Wadau washauri Michezo itumike kama njia ya kujikinga na Ukatili wa Kijinsia.
NA MARYAM NASSOR,
Sera ya
Michezo ya Zanzibar ya mwaka 2018,
imetamka wazi nia njema ya Serikali ,
katika kuhakikisha Usawa wa kijinsia katika Michezo.
Haya hivyo,
Sera hiyo haifanyi kazi ipasavyo, kama
wachezaji wakike na kiume
hawatopewa Elimu ya kujikinga na vitendo vya Udhalilishaji katika Michezo.
Kwa mujibu
wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa
Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF ya mwaka
2024,Inaonesha kuwa Zaidi ya wasichana
na wavulana milioni 370 ni waathirika wa ukatili wa kijinsia duniani kote,
kabla ya kutimia umri wa miaka 18.
Kulingana na
ripoti hiyo, inaonesha kwamba msichana
mmoja kati ya wanne ameathirika na aina hii ya unyanyasaji mbali na ule wa
kimtandao au wa maneno , idadi ya wasichana na wanawake waliyoathirika duniani kote imeongezeka
hadi kufikia milioni 650 , huku ikisisitiza umuhimu wa kuchukua mikakati ya dharura kukabiliana na hali hiyo.
Hivyo,Ipo haya ya kuitumia michezo kama njia
ya kujikinga na vitendo vya ukatili na Udhalilishaji, kwa wasichana na wavulana
Kwani vitendo hivyo, Kila kukicha
vinaonekana kuongezeka.
Akizungumza
na mwandishi wa makala hii, mchezaji wa
mpira wa miguu timu ya Wanawake ya
Worrious, Saada Saidi, amesema kwenye michezo kunatokea
vitendo vingi vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia hasa kwa wasichana
lakini pia na wavulana .
Amesema
kuwa, Ipo haja Kwa wachezaji kupewa elimu ya Udhalilishaji na ukatili wa
kijinsia kwani madhara ya vitendo hivyo,
huwa na athari kubwa na za kudumu
kwa waathirika wa vitendo hivyo.
Aidha amesema
kuwa, ukatili wa kijinsia dhidi ya Watoto ni janga,
na linaleta majeraha makubwa na
ya kudumu,ambapo waathirika hulibeba hadi utuuzima.
"Sisi
wachezaji wa mpira wa miguu, tunanza kucheza mpira tukiwa wadogo, na hatupewi
elimu ya kujikinga na Udhalilishaji Kwa hivyo, hata ukifanyiwa Udhalilishaji na
kocha wako hujui kama umedhalilishwa" amesema Saada.
Aidha
amesema kuwa, ni muhimu wachezaji wakapewa elimu ya kujikinga na vitendo vya
Udhalilishaji kupitia michezo kwani, vitendo hivyo vimekuwa vikiwarudisha nyuma wachezaji kufikia ndoto zao.
“ Wachezaji
wengi wamekuwa wakiacha kucheza na kufikia ndoto zao, kwenye michezo kutokana na udhalilishaji
michezoni” amesema mchezaji huyo anaesakata kabumbu katika timu ya wanawake ya Warrious Zanzibar.
Abubakar
Said, ni mchezaji wa mpira wa miguu Timu
ya Muembe Ladu FC, amesema michezo ni afya, ni pesa lakini pia ndio sekta inayoongoza kutoa ajira
Duniani kwa vijana, hivyo ni lazima wachezaji wa soka wakapewa elimu ya
kujikinga na vitendo viovu kama udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.
Amesema
kuwa, ni vyema watoto wakaitumia michezo kama njia ya kujikinga na vitendo vya
Udhalilishaji, kwani vinonekana kuongezeka siku hadi siku.
Nae,
mchezaji wa mpira wa miguu kutoka Timu
ya New Generation, Faidha Juma amesema
ipo haja ya kuitumia michezo kama njia ya kuwalinda watoto, dhidi ya
vitendo vya Udhalilishaji.
Aidha,
ametoa wito Kwa Jamii na wazazi Kwa ujumla, kuwaruhusu watoto wao kushiriki
michezo, mbali mbali tokea wako wadogo
ili kuwasaidia kukuza akili za Watoto,
na kuwafanya wawe wepesi katika
kujifunza.
"Wazazi
tuwaruhusu watoto kushiriki michezo mbali mbali , ili kuwajengea uwezo wa kimwili na kiakili ili wapate kujilinda na vitendo vya Udhalilishaji
Kwani wakiipata elimu hiyo kupitia michezo itawasaidia kujilinda "
ameshauri mchezaji huyo.
Nasra Juma
Mohamed ni Naibu kamishna wa Timu ya Uhamiaji Zanzibar na kocha wa Mpira wa Miguu,
amesema ipo haja Kwa sasa kutokana na hali
ilivyo, kuitumia michezo kama njia ya kujikinga na kujilinda na vitendo vya
Udhalilishaji kwa watoto.
Amesema
kuwa, haiwezi kupita siku bila ya
kusikia watoto wamebakwa au wamelawitiwa, hivyo ni lazima tutafute njia
mbadala ya kujikinga na kukabiliana na hali hiyo..
"Michezo
ni njia moja wapo ya kujikinga na kuwalinda watoto wetu na vitendo vya
Udhalilishaji kwani Watoto wanaoshiriki michezo huwa na uwezo mkubwa wa
kujihami ukilinganisha na wale wasio
shiriki michezo " amesema Kocha Nasra.
Aidha
amesema kuwa, tafiti zinaonesha Kila kwenye watoto watano mmoja kakumbwa na
vitendo vya Udhalilishaji wa kijinsia.
Nae, Kamishna wa Baraza la Michezo Zanzibar,
Mohamed Makame amesema ni vyema Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, ikapanga muda maalumu mashuleni wanafunzi wakafundishwa michezo mbali mbali
wakiwa bado wadogo.
Amesema
kuwa, hiyo itasaidia kuibua vipaji lakini pia , watoto hao kufundishwa michezo
kama njia ya kujikinga na vitendo vya Udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikiongezeka kila uchao.
Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma, alipokuwa
akizindua Mpango Mkakati Jumuishi wa Jinsia katika Michezo Zanzibar wa mwaka
2024/25-2028/29.alisema kuwa Mpango huo, utumike Kama Muongozo wa kujilinda na
vitendo vya udhalilishaji Michezoni.
Amesema
kuwa, Mpango huo umezingatia Usawa wa kijinsia, na Ujumuishi ili kusaidia Utekelezaji wa Dira ya Michezo
ya Zanzibar ya mwaka 2018.
Aidha,
aliishauri Jamii na wanamichezo kuusoma Mpango Mkakati huo, ili kuuelewa, na
wanamichezo kuutumia katika kujilinda na
vitendo vya Udhalilishaji wakiwa
kwenye michezo.
Khairat Haji,
ni Afisa Programu ya Michezo Kwa
Maendeleo kutoka Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar,
(TAMWA ZNZ) akisoma ripoti ya matukio ya Ukatili na Udhalilishaji katika maadhimisho
ya siku 16 za kupinga Udhalilishaji
,aliwataka Watoto wakike na wasichana
kuitumia michezo kama njia moja wapo ya kujikinga na vitendo vya
udhalilishaji.`
Akisoma,
ripoti ya majumuisho ya vitendo vya ukatili na Udhalilishaji , kutoka
January hadi Oktoba mwaka huu,
alisema takwimu za kesi hizo zinaonesha hali ya
kutisha kwa kuongezeka kwa vitendo
hivyo, kati ya kesi 1,582 za ukatili wa kijinsia ziliripotiwa na
waathirika Watoto walikuwa ni 1,337 kati ya hao wasichana walikuwa ni 1,095 na
wavulana 242.
Aidha
alisema kuwa, kesi 693 zilihusisha Watoto wa
umri kati ya miaka 15 hadi16 huku
, akitanabahisha kuwa vitendo hivyo
hufanyika kati ya saa 9:00 na saa tatu usiku , wakati ambao Watoto wengi wapo mazingira ya nyumbani ambapo kuna
usalama, huku wilaya ya Magharibi
‘B’ikiongoza kwa matukio mengi ya
udhalilishaji yakiwa ni 386, ikifuatiwa
na wilaya ya Mjini Unguja ambayo
iliripoti kesi 344 na Magharibi ‘A’
ikiwa na kesi 373.

Post a Comment