MANENO YENYE UKAKASI KWENYE SHERIA ZA HABARI NI KITENDAWILI.
Na - Maryam Nassor
WAANDISHI wa Habari wa Zanzibar kwa muda mrefu wamekuwa wakililia sheria mbaya za habari zibadilishwe, na kilio hicho kwa takribani miongo miwili sasa kimekuwa kikipita kwenye masikio yenye nta
Sheria ya Usajili wa
Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Namba 5 ya Mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria no. 8 ya mwaka
1997, imekuwa kikwazo kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao bila
hofu kwasababu sheria hiyo ina mitego sana.
Mkataba wa AFRIKAN CHART OF HUMAN AND PEOPLES
RIGHT unataka
kila nchi lazima ikuze demokrasia na uhuru wa kujieleza, ingawa wanaamini kuwa hakuna uhuru ambao hauna
mipaka lakini kutokana na sheria mbaya zenye maneno yasiyo na maana halisi
yanaufanya uhuru usiwepo.
Kifungu cha 30(1)
kinaeleza kuwa ‘’pale ambapo waziri atakuwa na maoni kwamba ni kwa masilahi ya umma au kwa ajili ya amani na utulivu, anaweza kuamrisha
kusimamishwa kwa gazeti na gazeti hilo lazima lisimamishe kazi zake kuanzia
tarehe ya amri iliyotolewa…
Kifungu cha 30(1) cha
sheria hii kimempa Waziri mamlaka ya kulifungia gazeti kwa sababu mbili ambazo
ndio msingi wa Makala hii.
Sababu ya kwanza; Kigezo
cha maslahi ya umma, sheria hii haikufafanua maana ya neno ‘masilahi ya umma’
bali imeelezea kuwa endapo Waziri atakuwa na maoni kwamba kulifungia gazeti ni
kwa maslahi ya umma, ni hatari sana, kwani maslahi hayo yanaonekana yapo au
hayapo kutokana na maoni ya mtu mmoja (waziri) hivyo yameunganishwa na matakwa
ya mtu.
Kigezo cha masilahi ya
umma kimekuwa kikitumika kwenye sheria nyingi na kwa bahati mbaya hakuna sheria
hata moja iliyofafanua neno hilo lina maana gani. Hata hivyo vigezo vifuatavyo
vinaweza kuzingatiwa kama ni vigezo vya maslahi ya umma.
i.
Uhakika wa taarifa husika iliyotolewa na
ambao unaweza kuathiri jamii fulani.
ii.
Taarifa yenye kueneza uchochezi wa siasa
au dini;
iii.
Taarifa yenye kuchochea ubaguzi wa
kidini, kikabila au kisiasa.
iv.
Taarifa za uongo na zenye uchochezi.
Ikiwa Waziri ataelezea
moja kati ya sababu za hapo juu kuwa amefungia gazeti kwa sababu hizo inaweza
kuzingatiwa kuwa amefungia kwa maslahi ya umma.
Sheria imempa mamlaka makubwa Waziri wakati inafahamika kuwa wadhifa huo
ni wa kisiasa, hivyo yupo kwa ajili ya kulinda maslahi ya chama au mamlaka
iliyopo, hivyo ikitokea habari ambayo inakosoa upande wake wa kisiasa anaweza
kutumia mwanya huu wa sheria kulifungia gazeti husika.
Sababu ya pili; ni
kigezo cha amani na utulivu ambacho kifungu cha 30(2) pia hakikufafanuliwa
maana yake halisi.
Akizungumza na Mwandishi
wa Makala hii, Afisa kutoka Ofisi ya Watetesi wa Haki za Binadamu Zanzibar (
THRDC) Shadida Mohamed anasema kuwepo na vifungu vyenye maneno magumu
yasiyo na maana halisi katika sheria yanaviza uhuru wa kujieleza.
Amesema kuwa, kifungu
cha 30 cha sheria hii ya Usaliji wa Wakala wa Habari kinasema kuwa endapo Waziri ataona ni kwa ‘maslahi ya umma’
au kwa ‘amani na utulivu’ anaweza
kuamuru kufungiwa kwa gazeti na gazeti litakoma kuchapishwa kuanzia siku hiyo
ni kitu kibaya sana kwa tasnia ya habari.
“Hasara ni kubwa kwa waandishi
wa habari kutokana na sheria kama hizi ambazo zinakwenda kinyume na mikataba ya
kimataifa ya kulinda haki za binadamu,” anasema Shadida.
Amesema kuwa, mamlaka
hayo ya kiutendaji ni makubwa kwa Waziri na anaweza kuyatumia kwa maslahi yake
binafsi au ya kisiasa badala ya maslahi ya umma, kwani mawaziri wengi wanateuliwa kutokana na mrengo
wa kisiasa.
“Lazimaa Sheria
iainishe kwa uwazi maana halisi ya
maslahi ya Umma na Amaani na Utulivu na hali zipi zinaweza kufungiwa kwa
gazeti” anashauri Shadida.
Naye, Mwanasheria Ali
Amour kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar anasema kuwa Waziri asipewe mamlaka ya
kufungia gazeti kwani hiyo itapelekea kuathiri uhuru wa habari.
Amesema kuwa, hofu ya chombo
cha habari kufungiwa inaweza kufanya vyombo vya habari kuepuka kuandika habari
zinazokosoa Serikali hata pale panapohitajika.
“Ni vyema sheria
zikafafanua kwa uwazi maneno kama hayo kwani yanaathiri vibaya tasnia ya
habari,” anashauri Ali.
Naye, mwandishi wa habari
mkongwe visiwani Zanzibar, Salim Said Salim anahoji ugumu wa kubadilishwa
sheria kandamizi kama hizi uko wapi? Kwani sheria nyingi za zamani
zinabadilishwa.
“Waandishi wa Habari
tumechoshwa na sheria kandamizi zenye maneno yasiyo na maana halisi, tunataka
sheria zinazokwenda na wakati na zinazojali haki za binadamu.” anasema Salim.
Naye, Mjumbe katika Kamati ya Wataalam wa Masuala ya Habari
Zanzibar (ZAMECO) Jabir Idrissa anasema
sheria ilitakiwa ieleze kwa uwazi na upana wake maana halisi ya maneno haya, ‘maslahi ya umma’ na ‘amani na utulivu.
Aidha amesema kuwa,
dunia sasa imekuwa ni kijiji kutokana na kukua kwa teknolojia, hivyo ni vyema
kuwepo sheria nzuri za habari ili waandishi watumie kalamu zao kuikosoa
Serikali inapobidi bila ya hofu ya
kufungiwa vyombo vyao.
Zaina Mzee ni Afisa
Programu ya Uchechemuzi wa Sheria za Habari kutoka Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania - TAMWA (ZNZ), amewataka waandishi wa habari kuendelea
kufanya uchechemuzi kwa kuandika habari na makala ili sheria rafiki za habari
zipatikane.
Aidha amesema kuwa, “huu
ni wakati wa kuungana pamoja waandishi wa habari na wadau wa habari kupigania
sheria rafiki ya habari ipatikane.”
Mwisho

Post a Comment