“Wanawake katika Uongozi  ni chachu ya kufikia dunia yenye usawa”

 NA MARYAM NASSOR

Pili Said Mohamed  diwani wa wadi ya Mahonda  wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja   simulinzi yake katika harakati za uongozi  inaonesha  historia ya kipekee katika  safari  za wanawake  wengi  wenye ndoto za uongozi visiwani  Unguja.

Pili   ambae alianza harakati za siasa mwaka  2020 akiwa mwanachama hai wa chama cha Mapinduzi-CCM ambaye aligombea nafasi ya udiwani mara mbili mwaka 2020 na mwaka 2015 ndipo aliposhinda na kuwa diwani.” Sikukata  tamaa, niligombea mara mbili nafasi ya udiwani, na mwaka  ule  (2015)  bahati ilikuwa upande wangu nilifanikiwa  kuupata  udiwani” amesema Pili.

Pili ambae ni mkulima na mama wa nyumbani, amesema   ushiriki mdogo wa wanawake katika  nafasi za uongozi  zinawanyima  wanawake  fursa za kushika nafasi za juu za uongozi na vyombo vya maamuzi. “Niliingia katika siasa kuongoza kama kielelezo. Kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma. Kwa miaka yote katika baraza letu la Madiwani, nimehakikisha masuala ya wanawake na watoto yanapewa uzito na umuhimu sawa”

Amesema kuwa, licha ya uhaba wao katika nafasi za uongozi lakini wakipata nafasi ya uongozi, wanafanya vizuri  ikiwemo kutetea haki za wanawake na Watoto na kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo katika wadi zao.”Nilijiunga  na siasa kwa sababu  nilitaka  kufanya mambo mengi  zaidi kwa ajili ya wasichana na wanawake ambao huku kwetu vijijini tuko nyuma kimaendeleo, katika kuwawezesha wanawake kiuchumi  wachukuwe mikopo  wajiendeleze kimaendeleo”

Amesema kuwa,  masuala mengi yanayohusu  wanawake hayaingizwi katika  sera, mipango na bajeti za Halmashauri  kwani wengi wanaoshikilia nafasi za juu za  upatikanaji  wa maji, uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake  zinashikiliwa na wanaume, hivyo ni vyema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wanawake  wajitokeze kwa wingi  kugombea nafasi za uongozi ili kuongeza ushiriki wao.

Maryam Ali Mussa diwani wa viti maalum katika Baraza la Manispa  wilaya ya Mjini Unguja , amesema  ushiriki  wa wanawake katika nafasi za uongozi bado ni mdogo, na kuwataka  wanawake  kuongeza ushiriki wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025.

Amesema kuwa, ni vyema wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kujitathimini kabla ya kugombea  nafasi wanayoitaka kugombea ili iwe rahisi kuipata” Nawashauri wanawake wenzangu wanaotaka kugombea ni vyema kuangalia kwa makini na kujitathimini nafasi wanazotaka kugombea ili iwe rahisi kwako  kuwahudumia wananchi watakapo chaguliwa” ameshauri   diwani  huyo wa viti maalum.

Amesema  kuwa, huu ndio wakati wa wanawake kushirikiana  kuelekea katika uchaguzi mkuu ili kupeana uzoefu wa kugombea ,na kushika majimbo mengi ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa takwimu   kutoka tume ya uchaguzi – ZEC  ya mwaka 2020  idadi ya madiwani  ni 110 wanaume  wakiwa 85 sawa na asilimia  77%  na wanawake 25  sawa na asilimia 23, huku wawakilishi  wanawake wa kuchaguliwa ni wanane kati ya 50 sawa na asilimia 16.  

 Kwa upande wa wabunge wa Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania wanaoiwakilisha Zanzibar  kwenye majimbo 50 ya  uchaguzi ni wanne tu, sawa na asilimia nane.

 Hali hiyo inaonesha,  haja ya wanawake kuongezeka  katika nafasi za uwakilishi  katika majimbo ya uchaguzi ifikapo  2025, kwani idadi ya wawakilishi  wanawake ni kidogo.

 Dk Mzuri Issa ni Mkurugenzi  Mtendaji wa Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar -TAMWA -ZNZ ambao kwa kushirikiana na Taasisi ya Kidemokrasia  -NDI, walifanya  utafiti juu ya kujua hali ya wanawake viongozi kwenye vyama vya siasa,” Ushiriki hai wa wanawake katika  siasa mara nyingi  husababisha  kuimarika  kwa hali ya kijamii na kiuchumi, kwani wanawake wana uwezo wa  kukabiliana na kupunguza umasikini ukilinganisha na wenzao  wanaume”Amemaliza Dk Mzuri  akiwa Ofisini kwake Tunguu Zanzibar.

Amesema kuwa,Ipo haja kwa Serikali, asasi za kiraia na vyama vya siasa kushirikiana na kufanya kazi kwa Pamoja ili  kuondoa vikwazo kwa wanawake ili  iwe rahisi kwao  kugombeea nafasi za uongozi, huku akiona utekelezaji wa mikataba na matamko mbali mbali ya kikanda na kimataifa ya kuhamasisha usawa wa kijinsia bado utekelezaji wake  haujafikiwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya sensa  ya watu na makazi ya Tanzania ya  mwaka 2022, inaonesha  kuwa  Zanzibar  ina wakazi  wapao milioni 1.8  kati ya hao wanaume ni 915,492 na wanawake ni 974, 281.

Hii ina maana kwamba,  wanawake ni asilimia  51.6 ya wakaazi wote  wa Zanzibar, lakini wingi wao huo hauonekani katika  nafasi za uongozi.

Abdulrazak Said Ali   mwanasheria kutoka   Ofisi ya msajii wa vyama vya Siasa Zanzibar ,amesema   kuongezwa kwa kifungu cha 10 C katika sheria ya vyama vya siasa  nchini itasaidia kuongeza kwa ushiriki wa wanawake kwani sheria hiyo inavitaka vyama vya siasa kuwa na sheria ya jinsia kwa muda wote” Lengo la kuongeza kwa kifungu hichi katika sheria ya vyama vya  siasa nchini ni kuongeza ushiriki wa wanawake  kwa kuwa na sera ya jinsia  kwa muda wote” amesema mwanasheria huyo.

 

                                          MWISHO

                                         

No comments

Powered by Blogger.