VITI MAALUM VINAVYOWALEMAZA WANAWAKE KUGOMBEA MAJIMBONI.


NA MARYAM NASSOR

 VITI Maalumu vya wanawake ni nafasi zinazotolewa na Serikali  kwa lengo la kuongeza idadi ya wanawake katika bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ingawa utaratibu huo  hutumiwa na nchi mbali mbali  duniani katika siasa,   kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Uwakilishi wa wanawake kupitia viti maalumu, sio wa kudumu ni nafasi za kujiandaa kisiasa, Pamoja na kuandaa mbinu za kupata ushindi wanapokwenda  jimboni ili iwe rahisi kwao  kushinda na kuwatumikia wananchi.

Lakini kinachotokezea  kwa baadhi ya wanawake  wanaopata nafasi hizo,wanahudumu  kwa  muda mrefu, tofauti na malengo  yake na kuwalemaza kwa hofu ya kuingia majimboni.

Asya Mohamed, ni mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini  Unguja kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo -CHADEMA amesema ni kweli viti maalum vinawalemaza baadhi ya wanawake wanaopata nafasi hizo.

Amesema kuwa, vyama haviwazuii pia kuendelea kugombea nafasi hizo, kwani hakuna sheria maalum iliyoweka ukomo wa viti maalum wa muda wa kugombea ni wewe mwenyewe na uwamuzi wako.” Lakini ni vyema kukaa miaka mitano tu inatosha kujipanda na kujiandaa kwenda jimboni kwani na wengine wanataka nafasi hizo ili kujifunza” ameshauri mbunge huyo.

Ameeleza kuwa,  ni vyema ukawekwa ukomo na sheria  maalumu inayowataka wagombea wa nafasi hizo, kukaa kipindi kimoja tu ili  nafasi hizo, zisiwalemaze  wanawake na badala yake wazitumie kwa kujifunza siasa na kugombea majimboni.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka baraza la wawakilishi Zanzibar (BLW)  idadi  ya wajumbe wote ni 78 kati yao wanawake ni 29 na wanaume 48, huku wanawake wawakilishi wa majimbo kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni wanne tu, wanaume wakiwa 42 na wanawake wa viti maalum ni 18 na wajumbe waliobakia ni nafasi za kuteuliwa na Rais.

Fatma Abdul habib Ferej Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, amesema kuwa  wanawake wengi wanaochaguliwa katika nafasi za viti maalumu, wanaenda kinyume  na dhamira ya kuanzishwa kwa nafasi hizo, kwa kudumu kwa muda mrefu.”Wapo wanawake wanaong’ang’ania nafasi za viti maalumu kwa miaka mingi , japo uwezo wao unaruhu Kwenda jimboni kugombea na kujilemaza kisiasa” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema kuwa, ni vizuri kuwekwa sheria ya  ukomo wa nafasi za viti maalum, kwani ipo haja kwa wanawake kuingia kwenye majimbo kugombea ili kuongeza wingi wao.

Ameeleza kuwa, wapo wanawake ambao  ni mfano mzuri wa kijifunza kutoka kwao, ni Rais Samia ambae alikaa kwa kipindi kimoja tu  katika nafasi za viti maalum na kijitupa jimboni katika jimbo la Makunduchi mkoa wa Kusini Unguja.

Mwakilishi wa jimbo la Mahonda, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja Asha Abdalla Mussa  amesema  kuwa, hakupita kwenye viti maalum alitoka kwenye nafasi ya udiwani  na kujitupa jimboni,” Wanawake tukiamua tunaweza ni vizuri kuwa na uthubutu  na kujiamini na utafanikiwa” Amesema Mwakilishi huyo huku akiwasihi wanawake mwaka 2025 kuchangamkia fursa za majimboni na wakikosa watarudi kwenye viti maalum.

   Mkurugenzi  wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar -TAMWA ZNZ, amesema ni kweli vyama vya siasa haviwasaidii wanawake  kuondokana na viti maalumu.’’ Kuna mtu utamkuta yupo anagombea kiti maalumu miaka mitano hii na mingine na bado yupo hapo hapo wakati inatakiwa mtu akae miaka mitano ajifunze kisha atokee aende jimboni akagombee” ameshauri Dk Mzuri.

Amesema kuwa, kutokana na hali hiyo ipo haja ya wanawake kuongezeka katika nafasi za  uwakilishi katika majimbo  ya uchaguzi ifikapo 2025 kwani idadi ya  viongozi wanawake wa kuteuliwa ni ndogo sana.

Ripoti ya sensa ya watu na makaazi ya Tanzania ya mwaka 2022, inaonesha  kuwa Zanzibar ina wakaazi milioni 1.8 kati ya hao wanaume  ni 915,492 na wanawake ni 974,281.hii ina maana kwamba  wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar, lakini wingi huo hauonekani katika nafasi za uongozi.

Mchambuzi wa Masuala ya uongozi na Siasa  Visiwani Zanzibar , Almasi Mohamed amesema kuwa,wanawake wengi wanaohudumu nafasi za viti maalumu wanajisahau na kubaki kwa kipindi kirefu katika nafasi hizo kinyume na malengo yake.” Uhaba wa wanawake katika majimbo bado  unaendelea kutokana na wale ambao, wanajifunza siasa kupitia nafasi za viti maalum , ni vyema mwaka 2025  wakajitupa majimboni kugombea ili kuongeza wingi wao” ameshauri Mchambuzi huyo.

Amesema kuwa, ipo haja kwa wanawake  waliopitia katika viti maalum kuonesha uthubutu wao kugombea katika majimbo mwaka 2025  ili kuongeza wingi wao katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi.  

 

 

 

 

 

No comments

Powered by Blogger.