TAMWA ZNZ, YATAKA ADHABU KALI KWA WATU WANAO WADHALILISHA WATOTO

                

NA MARYAM NASSOR

CHAMA cha wandishi wa habari  wanawake Tanzania Zanzibar,(TAMWA ZNZ) kimeonya kuhusu hali ya kukithiri vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto  na kuomba hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahalifu.

TAMWA ZNZ, Imeeleza kuwa ripoti ya hivi karibuni kutoka Ofisi ya mtakwimu mkuu wa Serikali Zanzibar inaonesha matukio 165 ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa mwezi julai2024, ambapo watoto walikuwa wathirika wakubwa.

Katika ripoti hiyo, watoto walihesabiwa kuwa ni 142, sawa na asilimia 86.1 ya wathirika waote, huku wasichana wakiwa 115( asilimia 81.0) na wavulana 27 ( asilimia 19.0) TAMWA ZNZ, imesema hali hii inahitaji udhibiti mkali kutoka kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na Serikali , taasisi za kijamii, wazee na watoto wenyewe.

''Tunaona hali hii ni mbaya  na ya kusikitisha na inahitaji kudhibitiwa kwa nguvu zote, wasimamizi wa watoto wanapaswa kuhakikisha haki za watoto zinazingatiwa na adhabu kali zinachukuliwa dhidi ya wahalifu  wa vitendo vya ukatili kwa mujibu wa sheria'' wameeleza TAMWA ZNZ.

TAMWA ZNZ, pia imetolea mfano wa tukio la hivi karibuni ambapo mtoto wa miaka miwili alikamatwa pamoja na mlezi wake na watendaji wa Manispa ya Magharibi 'A' kwa kisingizio cha wazazi wake kutolipa ada ya usafi.

'' Kitendo hiki kilizua taharuki kwa famila ya mtoto na jamii kwa ujumla, na kimenda kinyume na haki za mtoto pamoja na haki za binaadamu'' wamesema TAMWA ZNZ.

Sheria ya mtoto ya  Zanzibar Na 6 ya mwaka2011 inapinga udhalilishaji wa watoto wa aina yoyote ile, ili kukuza ustawi wao, aidha mkataba wa kimataifa wa haki za watoto(UNCRC) wa mwaka 1989, ambao Tanzania na Zanzibar wameuridhia , umesisitiza kulinda haki za watoto.

'' Tunatoa wito kwa jamii kuwalinda watoto wetu na pia kuhakikisha hawakumbwi na vitendo  vya udhalilishaji, ni jukumu letu sote  kulinda haki  za watoto na kuhakikisha  wanakuwa katika mazingira  salama '' walisema TAMWAZNZ.

                            MWISHO

No comments

Powered by Blogger.