MIFUMO DUME INAVYOWATESA WANAWAKE KATIKA VYAMA VYA SIASA
NA MARYAM NASSOR
“Niliingia
katika siasa kwa sababu, niliona maswala mengi ya wanawake hayaingii kwenye
sera mipango na bajeti kwa kuwa, nafasi nyingi za maamuzi zimeshikiliwa na wanaume.”
Hii ni kutokana na kushamiri kwa mifumo
dume katika vyama vya Siasa nchini “nilitamani kuingia kwenye uongozi kufanya jambo la ziada kwa
kuhakikisha masuala yanayohusu wanawake na makundi mengine, yanaingia
kwenye sera, mipango na bajeti, binafsi
niliamini kila mwanamke ni
kiongozi, anahitaji tu uthubutu na kuamua kushika hatamu”
amesema Lucy .
Lucy John Mtembo, 40 ni miongoni
mwa wanachama hai wa Chama cha Mapinduzi
-CCM na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
wa Tanzania -UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja.
alianza harakati za siasa miaka
ya 2010, ambapo enzi hizo nafasi za uongozi kama udiwani, Uwakilishi na Ubunge
ulikuwa unashikiliwa na mfumo dume, na wanawake walikuwa ni wapiga debe tu,katika
kampeni.“ Katika maisha nimejifunza kuwa tunapaswa kuwa na uthubutu na utayari
kujifunza mambo mapya na kujiwekea mipango inayotekelezeka ili tuwe viongozi wazuri”
amesema Lucy akionesha msisitizo.
Mwenyekiti huyo, wa Umoja wa Wanawake
Tanzania, kupitia Chama cha Mapinduzi -UWT, chama ambacho hujinasibu kuwepo kwa
usawa wa kijinsia wa viongozi wake kwenye uwakilishi amesema bado wanawake wapo kidogo katika
nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi.” Sisi wanawake tuko wengi kuliko
wanaume,lakini huu wingi wetu hauakisi
bado katika nafasi za uongozi na
vyombo vya maamuzi” amesema Lucy.
Licha ya Tanzania na Zanzibar kuridhia mikataba na matamko mbali mbali
ya kikanda na kimataifa, yenye wito wa usawa katika uwakilishi na ushiriki wa
wanawake na wanaume katika siasa, wanawake bado wana uwakilishi mdogo
katika vyombo vya maamuzi na nafasi za
uongozi, na baadhi ya sababu
zinazochangia hali hii zimetajwa ni mfumo dume, mitazamo hasi ya kibaguzi na
mgawanyo wa majukumu kijinsia.
Takwimu zinaonesha Zanzibar, hadi sasa kuna wanawake nane tu,
waliowahi kugombania nafasi za uongozi majimboni, ambao walishinda uwakilishi,
wanawake 18 walipata uwakilishi kupitia nafasi za viti maalum na hivyo, kufanya
idadi ya wanawake katika Baraza la Wawakilishi kuwa 29 kati ya 77
waliyochaguliwa sawa na asilimia 40.
Fatma Abdul Habib Ferej ni Mwenyekiti wa Ngome ya wanawake wa Chama
Cha ACT Wazalendo , ambae aliwahi kushika
nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
amesema bado wanawake wako kidogo katika
nafasi za uongozi jambo ambalo linahitaji kuangaliwa. “ Licha ya Serikali
kukubali mikataba mbali mbali ya kikanda na kimataifa , ya kuhamasisha usawa wa
kijinsia katika nafasi za uongozi na
vyombo vya maamuzi lakini bado,
ushiriki wa wanawake haujaridhisha” amesema Mwenyekiti huyo wa ngome ya Act Wazalendo.
Amesema katika chama chake cha Act
Wazalendo, wana mabaraza ya wanawake na kamati
kuu ya chama, ambayo yana ushiriki wa wanawake kwa asilimia 52 ya
washiriki wote.“ushiriki sawa wa wanawake katika kufanya maamuzi hauhitaji haki
au demokrasia tu, bali nilazima uonekane kama sharti muhimu la msingi ili maslahi ya wanawake yazingatiwe. “
amesema Mwenyekiti wa Ngome ya Act
Wazalendo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Anna Athanas Paul, amesema tathimini iliyofanywa na wizara hiyo, katika
taasisi mbali mbali imeonesha kuwa wanawake bado wapo kidogo katika nafasi za
Uongozi, ukilinganisha na wanaume jambo ambalo linahitaji kuangaliwa.
‘’Takwimu zilizokusanywa na wizara kutoka taasisi mbali mbali kwa
mwezi machi mwaka 2024, zinaonesha ni asilimi 30 tu ya wanawake ambao wako
katika uongozi, ukilinganisha na wanaume
ambao ni asilimia 70’’ Amesema Naibu Waziri Anna.
Anna, ameongeza kuwa Serikali inaendelea na jitihada katika
kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya 2050 na mpango wa Maendeleo (ZADEP)
2021/2026 ambapo lengo katika nafasi za uongozi ni kufikia 50/50. “ Serikali
imejipanga kuhamasisha ushiriki wa
wanawake katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi na lengo ni kufikia 50/50” amesema Anna.
Ripoti ya sensa ya watu na makaazi ya Tanzania ya mwaka 2022,
inaonesha kuwa Zanzibar ina wakaazi
milioni 1.8 kati ya hao wanaume ni
915,492 na wanawake ni 974,281.hii ina maana kwamba wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa
Zanzibar, lakini wingi huo hauonekani katika nafasi za uongozi.
Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar, - TAMWA
ZNZ ni Taasisi isiyo ya kiserikali, inayojishuhulisha na maswala ya utetezi wa
haki za mtoto wa kike na kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi,
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA ZNZ, Dk Mzuri Issa amesema katika vyama vingi vya siasa nchini,
vimetawaliwa na mfumo dume jambo ambalo linawarudisha nyuma wanawake kugombea nafasi za uongozi.
”Wanawake wenye nia ya kugombea wasivunyike moyo na wawe majasiri
ili kuongeza wingi wao katika nafasi za uongozi mwaka 2025 ili kufikia ile
50/50 tunayoitaka ” Amesema Dkt Mzuri .
Naibu Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania, kwa upande wa Zanzibar
Mohamed Ali Ahmed, amesema kuongezwa kwa
kifungu cha 10 C ndani ya sheria ya vyama vya siasa nchini, kinatoa nafasi kwa
wanawake kuongeza ushiriki wao” Kutokana na kuongezwa kwa kifungu hicho, vyama
vya siasa vitawajibika kwa kuwa na sera ya jinsia kwa muda wote, na kitasaidia
kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi” amemaliza Naibu Msajili huyo.
Post a Comment