UKATILI WA KIJINSIA UNAVYOWATIA HOFU WAGOMBEA WA KIKE, KUTOKA VYAMA VYA UPINZANI.



NA MARYAM NASSOR,

HUU ni mwaka wa uchaguzi nchini Tanzania,  ni miaka mitano  imepita  tokea   kufanyike uchaguzi wa  mwisho wa mwaka 2020,  lakini baadhi ya wagombea   wanawake waliyo shiriki  uchaguzi   huo kutoka vyama vya upinzani,   bado wanauguza majeraha  na vidonda  visivyo poa vya kunyanyaswa na   kupoteza ndugu zao wa karibu , watu wengi waliyeruhiwa na wengine kupoteza maisha.

   Mmoja wa hao ni Halima  Ibrahimu Mohamed,(40)   ambae   ni mwana siasa    aliyeshiriki  katika uchaguzi huo  kutoka  chama cha upinzani , lakini  kinyume cha matarajio yake  anasimulia  ukatili uliyo mkuta   ambao ulimshangaza  katika safari yake ya  kutafuta uongozi .

 Halima ambae  ana diploma  ya kozi ya ukarani, ni mama wa watoto watano, anaishi na mume wake kisiwani Unguja,   alianza safari yake ya siasa tokea miaka ya 1994,   anaeleza jinsi alivyokutwa  na  ukatili wa kijinsia wakati anagombea nafasi ya Uwakilishi mwaka 2020.

  Hii, ni baada ya kutakiwa   kutoka katika chumba cha kupigia kura  na  watu ambao wanadaiwa  kutoka vyombo vya dola , akiwa ni mgombea wa  Uwakilishi  kutoka ,Chama cha ACT Wazalendo katika jimbo la Malindi lenye wadi mbili na shehia 11.

"Nilitolewa katika chumba Cha kupigia kura, wakati Mimi nilikuwa ni mgombea   halali wa uwakilishi katika Jimbo  hilo mwaka 2020  na niliporudi  jioni kutaka kulinda kura zangu wakati niko njiani naelekea  kituo vha kupigia kura  alitokea askari mmoja  akaniekea bunduki kifuani kwangu  eti kunitaka nirudi nilipotoka," Anasimulia  Halima.

Amesema kuwa, Wakati wa uchaguzi  huo  alivumilia ukatili wa kimwili , vitisho lakini  pia mara kadhaa alinusurika kupigwa risasi na vikosi vya usalama ,“ Kiukweli wakati wa uchaguzi hapa kwetu Zanzibar hali si shwari , vitisho ni vingi hasa kwa sisi tunaogombea katika vyama vya upinzani,”  anasema Halima .

Katika hali kama hiyo, anasema  vitendo vya ukatili wanavyo fanyiwa wagombea wa upizani wakati  wa uchaguzi vinawavunya moyo, wanawake kurudi kwenye kinjanyanyiro' cha kutafuta  uongozi.

"Kila nikikumbuka Jinsia nilivyotolea katika chumba cha kupigia kura, na kunyimwa haki yangu  ya kuangalia  hesabu za kura zangu,  na mwenzangu wa chama x akaachwa ashuhudie kura zikihesabiwa, nilipata maradhi, " amesema Halima.

 Kama Hali haitabadilika katika  uchaguzi mkuu  wa mwaka 2025, basi wanawake wengi wa vyama vya upizani, hawatagombea  kwani hali ile  inawavunjwa moyo kugombea nafasi za uongozi, kutokana na ukatili unaowakuta wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo, huyo hakuwa pekee yake , ukatili  wa kijinsia  kwa wanawake wakati  wa uchaguzi ni suala linalowatafuna wanawake wengi wa vyama  vya siasa  hasa  kutoka vyama vya upizani, kama ulivyomkuta Asiata  Abubakar ( 40) .

Asiata  Abubakar, ni miongoni mwa wanawake  waliokumbwa na ukatili  unaohusishwa na uchaguzi ,  ambae aligombania  Ubunge  katika Jimbo la kikwajuni Unguja,  Kwa tiketi ya Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),  anasimulia ukatili wa kimwili na kisaikolojia uliompata wakati wa uchaguzi  mkuu mwaka 2020.

Anaeleza kuwa, aliambiwa na vyombo  vya dola, atokee nje  ya kituo cha  kupigia kura,baada ya kushuhudia mtu anapewa karatasi za kura zaidi ya moja." Ndipo nilipotolewa nje ya kituo cha  kupigia kura, eti sijulikani kama mimi  ni mgombea wa  ubunge katika Jimbo la kikwajuni "anasimulia Asiata.

Mwanasiasa huyo, ambae  aligombea ubunge   katika uchaguzi huo  anasema wagombea wa upizani wanapitia ukatili na udhalilishaji kutoka kwa  vyombo vya dola , ambao wao hawahusiki na uchaguzi."Jukumu la kulinda uchaguzi ni  la jeshi la Polisi na si la vyombo vya dola, kwani wao ndio wanaovuruga uchaguzi’’ amesema Asiata.

Utafiti uliyofanya na Taasisi ya kitaifa ya kidemokrasia -NDI  ikishirikiana na Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar TAMWA-ZNZ  imesema  Zanzibar imekumbwa na vurugu zinazohusishwa na uchaguzi , hasa uchaguzi wa mwaka 2020.

Ripoti, iliyoandaliwa na Chama Cha ACT-Wazalendo, kuhusu matukio ya vurugu zinazohusishwa na uchaguzi wa mwaka 2020, jumla ya matukio 343 ya udhalilishaji  yanayohusishwa  wanaume 256 na wanawake 87 yalitokea wakati wa uchaguzi, watu 14 walikufa na 55 walijeruhiwa kati ya Oktoba 26 hadi 30 mwaka 2020.

Tunu Juma Kondo, ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania  (UWT)   amesema  ni vyema wanawake wanaotia nia ya kugombea nafasi za uongozi, lazima  wajidhatiti na  wapambane katika  kutafuta nafasi hizo, ili kuongeza wingi wao hasa kugombea katika majimbo ambako huko wanawake bado wako kidogo.

“ Wanawake  wanaotia nia ya kugombea nafasi za Uongozi katika Uchaguzi Mkuu, lazima wajidhatiti  na wawe majasiri ili kuingia katika nafasi za uongozi” amesema Tunu.

Zanzibar imesaini mikataba mbali mbali ya kumlinda mwanamke dhidi ya aina zote za ukatili na udhalilishaji kama mkataba wa Cedaw ,Mkataba  huu  umeanzishwa mwaka 1979, lengo la mkataba huo ni kumlinda mwanamke na ukatili na Udhalilishaji unaowakuta  lakini utekelezaji wa mkataba huo bado unasuasua.

Kwa mujibu wa ripoti ya sensa  ya watu na makazi ya Tanzania ya  mwaka 2022, inaonesha  kuwa  Zanzibar  ina wakazi  wapao milioni 1.8  kati ya hao wanaume ni 915,492 na wanawake ni 974, 281.

 Hii ina maana kwamba,  wanawake ni asilimia  51.6 ya wakaazi wote  wa Zanzibar, lakini wingi wao huo hauonekani katika  nafasi za uongozi, kutokana na mambo mengi  lakini  pia , ukatili wa kijinsia unaowakuta wanawake kipindi cha uchaguzi.

Chama Cha Wandishi wa habari Wanawake Tanzania  Zanzibar,(TAMWA, ZNZ) ni Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishuhulisha na utetezi wa haki za Mtoto wa  kike, na kuhamasisha wanawake  kushiriki katika nafasi za Uongozi Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo  Dk Mzuri Issa, amesema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar -ZEC  inapaswa iwe na vikosi maalumu vinavyolinda uchaguzi na viwe chini ya tume hiyo, ili kuepusha vurugu wakati wa uchaguzi." Tumekuwa tukishuhudia vurugu na ukatili dhidi ya wanawake wakati wa uchaguzi na kupelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika majimbo" amesema Dr Mzuri.

 Ili kuengeza, ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi katika vyama vyote vya siasa , ni lazima tuwe na siasa  safi  ambazo hazina  vurugu.  ‘’ Kama tunataka kuongeza wingi wa wanawake katika nafasi za uongozi basi, ni lazima tuwe na siasa safi ambazo hazina vurugu’’ amesema Dk Mzuri.

Mkurugenzi waTume ya Uchaguzi Zanzibar -ZEC Thabiti Idarous Faina, amesema kuwa, tume  ya Uchaguzi haina takwimu za makosa ya ukatili na udhalilishaji unaotokea wakati wa uchaguzi,kwani takwimu hizo zinapelekwa kituo cha  Polisi." Kazi kubwa ya tume ya Uchaguzi ni kusimamia  shuhuli za Uchaguzi,  lakini haina takwimu za  kesi za Udhalilishaji unaotokea wakati wa Uchaguzi ‘’ amesema  Faina.

Ziko Mamlaka ambazo zinahusika na maswala ya ulinzi  na Usalama kwa raia na mali zao, Mkuu wa jeshi la Polisi  Mkoa wa Kusini Unguja, SP Daniel Shila, amesema  jeshi la Polisi  limejipanga  na litaendelea kulinda rai na mali zao  kama inavyowataka sheria  ya jeshi hilo sura ya 322.

Katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kugombea nafasi za uongozi,  amesema kuwa watasimamia sheria za nchi kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria. ‘’Tutamchukulia hatua mtu yoyote ambae, atahusika na vurugu kipindi cha uchaguzi, ikiwemo watakao toa maneno machafu kwa wagombea wanawake, hivyo tunatoa wito  kwa jamii , mgombea  yoyote wakike atakaefanyiwa vurugu wakati wa uchaguzi , aje kuripoti na  tutachukuwa hatua’’ amesema SP Shila.

 

                                 MWISHO

 

 

No comments

Powered by Blogger.