WAZIRI PEMBE ATAKA USAWA WA KIJINSIA MICHEZONI

NA MARYAM NASSOR,

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na  Watoto, Riziki Pembe Juma, amesema Usawa wa kijinsia ni lazima uzingatiwe Kila sehemu, ili kujenga Jamii yenye Usawa.

Ameyasema hayo,  huko katika uwanja wa Mau,katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Mkakati  Jumuishi wa Jinsia katika Michezo Zanzibar, wa mwaka 2024/25-2028/29.

Waziri Pembe, amesema kuwa Mpango huo mkakati, umekuja kusaidia Utekelezaji wa sera ya Michezo, ya mwaka 2018 na kuuondoa vizuizi vya kiutamaduni  na  kidini, vilivyopo.

"Kwenye huu Mpango Mkakati umezingatia, Usawa wa kijinsia, na kuondoa, vizuizi vya kiutamaduni na dini, ambavyo vipo"amesema Waziri Pembe .

Aidha, amesema kuwa Mpango huo, umezingatia kukuza Usawa wa kijinsia na ujumuishi kupitia michezo Kwa  wote, hususani Kwa Makundi maalumu ya watu wenye ulemavu.

Amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inataka Usawa wa kijinsia, Kila sehemu  hata kwenye Michezo, kutokana na hapo awali ulikuwa haupo.

Mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar, (ZAFELA)   ambao walioshiriki katika kuandaa Muongozo huo, Jamila Mahmoud, amesema ni vyema,ukapelekwa Kila sehemu ili walengwa wapate kusoma na kuuelewa ili kupata kujilinda.

Amesema kuwa, Muongozo huo wa kumlinda Mtoto wa kike, na watu wenye ulemavu, utasaidia kuweka mazingira salama michezoni na Kila mtu kushiriki michezo.

Nae, Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau ,Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara Hiyo, amesema Mpango Mkakati huo, utatoa ulinzi Kwa watu  wote, hususani watu wenye Ulemavu, na kuifanya Michezo  kuwa,sehemu salama Kwa Kila mtu kushiriki.

Aidha, ametoa wito Kwa Jamii na Wana michezo Kwa ujumla, kuusoma  muongozo huo na kuuelewa.


Hija Mohamed Ramadhan, ni mshauri Jinsia kutoka Taasisi ya Ujerumani (GIZ) amesema   kupitia mradi wa michezo Kwa maendeleo, watahakikisha , michezo hiyo inakuwa  sehemu salama,na  kuhamasisha Usawa  wa kijinsia.

Amesema kuwa, kupitia Mpango Mkakati Jumuishi wa Jinsia katika Michezo, utasaidia kutekeleza  sera ya Michezo ya Zanzibar ya mwaka 2018 ya Michezo Kwa wote.

Nao, baadhi ya wanamichezo wa Timu ya  Kabadi ya Km km,  Hajra Shauri na Faidha Ramadhan, walisema  Mpango Mkakati huo, ni Mzuri na kutoa wito Kwa wanamichezo wengine kuripoti vitendo vya Udhalilishaji vinavyotokea michezoni, ili wafanyaji wachukuliwe hatua.

Walisema kuwa, Mpango Mkakati huo, ni vyema ukawafikia walengwa, kwani wao ndio wathirika wakubwa wa vitendo vya Udhalilishaji Michezoni, na hawana elimu ya kuviripoti.

Mpango  Mkakati Jumuishi wa Jinsia katika Michezo, Zanzibar wa mwaka 2024/25- 2028/29.umeandaliwa Kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, wakiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Asasi za kiraia, Mashirikisho ya Michezo na Jamii Kwa ujumla.

No comments

Powered by Blogger.