TAMWA-ZANZIBAR: ''WANAWAKE JITOKEZENI 2025 MSIJALI VITISHO''
NA MARYAM NASSOR,
ZANZIBAR.
MKURUGENZI wa Chama
cha wandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali,
amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali
za uongozi majimboni, ili kuongeza ushiriki wao bila ya kuogopa
vitisho.
Dk. Mzuri ameyasema hayo leo
Oktoba 1, 2024 ukumbi wa mikutano wa chama hicho Tunguu Unguja, katika kikao
cha kueleza namna gani wanawake watapata ulinzi dhidi ya
ukatili wa kijinsia mitandaoni, kupitia mradi wa wakuwawezesha
waandishi wa habari vijana.
Amesema
kuwa, hamu yao ni kuona wanawake wengi wanaingia majimboni kugombea
nafasi mbali mbali, lakini suala la udhalilishaji mitandaoni, linawarudisha
nyuma.
“Jamii inaamii mtu akitaka kugombea nafasi ya
uongozi ni lazima awe msafi kwa asilimia 100, lakini mwanamke ni binadamu
na hakosi mapungufu,’’alisema.
Amesema kuwa, moja kati ya kikwazo kikubwa kwa
wanawake katika kugombea ni vitisho kutoka wagombea wanaume.
‘’Wanawake musiogope kujitokeza kugombea,
kwani wamekuwa kidogo katika kugombea nafasi za uongozi, wakisumbuliwa na
ukatili wa wa kijinsia mitandaoni lakini musivunjike
moyo,’’alifafanua.
Afisa kutoka Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhuhumu wa uchumi Zanzibar ‘ZAECA’ Yussuf Juma Suleiman, amesema moja kati ya vikwanzo vinavyowarudisha nyuma wanawake katika kugombea nafasi za uongozi ni rushwa ya ngono.
Amesema kuwa, kabla wanawake hawajaingia katika kugombea nafasi za uongozi, ni vizuri kupewa elimu ya uraia, ili kujua miiko na misingi ya uongozi, ili wasiwe na mwanya wa kutoa rushwa.Aidha amesema kuwa, serikali ya Mapinduzi
Zanzibar imepitisha sheria mpya ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi, sheria
namba 5 ya mwaka 2023, kifungu cha 53.
Amesema, kifungu hicho kimeharamisha rushwa ya
ngono, kwa kukataza mtu yoyote kushawishi, kuahidi kufanya ngono na adhabu yake
ni kifungo kisichopungua miaka saba na kisichozidi miaka 10.
“Rushwa ya ngono ni uhalifu kama ulivyo
mwingine, na serikali imeazisha sheria ili kukabiliana nayo, lakini wandishi wa
habari toeni elimu ili wanawake wanaotia nia wasiwe ni mwanya wa kutokea
rushwa,’’ alisema.
Nae Afisa sheria Mwandamizi kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Abdul-razak Said Ali amesema serikali imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali, katika kumuwezesha mwanamke kugombania nafasi za uongozi ili kuongeza ushiriki wao.
Alisema kuwa, moja ya hatua iliyochukuliwa na
serikali ni kuongeza kifungu katika sheria ya vyama vya siasa nambari 1 ya
mwaka 2024, kifungu namba 10 (c) ndani ya marekebisho, kinatoa masharti
yanayohusiana na uanzishwaji wa dawati la kijinsia na ushirikishwaji wa jinsia
na jamii.
Na washiriki wa mkutano huo Mwalim Mwatima
Issa, Rashid alisema wandishi wa habari wanatakiwa kujipa kipaumbele katika
kufanya kazi zao.
Nae mshiriki Nusra Shabani aliuliza kwanini
vyama vidogo vya siasa, havipewi ruzuku ili kuviwezesha vishiriki kikamilifu
katika uchaguzi.
Mwisho




Post a Comment