“Majukumu ya
nyumbani sio kikwazo tena kwa wanawake kugombea uongozi”
Na Maryam
Nassor,Zanzibar
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mikataba mbali mbali ya kikanda na kimataifa
ya kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya
wanawake, kama mkataba wa Cedaw ambao umeanzishwa mwaka 1987 na kuheshimu haki za wanawake kama
haki za binaadamu.
Licha ya
kuwa katiba ya nchi inatambua haki za raia wote, bado wanawake kama walivyo
raia wengine, hawajui haki zao na namna ya kuzitafuta hii inatokana
na sheria kuandikwa kwa lugha
ya kigeni na ya kisheria.
Katika ulimwengu wa sasa suala la usawa wa
kijinsia, limekuwa suala muhimu sana
hasa linapozungumziwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na vyombo
vya maamuzi.
Miongoni mwa mambo yanayowarudisha nyuma wanawake
katika kugombea nafasi za uongozi ni
mifumo dume, mila na desturi lakini pia mgawanyo wa majukumu kijinsia jambo ambalo
kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025
wanawake wamejipanga, na majukumu ya nyumbani sio kikwazo tena kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi.
Pavu Juma Abdallah Naibu Katibu Mkuu wa haki za Binadamu kutoka Chama cha ACT
Wazalendo , ambae alishawahi kugombea nafasi mbali mbali katika chama hicho Ni
mmoja wa wanawake wanao ona kuwa,
majukumu ya nyumbani sio kikwazo tena kwa wanawake kuwa viongozi.
Amesema
kuwa, kwenye siasa kuna changamoto
nyingi zinazowakumba wanawake ikiwemo
ukosefu wa fedha za kujikimu wakati wa kampeni lakini majukumu ya nyumbani
hawayachukulii tena kama kikwazo cha wao, kushiriki na kugombea nafasi za
uongozi,”majukumu ya nyumbani sihisi kama ni kikwazo kwani nilazima ujipange
vizuri katika majukumu na mikakati yako”
amesema bi Pavu.
Amesema
kuwa, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni vizuri wanawake kugombea katika
majimbo nafasi mbali mbali za uongozi ikiwemo udiwani, uwakilishi na ubunge
kwani huko bado kuna upungufu wa wagombea wanawake” mwaka huu ni mwaka wa
uchaguzi mkuu wanawake tuwe na mikakati
yetu na tujipange zaidi kila kwenye chanagamoto basi tuzichukulie kama fursa”
ameshauri bi Pavu.
Maryam Ali Mussa diwani wa viti maalum kutoka Chama cha Mapinduzi – CCM amesema kuwa
majukumu ya nyumbani ni mujibu kwa mwanamke mfano mzuri ni kwa mama Samia yeye
ni Rais lakini tunamuona siku anayokuwa
na muda anaingia jikoni anapika kwasababu
ni kazi za mwanamke ,” kazi za nyumbani
tunafundishwa tokea tuko wadogo majumbani kwetu vipi ziwe kikwazo kwetu
zitufanye tusishiriki katika kugombea nafasi za uongozi ambazo ni haki yetu ni
kujipanga tu” amehoji Maryam.
Amesema kuwa,
hayo sio kikwazo tena kwa wanawake
kwani upo mfano mzuri Tanzania wa rais mwanamke ambae amejipanga hadi kufika pale, kuelekea uchaguzi mkuu ni muhimu wanawake wakawa
na uthubutu kujitupa majimboni kugombea nafasi mbali mbali za uchaguzi ili
kuongeza ushiriki wao. Wanawake katika uongozi sio tu sauti za mabadiliko, bali
ni chachu ya kufikia dunia yenye usawa na matumaini
Sensa ya
watu na makaazi ya mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina watu milioni 1.8 kati ya hao wanaume ni 915,492 na
wanaake ni 974, 281, hii inamanisha
kwamba wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar lakini
wingi wao huo hauonekanikatika nafasi za uongozi.
Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania- UWT kwa upande wa Zanzibar kutoka
chama cha Mapinduzi -CCM Tunu Juma Kondo
amesema ,Licha ya wanawake kuwa ni wengi
bado kumekuwa na upungufu wa wanawake
kushiriki katika nafasi za uongozi kutokana na
hapo awali wengi wa wanawake walikuwa hawajui kuwa
kugombea nafasi za uongozi ni haki yao
na walikuwa wanadhani kuwa nafasi zile zipo kwa ajili ya wanaume tu.
Akizungumzia kuhusu majukumu ya nyumbani kwa
wanawake amesema sio kikwazo kabisa, kwani wapo watu ambao ni wafanyakazi wanaenda kazini lakini wakirudi nyumbani
wanaihudumikia familia na hawaoni kama
ni kikwazo,” Tunatakiwa tujipange
kufanya majukumu yetu ya
nyumbani lakini pia tushiriki
katika nafasi mbali mbali za uongozi ili kuongeza ushiriki wetu kwani ni haki yetu kugombea”
ameshauri Tunu.
Amesema
kuwa, takwimu zinaonesha wanawake wapo
kidogo katika nafasi za uongozi Hali hiyo inaonesha haja ya wanawake kuongezeka katika nafasi za uwakilishi katika majimbo, ifikapo
uchaguzi wa mwaka huu 2025, kwani
idadi ya wanawake ni kidogo katika
majimbo.
Kwa mujibu
wa takwimu kutoka baraza la wawakilishi
Zanzibar (BLW) idadi ya wajumbe wote ni 78 kati yao wanawake ni 29
na wanaume 48, huku wanawake wawakilishi wa majimbo kupitia uchaguzi mkuu wa
mwaka 2020 ni wanne tu, wanaume wakiwa 42 na wanawake wa viti maalum ni 18 na
wajumbe waliobakia ni nafasi za kuteuliwa na Rais.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Anna Athanas Paul, amesema tathimini iliyofanywa na wizara hiyo, katika
taasisi mbali mbali imeonesha kuwa wanawake bado wapo kidogo katika nafasi za
Uongozi, ukilinganisha na wanaume jambo ambalo linahitaji kuangaliwa. ‘’Takwimu
zilizokusanywa na wizara kutoka taasisi mbali mbali kwa mwezi machi mwaka 2024,
zinaonesha ni asilimi 30 tu ya wanawake ambao wako katika uongozi, ukilinganisha na wanaume ambao ni
asilimia 70’’ Amesema Naibu Waziri Anna.
Anna, ameongeza kuwa Serikali inaendelea na jitihada katika
kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya 2050 na mpango wa Maendeleo (ZADEP)
2021/2026 ambapo lengo katika nafasi za uongozi ni kufikia 50/50. “ Serikali
imejipanga kuhamasisha ushiriki wa
wanawake katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi na lengo ni kufikia 50/50” amesema Anna.
Mohamed Ali Ahmed, ni Naibu Msajili wa
vyama vya Siasa Tanzania ,kwa upande wa Zanzibar, amesema kuongezeka kwa kifungu
cha 10 C ndani ya sheria ya vyama vya siasa nchini, kinatoa nafasi kwa wanawake
kuongeza ushiriki wao ,na kuwajibika kwa vyama ,kwa kuwa na sera ya jinsia muda
wote kwani hapo awali havikupaswa vyama kuwa
na sera hiyo.”amemaliza naibu msajili huyo .
MWISHO
Post a Comment