FAKIHAT MWANAMKE MWENYE NDOTO YA KUWA KIONGOZI KUWASAIDIA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR

 





Fakihat – “Ulemavu huujazima sauti yangu ya kuwa kiongozi kwa jamii”.

Na - Maryam Nassor.

Zanzibar: ‘’Naumia nikiona watoto wenye ulemavu, hawapewi kipaumbele katika jamii kwani nao, wana haki sawa ya kupewa elimu na kushirikishwa katika  kugombea nafasi za uongozi’’ Anasema Fakihat.

Fakihat Omar Abubakar, 23 ni miongoni mwa watoto wa kike,mwenye ulemavu, ambae ana ndoto kubwa ya kuwa kiongozi ili kuisaidia jamii yake lakini pia, kuwasaidia watu wenye ulemavu.

‘’Bado jamii haitaki kukubali kuwa, Watoto wenye ulemavu wana haki sawa kama binadamu wengine na badala yake wanawekwa ndani na hawapewi haki zao za msingi ’’ Amesema Fakihat kwa masikitiko.  

Katika ulimwengu ambao mara nyingi huhusisha mafanikio na ukamilifu wa kimwili na kiakili ni muhimu kufahamu kuwa kuna watu wenye ulemavu ambao wamevuka changamoto.Hio na kutenda mambo makubwa katika jamii ambayo yanaweza kuwa mfano wa kuigwa duniani. Fakihat Omar Abubakar 23, ni Afisa Tehama katika Ofisi ya Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar – JUWAUZA. Amesema ‘’Watoto wenye ulemavu, bado hawapewi haki yao ya elimu kama watoto wengine, wasio na ulemavu na vigumu kutimiza ndoto zao’’Amesema Fakihat ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya usawa kwa jamii.

Akiwa mtoto wa pili wakike,kati ya watoto watatu wa familia ya Omar Abubakar, anayeishi Tomondo Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.Alizaliwa mwaka 2000 na  alipata ulemavu akiwa mtoto, madaktari walisema alichelewa kulia wakati anazaliwa ndio ikapelekea athari katika ubongo wake na baadhi ya viungo.

Licha ya changamoto hiyo, Fakihat haikumzuia kusoma na kutimiza ndoto zake za kielimu, amesema alipata elimu yake ya maandalizi hadi kidato cha nne katika skuli ya Al falah iliyopo Mombasa mjini Unguja.

Fakihat amesema, elimu  jumuishi kwa watu wenye ulemavu haiko sawa kwa hapa Zanzibar, ambapo alishindwa kufaulu  vizuri ,hii ni kwa sababu hakuweza kuandika vizuri kutokana na mikono yake kutetemeka hivyo, walimu  walishindwa kumzingatia wakati wa usahihishaji wa mitihani kama mtu mwenye ulemavu.

Amesema, baada ya matokea ya mitihani alishindwa kuendelea  na masomo ya elimu ya  juu, na kujiunga na chuo  Cha Mamlaka ya Elimu  na Mafunzo ya Ufundi –VETA ili kusomea ufundi wa maswala ya Tehama.Licha ya mapungufu yake ya kimwili yaliyosababishwa na ugonjwa huo,Fakihat aliendelea kusoma kwa bidii na kuthibitisha kwamba,nguvu za akili zinaweza kuvuka vikwazo vya kimwili.‘’Nilishawahi kupata mafunzo ya uongozi kule Jambiani, na yananisaidia kutetea haki zetu za watu wenye ulemavu’’Amesema.Fakihat.

 Kilichomshawishi kupata mafunzo ya  uongozi  ni kutokana na kuwa, na malengo ya kuwa kiongozi  hapo baadae, ili awasaidie watu wenye ulemavu kwani kuna pengo kubwa analiona.’’ Sisi watu wenye ulemavu bado  kuna pengo ambalo  lipo kwani bado hatuja shirikishwa vilivyo katika kugombea nafasi za uongozi ‘’ Amesema Fakihat ambaye ana ndoto za  kuwa kiongozi, lakini pia anatarajia kuingia katika katika michakato wa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.

“Lengo langu hapo, baadae ni kugombea nafasi za uongozi ili kuwatetea watu wenye ulemavu, katika mambo yanayowahusu lakini pia kuwaletea maendeleo katika jamii kwa ujumla”  amesema Fakihat.

Omar Abubakar ni baba mzazi wa Fakihat, amesema licha ya kuwa na changamoto ya ulemavu  ila amehakikisha anamsaidia binti yake  kutimiza ndoto zake.‘’Kwa kweli najivunia mwanangu, anajitoa sana kwa watu wenye ulemavu na kuitaka jamii, kujua haki za watu wenye ulemavu na kuwasaidia kufikia ndoto za kielimu’’Amemaliza Omar.

Omar amesema kuwa, ni vyema wazazi wawasaidie watoto wao, wote bila ya ubaguzi ili  watimize ndoto zao za kielimu ili kuja kuwa kiongozi wazuri baadae.‘’ Sisi wazazi tuna jukumu kubwa la kutimiza ndoto za watoto wetu, hususani hawa wenye mapungufu ili kuwa viongozi wazuri ’’ Amesema Omar.

Mwana sheria kutoka Jumuiya kwa  ajili ya watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar ZAPDD Halfan Amour amesema, watu wenye ulemavu wana haki sawa na binadamu wengine, ikiwemo haki ya kupatiwa elimu na kushiriki katika kugombea nafasi za uongozi.“Watu wenye ulemavu wana haki zote,sawa na binadamu wengine ikiwemo kupatiwa elimu na kushirikishwa katika kugombea nafasi za uongozi ‘’Amesema Halfan.

Sheria ya watu wenye Ulemavu, namba 6 ya mwaka 2006, imetamka wazi kuwa watu wenye ulemavu wana haki zote za msingi kama binadamu wengine, ikiwemo kupatiwa elimu na haki ya kuwa kiongozi.

Mtaalamu wa maswala ya mawasiliano Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar –JUWAUZA,Hawra Shamte amesema lengo la kwanza la Fakihat  kuletwa ofisini hapo,ilikuwa ni kumuwezesha kujihudumia mwenyewe kwani hapo awali, alikuwa anakaa ndani tu bila ya kutoka  na kujishuhulisha na kazi za kijamii.‘’Lengo kuu la Fakihat lilikuwa ni kuja hapa ofisini, kujichanganja na watu kwani, alikuwa amesoma lakini wazazi wake walikuwa wanaendelea kumlea,hivyo mwenyekiti wa JUWAUZA akaona aletwe hapa ofisini’’ Amesema  Bi Hawra huku akiongeza  kuwa, nafasi ya Fakihat kuja JUWAUZA, amekuwa mweledi kazini na anafanya kazi zake vizuri  , lakini pia na mtetezi wa haki za watu wenye ulemavu Zanzibar.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya  Wanawake  Wenye  ulemavu   Zanzibar- JUWAUZA Salma Saadat, amesema kuwa jamii ibadili mtazamo wao juu ya watu  wenye  ulemavu na kuwapatia  elimu  ili wasome na waje kuwa  viongozi.’’Jamii inapaswa ibadili mitazamo yao kuhusu watu wenye ulemavu na wawaone kama binadamu wengine, na wawape haki zao zote za msingi ikiwemo elimu ili waje kuwa viongozi wazuri baadae’’. Amesema Salma Saadat.

 

 

  

 

No comments

Powered by Blogger.