafasi za uongozi ni haki ya kila mmoja raia wa  Tanzania aliyenae na sifa," amemaliza Mohamed.

No comments

Powered by Blogger.